TIMU ya Simba SC imerejea kileleni mwa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Dodoma Jiji FC usiku huu Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam.
Pongezi kwa mfungaji wa bao hilo pekee la Wekundu wa Msimbazi winga Mkongo, Elie Mpanzu Kibisawala dakika ya 63 na kwa ushindi huo Simba SC imefikisha pointi 58 katika mchezo wa 25 na kurejea kileleni ikiwazidi pointi moja mabingwa watetezi, Yanga SC ambao pia wana mchezo mmoja mkononi.
Kwa upande wao Dodoma Jiji FC baada ya kupoteza mchezo huo wanabaki na pointi zao 33 za mechi 25 pia nafasi ya nane kwenye Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara inayoshirikisha timu 16.
Ikumbukwe mwisho wa msimu timu mbili zitashuka Daraja moja kwa moja, wakati nyingine mbili zitakazomaliza nafasi ya 14 na 13 zitamenyana baina yao kwa mechi mbili za nyumbani na ugenini na mshindi wa jumla atasalia Ligi Kuu.
Timu itakayofungwa itakwenda kumenyana na timu kutoka Ligi ya Championship katika mechi nyingine mbili za mchujo nyumbani na ugenini na mshindi wa jumla ndiye atacheza Ligi Kuu msimu ujao.



.png)
0 comments:
Post a Comment