Na Mahmoud Bin Zubeiry |
MRISHO
Khalfan Ngassa anatafutwa ili ahusishwe katika mpango wa kuuzwa kwake klabu ya
El Merreikh ya Sudan, lakini hapatikani na simu kazima.
Wakati huo
huo, Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF), chini ya Mwenyekiti wake, Wakili Alex Mgongolwa, inatarajiwa
kukutana leo mjini Dar es Salaam kujadili uhalali wa kuuzwa kwa mchezaji huyo.
Hiyo
inafuatia awali kutokea mgogoro baina ya klabu yake kisheria, Azam FC na Simba
SC alikopelekwa kwa mkopo kuhusu uhalali wa kuuzwa kwake.
Azam wakiwa
wamemtoa kwa mkopo Ngassa, walilalamikiwa na Simba SC kumuuza Merreikh mchezaji
huyo bila kuwashirikisha wao.
Simba
walikuwa wana hoja ya msingi na ndiyo maana busara imetumika, klabu hizo mbili
zimeketi meza moja na kumaliza suala la mchezaji huyo.
Maana yake,
Kamati ya Mgongolwa itakutana kutatua kesi nyepesi tu baada ya Simba SC na Azam
FC kufikia makubaliano ya kumuuza kwa pamoja mshambuliaji huyo kwenda El
Merreikh ya Sudan.
Suluhu hiyo
inakuja baada ya Merreikh kuongeza dau la kumnunua Ngassa kutoka dola za
Kimarekani 70,000 hadi 100,000, zaidi ya Sh. Milioni 150 za Tanzania.
Baada ya
kuongeza dau hilo, Azam ilikutana na Simba kujadili pamoja ofa hiyo mpya na
kukubaliana kumuuza na kugawana nusu kwa nusu.
Upande wa
Azam uliwakilishwa na mmoja wa Wakurugenzi wa bodi ya klabu hiyo, wakati kwa
Simba waliwakilishwa na Makamu wao Mwenyekiti, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’.
Upande wa
maslahi ya mchezaji umeboreshwa pia, Ngassa sasa atapewa dola za Kimarekani
75,000 zaidi ya Sh. Milioni 120,000 kwa kusaini mkataba wa miaka miwili na
mshahara utabaki kuwa dola 4,000 (Sh. Milioni 6).
Habari
zinasema kwamba, baada ya makubaliano hayo, jana Simba na Azam walisaini
mkataba wa kumuuza rasmi mchezaji huyo.
Hata hivyo,
tangu wakati kikao hicho kinaendelea jioni ya juzi, Ngassa alikuwa akitafutwa
ili kuhusishwa, lakini hakupatikana kwenye simu.
Wasiwasi
umeibuka kwamba huenda Ngassa anaweza akawa ameghairi mpango wa kwenda Merreikh
kutokana na ushauri mbaya wa watu wake wa karibu na mchezaji mmoja wa timu ya
taifa, alisema wiki hii kwamba Ngassa anafikiria kuachana na mpango wa kucheza
Sudan, kwa sababu anasikia ni nchi ya Kiislamu na haina starehe.
Ilipofikia
Ngassa anahitaji ushauri nasaha, kwani nafasi aliyopata ni adimu na ni muhimu
kwa taifa na hata kwa maslahi yake binafsi.
Achilia
mbali maslahi mazuri, lakini anakwenda kucheza timu ya ushindani ambayo itakuza
kiwango chake aweze kuisaidia timu ya taifa pia. Merreikh ni timu ambayo karibu
kila mwaka inashiriki Ligi ya Mabingwa.
Ikumbukwe, Azam
walimtoa kwa mkopo Ngassa mwanzoni mwa Agosti, mwaka huu baada ya kukerwa na
kitendo cha mchezaji huyo kubusu jezi ya timu yake ya zamani, Yanga, katika
Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, dhidi
ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Alifanya
hivyo, baada ya kufunga bao la ushindi akitokea benchi na kuiwezesha Azam
kutinga fainali ya michuano hiyo, ambako walifungwa na Yanga 2-0, naye kwa mara
nyingine akitokea benchi na kushindwa kufunga, hivyo kutuhumiwa kucheza kinazi.
Ilielezwa
kwamba Simba walitoa Sh. Milioni 25 kumnunua kwa mkopo mchezaji huyo, ingawa
baadaye Simba wakasema waliununua mkataba wa mwaka mmoja aliobakiza mchezaji
huyo Azam FC, nao wakamuongezea wa mwaka mmoja kwa kumsainisha kwa Sh. Milioni
30, kati ya hizo Milioni 12 akipewa taslimu na 18 akipewa gari.
Vema Simba
na Azam wamemalizana. Nilikuwa nafuatilia sakata la Ngassa kuuzwa kwake, tangu
mwanzoni, nilipokuwa Uganda kwenye Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na
Kati, CECAFA Tusker Challenge.
Nikiwa huko,
nilizungumza na Ngassa baada tu ya kuibuka habari hizo, akasema ni kweli na
yeye amekwishakubaliana na Merreikh kuhusu maslahi yake binafasi na kilichobaki
ni klabu hiyo kongwe ya Sudan kumalizana na klabu zake.
Lakini ajabu
sasa, baada ya klabu zake kumalizana, yeye anakimbia kuhusishwa. Jana
alikaririwa na kituo kimoja cha Radio akisema anakwepa kwa sababu Simba na Azam
zinataka kumuuza kama mzigo, bila kumhusisha na hajui chochote.
Kwanza hili
si kweli- Ngassa anajua hili dili vema, kwa sababu Waandishi wengine wa
Tanzania walizungumza naye pia Uganda na akatoa ufafanuzi mzuri tu.
Lakini hata
tukisema tukubaliane na Ngassa kwa anachosema, hajui- inakuwaje sasa anaitwa
kushirikishwa hapatikani?
Kama kipo
kitu Ngassa anahitaji juu ya ile ofa iliyotolewa kwake Merreikh, vema angeibuka
kukutana na klabu zake, akatoa dukuduku lake, lakini kujificha si jibu na ni
utoto.
Hakuna
sababu ya Ngassa kusumbua vichwa vya watu wazima, kama suala ni maslahi
haridhishwi nayo atoe pendekezo lake, na kama Merreikh wakishindwa biashara
ife.
Merreikh ni
klabu kubwa, ambayo ina uwezo wa kusajili mchezaji yoyote barani Afrika
inayemtaka, Ngassa anatakiwa kujua hilo.
Merreikh ni
heshima kwa Ngassa na nafasi zaidi ya kukuza kiwango chake kwa kucheza
mashindano makubwa, kama ilivyo kwa wenzake Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu
ambao tumewashuhudia mwaka huu wakicheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa
Afrika na klabu yao, TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Lakini pia
maslahi ya kule ni makubwa mno, mbali na mshahara wa Sh. Milioni 6, kule kuna
bonasi nyingi mno anapocheza na kufanya vizuri katika mashindano, hususan ya
Ligi ya Mabingwa.
Kila bao
atakalofunga Ngassa katika Ligi ya Mabingwa ni fedha kwake. Kila mechi
watakayoshinda au kutoa sare, Ngassa anaingiza fedha. Lakini pia, Ngassa
anajiweka sokoni zaidi kwa kucheza kule, kwani atakuwa akionekana akicheza Ligi
ya Mabingwa kila msimu na kujitengenezea mazingira ya kutimiza ndoto zake za
muda mrefu, kucheza Ulaya.
Sijui
nielezee nini katika hili, maana inafikia wakati nashindwa kuelewa kilicho
nyuma ya Ngassa katika sakata hili, kama ni ujinga au weledi zaidi.
Hizi habari
za kwamba hataki kwenda Sudan kwa sababu hakuna starehe, kwanza sitaki
kuziamini sana, lakini hata kama ni kweli pia, Ngassa anataka kustarehe kwa
kiwango gani zaidi ya kufanya kazi kwa sasa ili kujiandalia maisha yake ya
baadaye akistaafu soka?
Wachezaji
wakubwa waliocheza Ulaya kama Celestine Babayaro aliyewika Cheslea, sasa analia
hali ngumu ya kiuchumi, miaka michache tangu astaafu, je Ngassa anaingaliaje
kesho yake?
Nani mshauri
wa Ngassa kwa sasa. Nitafurahi nikijua baadaye, Ngassa alikuwa anakwepa dili ya
Merreikh ili akamate dili nyingine ya maana ya maslahi mazuri kuliko hiyo,
lakini ikija kuwa ni upuuzi, kwa kweli nitakuwa sehemu ya Watanzania
watakaoanza kumdharau Mrisho.
Yote kwa
yote, Mrisho ni mtu mzima mwenye akili zake timamu, ambaye anapaswa kujiamini
na kuwa wazi, kuliko kuwa na kauli mbilimbili. Sitaki kuamini eti Azam wana
shida ya fedha kiasi cha kutaka kumuuza Ngassa bila ridhaa yake. Na sitaki
kuamini Simba wanataka fedha kuliko Ngassa mwenyewe.
Lakini sioni
kama ni vema kwa Ngassa kuibuka na kutoa kauli ambazo zina mwelekeo wa
kuwachafulia majina Wakurugenzi wa Azam. Ngassa ana mkataba na Azam, yupo kwa
mkopo Simba SC, ambao ameuongezea mkataba wa mwaka mmoja. Hayo yako wazi.
Hata
ajifiche vipi, mwisho wa siku, atatakiwa kuripoti kituo chake cha kazi, Simba
SC na asipofanya hivyo, mamlaka za soka zinaweza kuidhinisha adhabu
itakayotolewa dhidi yake.
Hakuna
mchezaji duniani anaweza kuuzwa bila ridhaa yake- hata kama awe mzigo kwenye
klabu, ataendelea kukaa benchi akila manufaa ya mkataba wake, hata Ngassa
anaweza kusema hataki kuuzwa ili autumikie mkataba wake hadi uishe. Sasa kwa
haya yote, Ngassa anajificha ili iweje kama si utoto tu? Tujadili waungwana.