• HABARI MPYA

    Thursday, May 21, 2026

    SIMBA SC YAICHAPA COASTAL UNION 2-1 NA KUPANDA KILELENI LIGI KUU



    TIMU ya Simba SC imerejea kileleni mwa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya wenyeji, Coastal Union usiku huu Uwanja wa Mkwakwanin Jijini Tanga.
    Haukuwa ushindi mwepesi kwa Wekundu wa Msimbazi, kwani ilibidi watoke nyuma baada ya Coastal Union kutangulia na bao la mshambuliaji wake tegemeo, Maabad maulid Maabad dakika ya nane.
    Hata hivyo, Simba ikapata mabao mawili ndani ya dakika saba kupitia kwa Mawinga wake wapya, Msenegal Libasse Gueye dakika ya 37 na Muivory Coast, Alain Anicet Oura dakika ya 44 wote wakinufaika na kazi nzuri ya kiungo Mzambia, Clatous Chota Chama.
    Kwa ushindi huo, Simba SC inafikisha pointi 55 katika mchezo wa 24 na kurejea kileleni mwa Ligi Kuu ikiwazidi pointi moja mabingwa watetezi, Yanga SC ambao hata hivyo wana mchezo mmoja mkononi na kesho wanacheza na Singida Black Stars Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam.
    Kwa upande wao Coastal Union baada ya kupoteza mchezo huo wanabaki na pointi zao 25 kufuatia kucheza mechi 24 pia wakisalia nafasi ya 12 kwenye ligi ya timu 16.
    Ikumbukwe mwisho wa msimu timu mbili zitashuka Daraja moja kwa moja, wakati nyingine mbili zitakazomaliza nafasi ya 14 na 13 zitamenyana baina yao kwa mechi mbili za nyumbani na ugenini na mshindi wa jumla atasalia Ligi Kuu.
    Timu itakayofungwa itakwenda kumenyana na timu kutoka Ligi ya Championship katika mechi nyingine mbili za mchujo nyumbani na ugenini na mshindi wa jumla ndiye atacheza Ligi Kuu msimu ujao.  

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC YAICHAPA COASTAL UNION 2-1 NA KUPANDA KILELENI LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top