• HABARI MPYA

    Wednesday, September 10, 2014

    JOHN BOCCO NJE MECHI YA NGAO NA YANGA JUMAPILI, AZAM FC WAINGIA KAMBINI LEO CHAMAZI

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    MSHAMBULIAJI wa Azam FC, John Raphael Bocco ‘Adebayor’ anatakiwa kuwa nje kwa wiki mbili au tatu kuanzia leo kutokana na matatizo ya misuli- maana yake hatacheza mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga SC Jumapili Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Meneja wa Azam FC, Jemadari Said Kazumari ameiambia BIN ZUBEIRY leo asubuhi kwamba, Bocco aliyeumia kwenye michuano ya Kombe la Kagame mwezi uliopita mjini Kigali, Rwanda baada ya kufanyiwa vipimo, ametakiwa kupumzika ili kupona vizuri.

    Atakosekana: John Bocco 'Adebayor' kushoto atakosekana katika mchezo wa Ngao ya Jamii Jumapili 

    MABINGWA WA MECHI ZA NGAO YA JAMII:

    Mwaka  Mshindi Matokeo     
    2001: Yanga SC  2-1 Simba SC
    2009: Mtibwa Sugar  1-0 Yanga SC
    2010: Yanga SC  0-0 Simba (3-1penalti)
    2011: Simba SC   2-0 Yanga SC
    2012: Simba SC  3-2 Azam FC
    2013: Yanga SC 1-0 Azam FC

    “Tuna majeruhi wawili ambao hawatakuwepo kwenye programu ya mchezo wa Ngao ya Jamii, ambao ni beki Waziri Salum na Nahodha wetu, John Bocco,”amesema mshambuliaji huyo wa zamani wa Kariakoo United ya Lindi.
    Bocco aliuamia katika mchezo wa Robo Fainali Kombe la Kagame dhidi ya El Merreikh ya Sudan ambao Azam FC ilitolewa kwa penalti baada ya sare ya 0-0 ndani ya dakika 90.
    Jemadari amesema kwamba, Azam FC itaingia kambini jioni ya leo katika hosteli za Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam kuelekea mchezo huo wa Ngao ya Jamii.
    Wachezaji wengine wote wapo fiti na wamekuwa wakiendelea na mazoezi Uwanja wa Azam Complex na wanatarajiwa kuingia kambini leo.     
    Mabingwa hao wa Tanzania Bara wanaonolewa na kocha Mcameroon, Joseph Marius Omog watamenyana na washindi wa pili, Yanga SC walio chini ya kocha Mbrazil, Marcio Maximo Jumapili Uwanja wa Taifa. 
    Yanga SC nayo inatarajiwa kuingia kambini leo kwa ajili ya mchezo huo, ambao unatarajiwa kuwa marudio ya mchezo wa Ngao ya Jamii mwaka jana timu zilipokutana tena Uwanja wa Taifa.
    Hii itakuwa mara ya tatu mfululizo, Azam FC kucheza mechi ya Ngao ya Jamii na mara zote ikifungwa kwanza na Simba SC na baadaye na Yanga SC- lakini safari hii kocha Omog anataka kupindua matokeo hayo. 
    Yanga SC ndio washindi mara nyingi zaidi wa Ngao, mara ya kwanza wakitwaa mwaka 2001 walipoifunga mabao 2-1 Simba SC, enzi hizo Ligi Kuu inadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia ya Safari Lager. 
    Baada ya hapo, haikuchezwa tena mechi ya Ngao hadi mwaka 2009 wakati Mtibwa Sugar ilipoilaza 1-0 Yanga SC.
    Mwaka 2010 Yanga walirejesha Ngao kwenye himaya yao, baada ya kuwachapa tena wapinzani wao wa jadi, Simba kwa penalti 3-1 kufuatia sare ya bila kufungana ndani ya dakika 90.
    Simba SC walitwaa mara mbili mfululizo Ngao na kufikia rekodi ya watani, kwanza 2011 walipoifunga 2-0 Yanga na 2012 walipotoka nyuma kwa 2-0 na kuilaza Azam 3-2.
    Mwaka jana, Yanga SC ikaweka rekodi ya kuwa timu iliyotwaa mara nyingi zaidi Ngao ya Jamii, baada ya kuilaza 1-0 Azam FC, bao pekee la kiungo Salum Abdul Telela ‘Master’.
    Na mwaka huu, tena Azam FC na Yanga SC zinarudia mechi ya Ngao ya msimu uliopita, zitakapokutana tena Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

    Jumapili patachimbika: Yanga SC nayo inatarajiwa kuingia kambini leo
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: JOHN BOCCO NJE MECHI YA NGAO NA YANGA JUMAPILI, AZAM FC WAINGIA KAMBINI LEO CHAMAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top