• HABARI MPYA

    Tuesday, May 29, 2018

    SIMBA NA YANGA ZAENDA KUTAFUTANA KENYA KWA MECHI YA NNE YA MSIMU

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MAHASIMIU wa jadi katika soka ya Tanzania, Simba na Yanga wanaweza kukutana kwa mara ya nne msimu huu kwenye Nusu Fainali ya michuano ya SportPesa Super Cup nchini Kenya.
    Hiyo ni kama vigogo hao wa soka ya Tanzania watashinda mechi zao za kwanza za michuano hiyo wakianzia Robo Fainali, Simba SC wakimenyana na Kariobangi Sharks Juni 3 na Yanga na Kakamega Homeboys Juni 4, mechi zote zikichezwa Uwanja wa Afraha, Nakuru.
    Kwa msimu huu, tayari Simba na Yanga zimekutana mara tatu, kwanza katika Ngao ya Jamii Agosti 23, mwaka 2017 ambayo Simba ilishinda kwa penalti 5-4 baada ya sare ya 0-0.
    Siku hiyo waliofuga penalti walikuwa ni Papy Kabamba Tshishimbi, Thabani Kamusoko, Donald Ngoma na Ibrahim Ajib kwa upande wa Yanga na Method Mwanjali, Emmanuel Okwi, Haruna Niyonzima, Shiza Kichuya na Mohammed Ibrahim ‘Mo’ kwa Simba.

    Waliokosa walikuwa ni Kevin Yondan na Juma Mahadhi kwa upande wa Yanga na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ kwa upande wa Simba
    Baada ya hapo wababe hao wakakutana katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Oktoba 28, 2017 na kumalizan akwa sare ya 1-1, Simba wakitangulia kwa bao la Shiza Kichuya dakika ya 57, kabla ya Obrey Chirwa kuisawazishia Yanga dakika ya 60.
    Mechi ya mwisho kuzikutanisha timu hizo ilifanyika Aprili 29, mwaka huu nao pekee la beki anayeweza kucheza kama kiungo pia, Erasto Edward Nyoni dakika ya 37 likaipa Simba SC ushindi wa 1-0, mechi zote hizo zikichezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Mbali na Simba na Yanga, timu nyingine zinazotarajiwa kucheza michuano hiyo ni mabingwa watetezi, Gor Mahia FC, AFC Leopards, Kariobangi Sharks, Kakamega Homeboyz za Kenya, Singida United FC na JKU za Tanzania pia.
    Gor Mahia itafungua dimba JKU Juni 3, wakati Singida United itaanza na AFC Leopards Juni 5 na ikumbukwe bingwa wa michuano hiyo ataondoka kitita cha dola za Kimarekani, 30,000, mshindi wa pili dola 10,000, wa tatu dola 7,500 zitakazoishia Nusu Fainali dola 5,000 na za Robo Fainali dola 2,500.
    Pamoja na dola 30,000, bingwa wa michuano hiyo kwa mwaka huu atapata fursa ya kwenda kumenyana na klabu ya Everton nchini England.
    Mwaka jana Gor Mahia ilikuwa bingwa wa kwanza wa michuano hiyo baada ya kuwafunga mahasimu wao, AFC Leopard 2-1 katika fainali kwenye michuano iliyofanyika Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA NA YANGA ZAENDA KUTAFUTANA KENYA KWA MECHI YA NNE YA MSIMU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top