• HABARI MPYA

    Sunday, May 27, 2018

    MCHAKATO WA MABADILIKO YA KATIBA SIMBA SC HAUKUZINGATIA TARATIBU NA DEMOKRASIA

    WANACHAMA wa Simba SC wamekubali kuingia katika mfumo mpya wa uendeshaji wa klabu yao baada ya kuridhia Katiba mpya inayowaingiza kwenye mfumo wa hisa.
    Hayo yalifikiwa katika mkutano maalum wa kupitisha mabadiliko ya katiba ya Simba SC kuingia kwenye mfumo wa soko la hisa, uliofanyika ukumbi wa mikutano wa Mwalimu Nyerere Jumapili ya wiki iliyopita mjini Dar es Salaam.
    Katika mkutano huo uliohudhuriwa na wanachama 1,000 na ushei ukiongozwa na Kaimu Rais, Salim Abdallah ‘Try Again’ na kuhudhuriwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, marekebisho ya Katiba ya Simba SC yalipita kwa kishindo, wanachama watatu tu wakinyoosha mikono kupinga.

    Katika marekebisho hayo, Bodi ya Wakurugenzi wa Simba SC chini ya Mwenyekiti ambaye pia atakuwa Rais wa klabu, atatakiwa kuwa na elimu ya kiwango cha Shahada sawa na Wajumbe wake wawili wa kuchaguliwa – na Mwenyekiti huyo atakuwa na mamlaka ya kuteua Wajumbe wengine wawili, mmoja mwanamke.
    Kupitishwa kwa mabadiliko ya katiba ndani ya Simba kunafungua milango ya mfanyabiashara Mohammed ‘Mo’ Dewji kuwa mwanahisa mkuu wa klabu.
    Hiyo ni baada ya Mo Dewji, Mbunge wa zamani wa Singida Mjini, kukubali kununua asilimia 49 za hisa za klabu ya Simba SC kulingana na maelekezo ya Serikali badala ya asilimia 51 alizotaka yeye awali katika mkutano Desemba 3, mwaka jana, ambao uliazimia kumfanya mwanahisa mkuu wa klabu katika mfumo mpya wa uendeshwaji.
    Mo pekee aliweka dau la Sh Bilioni 20 kuomba asilimia 50 ya hisa, baada ya klabu kutangaza kuuza asilimia 50 ya hisa zake kwa Sh. Bilioni 20 miezi miwili iliyopita, ingawa baadaye Serikali ikaagiza klabu hiyo isiuze zaidi ya asilimia 49 kwa mtu mmoja.
    Wanachama 1320 walihudhuria mkutano huo wa Desemba 3, mwaka jana kutoka Dar es Salaam na mikoa jirani na kwa furaha ya ushindi huo, Mo Dewji alitoa ahadi 10 za kuleta mabadiliko makubwa, ikiwemo ujenzi wa Uwanja wa mazoezi wa nyasi za asili na nyasi bandia pamoja na hosteli ya kisasa ya wachezaji.
    Mkutano huo ulitanguliwa na mikutano kadhaa ya matawi kutoa elimu kwa wanachama juu ya muundo mpya wa klabu iliyofanyika Dar es Salaam na mikoa jirani.
    Mimi ni muumini wa mabadiliko katika klabu kongwe za soka nchini, Simba pamoja na watani wao wa jadi, Yanga – lakini pia ni muumini wa utaratibu. Napenda mambo kufanyika kwa taratibu ili kuweka kumbukumbu nzuri za michakato.
    Michakato ya aina hii inapendeza kufanyika katika misingi ya demokrasia na uwazi wa kutosha ili kuondoa mambo kama yanayoanza kutokea sasa kwa baadhi ya wanachama, tena mashuhurin kuibuka kupinga.
    Simba ina wanachama zaidi ya 20,000 kwa sasa, lakini Katiba mpya imepitishwa na wanachama 1,000 na ushei tu – haya ni mapungufu makubwa na yanaanzia katika namna ambavyo mchakato wenyewe uliendeshwa.
    Unapowaita watu 20,000 katika eneo ambalo halina uwezo wa kukutanisha kwa pamoja watu angalau 2,000, mosi huo ni mzaha, lakini pili unapaswa kujipima na wewe mwenyewe uliyeamua hivyo.
    Takwimu zinaonyesha mkutano wa Desemba 3 ulivituia watu zaidi na wengine wakakosa nafasi ya kuingia japo ukumbini – wazi kuupeleka mkutano mwingine pale ni kuwazuia hata wengine waliojitokeza awali kwenda tena.
    Katika hali ya kawaida Simba SC ilihitaji kuweka rekodi ya kuvutia wanachama wake wengi katika mkutano, katika eneo kubwa ili mabadiliko ya Katiba yapite kwa rekodi nzuri ya kihistoria. Haikuwa hivyo.
    Lakini pamoja na kukutanisha wanachama wachache tu, hata misingi ya kidemokrasia haikuzingatiwa ukumbini mfano katika zoezi la kupiga kura kuunga mkono au kukataa mabadiliko, wanachama waliambiwa wainue mikono kukubali, wasiinue kupinga na eti hapo mchakato ukawa umekamilika na mabadiliko yamepita.
    Uongozi unaoweza kuamua kwa urahisi mambo mazito kama hayo hata tena mbele ya viongozi wetu wa Serikali ni wa kutilia shaka juu ya mapenzi yao kwa klabu.
    Mchakato wa mabadiliko hauishii tu kwa nani anapewa umiliki wa klabu kununua hisa nyingi, lakini pia tunapaswa kufikiria kwa mapana marefu juu ya mustakabali wa klabu huko inapoelekezwa na kwa hao inaopelekewa.
    Najua kwa sasa Simba SC wanachofikiria ni ofa za Mo Dewji kwa matamanio ya kuiona klabu yao inakuwa kubwa na yenye mafanikio – na ni kwa sababu hiyo michakato inakimbizwa ili mambo yakamilike Mo Dewji akabidhiwe hisa zake klabu iingie katika zama mpya.    
    Lakini upande wa pili wa shilingi, kama mambo yataendelea kufanyika ‘kimagumashi’ kama kupitisha Katiba kwa vidole juu, huo utakuwa mchakato wasiwasi na mbele ya safari unaweza kukwamishwa kwa urahisi tu – kwa sababu tu taratibu hazikufuatwa.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MCHAKATO WA MABADILIKO YA KATIBA SIMBA SC HAUKUZINGATIA TARATIBU NA DEMOKRASIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top