• HABARI MPYA

    Friday, January 04, 2013

    SIMBA NA TUSKER NGUVU SAWA KOMBE LA MAPINDUZI

    Kikosi cha Simba kilichotoa sare ya 1-1 na Tusker usiku huu Amaan

    Na Mahmoud Zubeiry, Zanzibar
    SIMBA SC imetoka sare ya kufunga bao 1-1  na Tusker ya Kenya katika mchezo wa Kundi A, Kombe la Mapinduzi usiku huu kwenye Uwanja wa Amaan mjini hapa.
    Kwa matokeo hayo, Tusker inaendelea kuongoza Kundi A, kwa piointi zake tatu sawa na Simba, lakini mabingwa hao wa Kenya wana wastani mzuri zaidi wa mabao.
    Hadi mapumziko timu hizo zilikuwa zimekwishafungana bao 1-1, Simba wakitangulia kupata bao dakika ya 18 mfungaji Haruna Moshi Shaaban, maarufu kama Boban au Balotelli wa Bongo kabla ya Tusker kusawazisha dakika ya 39, mfungaji Khalid Aucho.
    Boban alifunga bao tamu sana kwa ufundi wa hali juu akiwa amedhibitiwa na beki ngongoti wa Tusker, Joseph Shikokoti na kuirukia pasi ya Ramadhan Chombo ‘Redondo’ kuitumbukiza nyavuni.
    Baada ya kufunga bao hilo, Boban aliangukia mkono na kuumia, hivyo hakushangilia bao lake na moja kwa moja alianza kutibiwa na Daktari Cossmas Kapinga wa Simba.
    Baada ya bao hilo, Simba iliongeza mashambulizi langoni mwa Tusker na Boban alikaribia kufunga tena dakika ya 30 kama si shuti lake kutoka nje sentimita chache.
    Aucho alifunga bao lake akiunganisha krosi ya Jeremiah Bright kutoka upande wa kushoto wa Uwanja.
    Baada ya hapo, timu zilianza kushambuliana kwa zamu hadi refa Ramadhani Kibo alipopuliza kipyenga cha kuhitimisha ngwe ya kwanza.
    Kipindi cha pili timu zote zilirudi vizuri na kucheza kwa umakini wa hali ya juu, jambo ambalo lilisababisha dakika 90 zimalizike zikiwa zimefungana 1-1.
    Katika mchezo huo, kikosi cha Simba kilikuwa; William Mweta, Miraj Adam, Paul Ngalema, Shomary Kapombe, Komabil Keita, Jonas Mkude, Haroun Athumani/MKussa Mudde75, Mwinyi Kazimoto, Felix Sunzu, Haruna Moshi na Ramadhan Chombo ‘Redondo’/Edward Christopher dk 52.
    Tusker FC; Samuel Odhiambo, Luke Ochieng, Jeremiah Bright/Humphrey Okoth, Mark Odhiambo, Joseph Shikokoti, Khalid Aucho, Edwin Manono/Benson Amanda, Justin Monda, Ismail Dunga/Michael Olunga, Jesse Were na Robert Omonuk.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: SIMBA NA TUSKER NGUVU SAWA KOMBE LA MAPINDUZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top