• HABARI MPYA

  Jumapili, Januari 27, 2013

  YANGA YAWAADHIBU MAAFANDE WA MAGEREZA, TEGETE WA UTURUKI KWELI BALAA

  Jerry Tegete akichomoka kushangilia baada ya kuifungia Yanga bao la kwanza katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya TZ Prisons Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jioni hii. Yanga ilishinda 3-1.

  Na Mahmoud Zubeiry
  YANGA SC imezidi kupaa kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baada ya jioni hii kuitandika Prisons ya Mbeya mabao 3-1 katika mchezo wa ligi hiyo uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Kwa ushindi huo, Yanga imetimzia pointi 32 baada ya kucheza mechi 14, hivyo kuendelea kuongoza Ligi Kuu kwa wastani wa pointi tano, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 27 na Simba 26.
  Hadi mapumziko, timu hizo zilikuwa tayari zimefungana bao 1-1, Yanga wakitangulia kupata bao lao dakika ya 10 kabla ya Prisons kusawazisha dakika ya 17.
  Bao la Yanga lilifungwa na Jerry Tegete aliyeunganisha krosi nzuri ya Simon Msuva kutoka wingi ya kulia, wakati la Prisons lilifungwa na Elias Maguri, aliyeunganisha krosi nzuri ya Misango Magai kutoka wingi ya kushoto.
  Tegete akiigusa nembo ya Yanga baada ya kufunga la tatu. PICHA ZAIDI BAADAYE.
  Yanga walicheza vizuri dakika 15 za mwanzo na baada ya hapo, timu hizo zilianza kushambuliana kwa zamu, ingawa Watoto wa Jangwani ndio waliopoteza nafasi nzuri zaidi za kufunga.
  Kipindi cha pili, Yanga walirudi na kasi nzuri kusaka ushindi na iliwachukua dakika 11 tu kupata bao la pili, lililofungwa na Mbutu Twite baada ya kutokea piga nikupige langoni mwa Prisons.
  Wakati Prisons wakiwa kwenye jithada za kusaka bao la kusawazisha, walijikuta wakitandikwa bao la tatu, Tegete tena akiwainua vitini mashabiki wa Yanga, baada ya kupokea pasi nzuri ya Nurdin Bakari dakika ya 65.
  Baada ya bao hilo, Yanga walianza kuonyesha vitu vya Uturuki walipoweka kambi ya wiki mbili kabla ya kuanza kwa mzunguko huu wa pili wa Ligi Kuu, wakicheza soka ya madoido pasi nyingi, uzungu na kila aina ya mbwembwe, ili mradi tu kuwaburudisha mashabiki wake.
  Mapema kabla ya mchezo huo, kiungo wa Yanga, Frank Domayo alipatwa na Malaria ya ghafla na kuenguliwa kwenye kikosi cha kwanza na nafasi yake akaanza Nurdin Bakari, wakati mshambuliaji mpya wa Prisons, Emmanuel Gabriel alienguliwa kwenye kikosi cha kwanza na nafasi yake akachukua Elias Maguri, kwa sababu ya kutokuwa na leseni ya TFF ya kumruhusu kucheza Ligi Kuu. Suala la leseni ya Gabriel, dhahiri ni uzembe wa viongozi wa Prisons.
  Katika mchezo wa leo, kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Mbuyu Twite/Juma Abdul dk 82, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Athumani Iddi ‘Chuji’, Simon Msuva, Nurdin Bakari/David Luhende dk 66, Didier Kavumbangu/Hamisi Kiiza dk 64, Jerry Tegete na Haruna Niyonzima.
  TZ Prisons; David Abdallah, Aziz Sibo, Henry Mwalugala, Lugano Mwangama, Jumanne Elfadhil, Nurdin Issa, Sino Augustino, Freddy Chudu, Elias Maguri, Misango Magai/John Matei dk58 na Jeremiah Juma. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: YANGA YAWAADHIBU MAAFANDE WA MAGEREZA, TEGETE WA UTURUKI KWELI BALAA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top