TIMU ya Arsenal imefanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya England nje ya Uwanja baada ya waliokuwa mabingwa watetezi, Manchester City kulazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na wenyeji, AFC Bournemouth usiku wa Jumanne (Mei 19, 2026) Uwanja wa Vitality, Boscombe, Bournemouth, Dorset.
Linakuwa taji la 14 kwa Washika Bunduki hao wa London na la kwanza tangu msimu wa 2003–04 – huku mengine ikiyabeba katika misimu ya 1930–1931, 1932–1933, 1933–1934, 1934–1935, 1937–1938, 1947–1948, 1952–1953, 1970–1971, 1988–1989, 1990–1991, 1997–1998 na 2001–2002.
Katika mchezo ulioipa ubingwa wa kwanza Arsenal baada ya miaka 22 – wenyeji walitangulia kwa bao la mshambuliaji Mfaransa, Eli Junior Éric Anatole Rainha Kroupi anayezaliwa na baba, mwanasoka wa zamani wa KImatafa wa Ivory Coast na mama Mreno aliyefunga dakika ya 35.
Manchester City ikafanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya 90’+5 kupitia kwa mshambuliaji wake tegemeo, Mnorway Erling Braut Haaland, ingawa haikuzuia Arsenal kumaliza ukame wa miaka 22 wa kutwaa taji la Ligi Kuu ya England.
Arsenal imefikisha pointi 82 baada ya kucheza mechi 37 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine.
Manchester City inafuatia kwa pointi zake 78, Manchester United pointi 68, Aston Villa pointi 62 na Liverpool pointi 59 ambazo zote zinafuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kocha Mspaniola, Mikel Arteta Amatriain ambaye aliichezea The Gunners kuanzia 2011 hadi 2016 anaipa Arsenal ubingwa wa Ligi Kuu ya England baada ya takriban miaka sita na nusu tangu awasili Desemba 22, mwaka 2019 akitokea Manchester City, ambako alikuwa Msaidizi wa Mspaniola mwenzake, Pep Guardiola.
Kwake linakuwa taji la nne kuipa Arsenal kama mchezaji baada ya awali Kombe la FA msimu wa 2019-2020 na Ngao ya Jamii mara mbili, 2020 na 2023 – idadi sawa na mataji aliyoshinda wakati akiwa mchezaji, aliposhinda Kombe la FA mara mbili 2013-2014 na 2014 2015 na Ngao ya Jamii mara mbili pia, 2014 na 2015.
Arsenal ina nafasi ya kushinda taji lingine kabla ya kufunga msimu itakapomenyana na Paris Saint-Germain katika Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya Jumamosi ya Mei 30, 2026 Uwanja wa Puskás Aréna Jijini Budapest nchini Hungary.



.png)
0 comments:
Post a Comment