WENYEJI, Tanzania Prisons wameibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Fountain Gate FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara mchana wa leo Uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya.
Pongezi kwa mfungaji wa bao hilo pekee, George Mpole Mwaigomole dakika ya 25 na kwa ushindi huo Tanzania Prisons wanafikisha pointi 17, ingawa wanabaki nafasi ya 15 kwenye ligi ya timu 16 mbele ya KMC FC inayoshika mkia kwa pointi zake tisa baada ya timu zote kucheza mechi 23.
Kwa upande wao, Fountain Gate baada ya kupoteza mchezo huo wanabaki na pointi zao 25 kufuatia kucheza mechi 23 na wanashuka kwa nafasi moja hadi ya 11.
Ikumbukwe mwisho wa msimu timu mbili zitashuka Daraja na mbili zitakazomaliza nafasi ya 14 na 13 zitamenyana baina yao kwa mechi mbili za nyumbani na ugenini na mshindi wa jumla atasalia Ligi Kuu.
Timu itakayofungwa itakwenda kumenyana na timu kutoka Ligi ya Championship katika mechi nyingine mbili za mchujo nyumbani na ugenini na mshindi wa jumla ndiye atacheza Ligi Kuu msimu ujao.



.png)
0 comments:
Post a Comment