• HABARI MPYA

    Thursday, May 31, 2018

    TSHISHIMBI, AJIB, KAMUSOKO WAENDA NA YANGA SC NAKURU

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    VIUNGO Ibrahim Ajib, Thabani Kamusoko na Papy Kabamba Tshishimbi ni miongoni mwa wachezaji 20 wanaotarajiwa kusafiri na kikosi cha timu hiyo mchana wa leo kwenda mjini Nakuru nchini Kenya kwenye michuano ya SportPesa Super Cup.
    Pamoja na mzawa Ajib, Mzimbabwe na Tshishimbi kutoka Jamhuri ya Kidemokrsia ya Kongo (DRC) kuwemo kwenye kikosi hicho, lakini mshambuliaji Mzambia, Obre Chirwa hayumo. 
    Kikosi cha Yanga kinachoondoka mchana wa leo kinaundwa na kipa Mcameroon Youthe Rostand, mzawa Ramadhani Kabwili, mabeki Hassan Kessy, Mwinyi Hajji Mngwali, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ na Pato Ngonyani.

    Papy Kabamba Tshishimbi ni miongoni mwa wachezaji 20 wanaokwenda Nakuru na Yanga

    Viungo ni Baruan Akilimali, Pius Buswita, Ajib, Maka Edward, Kamusoko, Juma Mahadhi, Said Juma ‘Makapu’, Said ‘Ronaldo’ Mussa, Tshishimbi, Yussuf Mhilu na Raphael Daudi, wakati washambuliaji ni Yohana Oscar Nkomola, Matheo Anthony na Mrundi Amissi Tambwe.
    Yanga watafungua dimba na Kakamega Homeboys Jumatatu, siku moja baada ya mahasimu wao, Simba SC kumenyana na Kariobangi Sharks Jumapili, mechi zote zikichezwa Uwanja wa Afraha, Nakuru.
    Mabingwa watetezi, Gor Mahia wao pia wataanza na JKU Jumapili, wakati Singida United itaanza na AFC Leopards Jumanne. 
    Ikumbukwe bingwa wa michuano hiyo ataondoka kitita cha dola za Kimarekani, 30,000, mshindi wa pili dola 10,000, wa tatu dola 7,500 zitakazoishia Nusu Fainali dola 5,000 na za Robo Fainali dola 2,500.
    Pamoja na dola 30,000, bingwa wa michuano hiyo kwa mwaka huu atapata fursa ya kwenda kumenyana na klabu ya Everton Uwanja wa Goodison Park mjini Walton, Liverpool nchini England.
    Mwaka jana Gor Mahia ilikuwa bingwa wa kwanza wa michuano hiyo baada ya kuwafunga mahasimu wao, AFC Leopard 2-1 katika fainali kwenye michuano iliyofanyika Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TSHISHIMBI, AJIB, KAMUSOKO WAENDA NA YANGA SC NAKURU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top