• HABARI MPYA

    Wednesday, May 30, 2018

    SAMATTA AENDA KUFANYA IBADA YA HIJA NDOGO MAKKA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta anayechezea KRG Genk ya Ubelgiji ameenda kufanya ibada ya Hijja ndogo katika miji ya Makka na Madina.
    Samatta ameposti picha akiwa na mchezaji mwenzake wa KRC Genk, beki Mgambia Omar Colley wapo kwenye vazi maalum la ibada hiyo lijulikanalo kama Ihram katika mji wa Makka.
    Wanaonekana wapo ndani ya msikiti wa Haram ambao hawaruhusiwi kuingia watu waovu au wafanya haramu yoyote, wakiwa jirani na Alqaaba, nyumba maalum ya Mwenye Mungu ambayo waendao ibada hiyo huizunguka mara saba na ambako pia (Alqaaba) waislamu wote duniani huelekea wanapofanya ibada zao za sala.
    Mbwana Samatta akiwa na mchezaji mwenzake wa KRC Genk, beki Mgambia Omar Colley (kulia) katika vazi Ihram msikiti wa Haram mjini Makka 

    Mbwana Samatta (kulia) akiwa jirani na Alqaaba (kulia kwake) katika ibada  ya Umra

    Samatta amekwenda kufanya ibada hiyo baada ya kumaliza msimu wa Ligi Kuu ya Ubelgiji akiisaidia KRC Genk kupata tiketi ya kucheza michuano ya Europa League baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Zulte Waregem Uwanja wa Luminus Arena mjini Genk mwishoni Jumapili.
    Nahodha huyo wa Taifa Stars siku hiyo alifunga bao la kwanza dakika ya 18, akimalizia pasi ya mshambuliaji mwenzake, kinda wa umri wa miaka 23, Leandro Trossard, kabla ya beki Mfinland, Jere Uronen kufunga la pili dakika ya 28 akimalizia pasi ya kiungo Mspaniola, Alejandro Pozuelo Melero.
    Samatta, mwenye umri wa miaka 25, Mei 27 mwaka huu alifikisha mabao 26 akicheza mechi yake ya 90 tangu ajiunge na Genk Januari mwaka 2016 akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ambayo nayo ilimtoa Simba SC ya Tanzania mwaka 2011 alikodumu kwa msimu mmoja baada ya kusajiliwa kutoka African Lyon.
    Samatta alianza kuchezea Lyon tangu ikiitwa Mbagala Market katika Ligi Daraja la Kwanza 2008 na akaipandisha hadi Ligi Kuu mwaka 2009. 
    Akiwa Mazembe, pamoja na kushinda mataji manne ya ubingwa wa Ligi Kuu ya Kongo, maarufu kama  Linafoot katika miaka ya 2011, 2012, 2013 na 2014, pia alitwaa Super Cup ya DRC mwaka 2013 na 2014 na taji la Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2015 na kushinda tuzo ya Mwanasoka Bora Anayecheza Afrika mwaka 2015.
    Ikumbukwe Samatta ameandaa mechi maalum ya Hisani baina ya yeye na Marafiki zake, dhidi ya marafiki wa mwanamuziki Ali Kiba itakayofanyika Juni 9, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuchangisha madawati na miundombonu ya shule.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SAMATTA AENDA KUFANYA IBADA YA HIJA NDOGO MAKKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top