Kikosi cha Zanzibar kilichocheza Challenge Uganda |
Na Mwandishi Wetu,
Zanziabr
NAHODHA wa
Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ni
miongoni mwa wachezaji 16, waliofungiwa kwa muda usiojulikana kucheza soka popote
duniani na Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), ambacho pia kimeivunja rasmi timu ya taifa,
Zanzibar Heroes kwa tuhuma ya utovu wa nidhamu.
Akitangaza
maamuzi ya kikao cha Kamati Utendaji ya ZFA kilichofanyika leo mchana ofisi za chama
hicho zilizopo Kiembe Samaki, nje kidogo ya mji wa Zanzibar, Makamu wa Rais wa
ZFA Unguja, Alhaj Haji Ameir, alisema Wajumbe wote wa Kamati ya Utendaji
waliohudhuria kikao wameunga mkono hatua hiyo, ili iwe fundisho kwa wachezaji
wengine.
Kikao hicho
cha dharura kimekuja kufuatia sakata la wachezaji wa Zanzibar Heroes kuamua kugawana
kiasi cha dola za Kimarekani 10,000 walizopata baada ya kushika nafasi ya tatu
katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker
Challenge iliyomalizika wiki iliyopita mjini Kampala, Uganda, kufuatia kuifunga
Bara, Kilimanjaro Stars kwa penalti 6-5, baada ya sare ya 1-1.
Inadaiwa
kuwa wachezaji hao waliamua kugawana fedha hizo kwa madai kuwa wamekuwa
wakidhulumiwa fedha zao na ZFA.
Hata hivyo
katika ufafanuzi uliotolewa leo na Katibu Mkuu wa ZFA Taifa, Kassim Haji Salum,
amesema haijawahi kutokea wachezaji wa timu hiyo kudhulumiwa haki yao
akikumbushia fedha za zawadi walizopata mwaka 1995 katika mashindano kama haya
yaliyofanyika nchini Uganda na Zanzibar ikafanikiwa kutwaa ubingwa na mwaka
2009 waliposhika nafasi ya tatu na mara zote walipewa stahili zao.
Kwa upande
wake, Kocha Mkuu wa Zanzibar, Salum Bausi ambaye jana alitangaza rasmi
kujiuzulu kuifundisha timu hiyo, amesema hatua hiyu ni sahihi kabisa kwa sababu
kitendo hicho kimewafedhehesha wadau wa soka na Wazanzibari kwa ujumla.
Tayari ZFA
Taifa walikwishatuma barua rasmi kwa TFF juu ya hatua hiyo huku nakala ya barua
hizo zikitarajiwa kusambazwa kwa vilabu wanavyochezea wachezaji hao.
Wachezaji
wanne walionusurika na adhabu hiyo ni wale walioamua kuzirejesha fedha hizo
ambao majina yao hayakutatwa kwa sababu maalum, hata hivyo taarifa zilizopo ni
kuwa wachezaji hao wanatoka katika klabu ya Kipanga timu inayomilikiwa na JWTZ,
Jamhuri, Zimamoto na KMKM.
Kikosi cha
Zanzibar kilichokwenda Challenge ni makipa; Mwadini Ali (Azam), Suleiman Hamad
(Black Sella), Abdalla Juma (Kipanga), mabeki; Nassor Masoud 'Chollo' (Simba),
Samir Haji Nuhu (Azam), Aggrey Morris (Azam), Nadir Haroub Ali 'Canavaro'
(Yanga), Aziz Said Ali (Kmkm), Mohammed Juma Azan (JKU) na Ali Mohammed Seif
(Mtende Rangers).
Viungo ni;
Hamad Mshamata (Chuoni), Ali Bakar (Mtende Rangers), Is-haka Mohammed (JKU),
Twaha Mohammed(Mtibwa Sugar), Suleiman Kassim 'Selembe' (Coastal Union), Saad
Ali Makame (Zanzibar All Stars), Makame Gozi (Zimamoto), Issa Othman Ali
(Miembeni), Aleyuu Saleh (Black Sella), Khamis Mcha Khamis 'Viali' (Azam) na washambuliaji;
Amir Hamad (JKT Oljoro), Jaku Juma Jaku (Mafunzo), Abdallah Othman (Jamhuri),
Nassor Juma (JKU) na Faki Mwalim (Chipukizi).