• HABARI MPYA

    Friday, January 25, 2013

    SERIKALI KUCHUKUA ASILIMIA 15 TU MECHI ZA TAIFA


    Waziri Makala akizungumza kushoto na kulia ni Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah  
    Na Mahmoud Zubeiry
    SERIKALI imezipa ahueni klabu za Ligi Kuu kwa kupunguza makato yanayotokana na viingilio vya mechi mbalimbali zinazochezwa kwenye Uwanja huo na sasa itakuwa inakata asilimia 15 tu baada ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).
    Akizungumza na Waandishi wa Habari ofisini kwake asubuhi ya leo, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Amos Makala alisema kwamba kuanzia sasa Serikai itakuwa inachukua asilimia 15 ya mapato yote ya mechi zinazochezwa kwenye Uwanja huo na hakutakuwa na makato mengine yoyote.
    Makalla alisema kwamba, awali Serikali ilikuwa inachukua asilimia 10 ya mapato, lakini kulikuwa kuna makato mengine mengi, kama usafi, Wachina na kadhalika, ambayo sasa yanaondolewa kabisa.
    “Kulikuwa kuna malalamiko ya makato ya Uwanja wa Taifa, serikali tumelishughulikia. Tulianza kwa vikao, kati yetu serikali, Katibu TFF, BMT, Wakurugenzi na Kamati ya ligi, ilikuwa ni mijadala mirefu, mwanzoni mambo yalikuwa magumu kidogo, ila baadaye tukafikia mwafaka,”alisema Makala.
    Makala alikumbushia awali Uwanja wa Taifa ulikuwa kwa ajili ya mechi kubwa, lakini baadaye Simba na Yanga zikaomba zikaruhusiwa. “Ikaja kuonekana timu zote zinautaka huo Uwanja ndio tukawaruhusu watumie. Tukawa tunafanya gharama za Uwanja asilimia 20, tunachukua na bado kulikuwa kuna makato mengine mengi, klabu zikalia lia, tukapunguza hadi ikawa asilimia 10,”alikumbushia.
    Makala alisema ili kuondoa dhana ya makato ya kinyonyaji, pande zote zimekubaliana na kutia saini leo mkataba wa makubaliano mapya ya kutumia Uwanja wa Taifa.
    Aidha, Makala alikumbushia umuhimu wa kuutunza huo kwa sababu unasifika mno barani Afrika. “Nilipokuwa Nairobi (Kenya), Wakenya watu wa AFC Leopard walikuwa wanausifia sana Uwanja ule, wanasema ni kati ya viwanja vizuri sana hapa Afrika, kwa hivyo tuna wajibu wa kuutunza,”alisema.
    Alisema mara ujenzi wa Uwanja wa Uhuru utakapokamilika kati ya Aprili na Juni, mwaka huu matumizi ya Uwanja wa Taifa yatarudi kuwa kama mwanzo, kwa ajili ya timu za taifa na mechi za wapinzani wa jadi, Yanga na Simba, wakati mechi nyingine zote zitahamia Uhuru.
    Pamoja na utaratibu huo mpya wa makato, Naibu Waziri huyo alisema kwamba kwa watakaotaka kuukodisha Uwanja kwa shughuli mbalimbali, watalazimikka kulipia Sh Milioni 20.
    Makala pia alisema kwamba serikali imekubali kulipa kodi za mishahara ya makocha wa timu ya taifa, ambazo zilisababisha akaunti ya Ligi Kuu ikazuiwa kutokana na ukubwa wa deni hilo la TFF.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: SERIKALI KUCHUKUA ASILIMIA 15 TU MECHI ZA TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top