• HABARI MPYA

    Wednesday, May 23, 2018

    SHAABAN IDDI CHILUNDA ASEMA KAMA SI MAUMIVU ASINGESHIKIKA MSIMU HUU

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MSHAMBULIAJI wa Azam FC, Shaaban Idd, amesema kuwa kuwa nje ya dimba kwa takribani miezi saba akiuguza maumivu ya nyonga kulimharibia kuendeleza kasi aliyokuwa nayo msimu uliopita.
    Mwishon mwa wiki, Shaaban aliiongoza Azam FC kuichapa Tanzania Prisons mabao 4-1 kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara akifunga mabao matatu peke yake na lingine likifungwa na kiungo Frank Domayo.
    Mara baada ya Shaaban kukosa raundi ya kwanza ya ligi kutokana na maumivu aliyopata mwishoni mwa msimu uliopita, hivi sasa amerejea vema kabisa baada ya hat-trick hiyo kumfanya akikishe mabao nane kwenye ligi msimu huu, huku akiandika rekodi ya kufunga mabao sita ndani ya mechi nne zilizopita.

    Shaaban Idd amesema maumivu ya nyonga yamemrudisha nyuma 

    Mabao hayo nane yamemfanya kuvunja rekodi yake ya msimu uliopita alipopandishwa timu kubwa akitokea Azam B, na kufunga mabao sita kwenye msimu wake wa kwanza wa ligi.
    Akizungumza jana mjini Dar es Salaam, Shaaban alisema ilimlazimu kuvuta subira ili kurejea kwenye ubora wake na anamshukuru Mwenyezi Mungu hivi sasa ameanza kufanya vizuri huku akiahidi makubwa zaidi msimu ujao.
    “Mimi sikuanza msimu kwenye raundi ya kwanza ila nimerudi raundi ya pili, nimekaa nje ya dimba zaidi ya miezi sita kwa hiyo nipate ile kasi yangu ambayo nilimaliza nayo msimu ulioisha ilibidi ichukue muda na lazima iwe hivyo kwa sababu mpira ni mchezo unaohitaji utulivu wa akili, utimamu wa mwili.
    “Miezi sita si midogo kwa sababu sikuruhusiwa hata kugusa mpira, haikuwa na maana kwamba kiwango changu kimeshuka bali nilikuwa kwenye njia ya kunifanya mimi nifanye kazi kwa bidii ili kurejea katika kiwango ambacho nilikuwa nacho, namshukuru Mungu nimejitahidi na ndio kama unavyoona nimechanganya kwenye mechi za mwisho,” alisema.
    Mshambuliaji huyo ambaye mpaka sasa msimu huu ameshafunga mabao tisa kwenye mashindano yote, hakusita kuelezea furaha yake baada ya kuwa na muendeleza mzuri wa kufunga mabao, katika mechi nne zilizopita akiwa ametumbukia nyavuni mara sita.
    “Ni rekodi nzuri pia mwenyewe nimeifurahia, kila mchezaji ambaye anapenda maendeleo yake na timu yake lazima acheze kwa rekodi inshallah Mungu akijalia naahidi kufanya kazi nzuri zaidi kwa ajili ya timu yangu,” alisema.
    Shaaban amebakisha bao moja tu kufunga ili kufikia rekodi yake ya msimu uliopita, alipomaliza akiwa amefunga mabao 10 kwenye mashindano yote, sita kwenye ligi, moja Kombe la Mapinduzi na matatu Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) akimaliza nyuma ya aliyekuwa Nahodha wa timu hiyo, John Bocco ‘Adebayor, aliyefunga 12 na kuwa kinara wa ufungaji ndani ya Azam FC.
    Mshambuliaji huyo ambaye huitwa mara kwa mara kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ chini ya Kocha Mkuu, Salum Mayanga, aliwageukia mashabiki wa Azam FC na kuwaambia kuwa wawe na uvumilivu kwa wachezaji huku akiwataka waendelea kuisapoti timu.
    “Mashabiki wawe na uvumilivu na wazidi kutusapoti kwa sababu hii ndio timu yao na sisi ndio wachezaji wao, kwenye shida na raha wazidi kuwa pamoja nasi,” alimalizia.
    Mara baada ya mchezo wa jana, kikosi cha Azam FC kimefikisha jumla ya pointi 55 kikiwa nafasi ya pili kwenye msimamo, kikiizidi Yanga pointi saba ambayo ina mechi mbili mkononi, huku Simba ikiwa tayari imeshatangaza ubingwa ikiwa nazo 68.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SHAABAN IDDI CHILUNDA ASEMA KAMA SI MAUMIVU ASINGESHIKIKA MSIMU HUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top