TIMU ya Azam FC imetumia vyema Uwanja wa nyumbani, Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam kwa kuichapa Pamba Jiji FC ya Mwanza mabao 2-0 katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara.
Pongezi kwa wafungaji wa mabao hayo, kiungo Feisal Salum Abdallah dakika ya 90 na mshambuliaji Mkongo, Jephte Kitambala Bola dakika ya 90’+4 na kwa ushindi huo, Azam FC wanafikisha pointi 46, ingawa wanabaki nafasi ya tatu nyuma ya Simba SC yenye pointi 52 na mabingwa watetezi, Yanga pointi 54 baada ya timu zote kucheza mechi 23.
Kwa upande wao Pamba Jiji FC baada ya kupoteza mchezo huo wanabaki na pointi zao 30 za mechi 23 nafasi ya nane kwenye ligi ya timu 16, ambayo mwisho wa msimu mbili zitashuka Daraja.
Timu nyingine mbili zitakazomaliza nafasi ya 14 na 13 zitamenyana baina yao kwa mechi mbili za nyumbani na ugenini na mshindi wa jumla atasalia Ligi Kuu.
Timu itakayofungwa itakwenda kumenyana na timu kutoka Ligi ya Championship katika mechi nyingine mbili za mchujo nyumbani na ugenini na mshindi wa jumla ndiye atacheza Ligi Kuu msimu ujao.


.png)
0 comments:
Post a Comment