• HABARI MPYA

  Jumatano, Januari 30, 2013

  SIMBA WAWE NA SUBIRA, VINGINEVYO WATAHARIBU KABISAAAA

  Na Bin Zubeiry

  MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Simba SC waliuanza vyema mzunguko wa pili wa ligi hiyo, baada ya kuifunga African Lyon mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Jumamosi.
  Huo ulikuwa mwanzo mzuri, ingawa matokeo ya mechi nyingine za Ligi hiyo, ikiwemo Yanga na Azam kushinda kwa idadi sawa na hiyo ya mabao, yanafanya msimamo wa Ligi Kuu kwa timu tatu za juu ubaki kama ulivyokuwa.
  Yanga wenye pointi 32 wanaongoza, wakifuatiwa na Azam wenye pointi 27, wakati Simba ni ya tatu ikiwa na pointi 25.
  Pamoja na ushindi huo, mashabiki wa Simba walitoka uwanjani na nongwa ya kutofurahishwa na kiwango cha timu, huku vyombo vya habari vikiponda timu hiyo ilivyocheza kipindi cha pili.
  Katika utetezi, Kocha Msaidizi wa Simba, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ alidai wachezaji waliathiriwa na hali ya hewa ya Dar es Salaam, kwa sababu ya kukaa kambini Oman kwa wiki mbili kujiandaa na mzunguko wa pili wa ligi hiyo.
  Haya ya Julio ni blah blah ambazo tumezizoea kuzisikia kutoka kinywa chake- lakini haizuii ukweli yeye ni kocha na mtaalamu.
  Ukweli ambao wana Simba wanapaswa kuuelewa kwa sasa ni mabadiliko makubwa ndani ya kikosi chao kutoka kile cha msimu uliopita, hasa katika safu ya ulinzi na hilo limekuwa likiitesa timu hiyo tangu kwenye Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame Julai mwaka jana.
  Simba wanakabiliwa na changamoto ya kuunda ukuta mpya, baada ya ule uliowafanya watambe msimu ulipita kutawanyika.
  Ukitazama uchezaji wa Simba, kuanzia kwenye safu ya kiungo kwenda mbele huwezi kuona tatizo na timu inashambulia sana, wanacheza kwa kuonana na wana wachezaji wenye kasi nzuri tu pale mbele, ukiondoa Mrisho Ngassa wapo chipukizi kama Ramadhani Chanongo anayeinukia vizuri.
  Lakini pia kuna kitu nilikiona ndani ya kikosi cha Simba ikimenyana na Lyon, ni kama wamebadilisha aina ya uchezaji wao wa taratibu wakigonga pasi nyingi na sasa wanashambulia kwa kasi kupitia pembeni.
  Kwa sababu hiyo, sikustaajabu hata siku hiyo wachezaji wasio na kasi kama Haruna Moshi ‘Boban’ wakianzia benchi. Aina ya mchezo wanaohamia Simba SC kwa sasa unahitaji wachezaji kuwa fiti sana ili kuumudu kwa muda wote.
  Ndiyo maana nikasema, aliyosema Julio ni blah blah ambazo tumezizoea, ila ukienda kwenye suala la msingi la kiufundi kwa sasa Simba inakabiliwa na changamoto ya kutengeneza timu mpya na kuumudu pia mfumo wa uchezaji wa kasi, ambao inaonekana ndiyo anaoupenda kocha wao mpya, Mfaransa Patrick Liewig.
  Na ndiyo maana utaona aina ya wachezaji waliopangwa kwenye mechi hiyo wengi ni wenye kasi na hata wale ambao tumezoea kuwaona wakicheza taratibu, siku hiyo walibadilika kidogo kama Ramadhan Chombo ‘Redondo’.
  Kocha ndiye anayeiongoza timu na ndiye anayeamua timu icheze kwa aina ipi- na kwa aina anayotaka lazima apange aina ya wachezaji ambao watamudu kuicheza. Amekaa na wachezaji mazoezini kwa wiki takriban tatu kuanzia Zanzibar na baadaye Oman, amewafundisha na amejua ni akina nani watamfaa katika kampeni zake.
  Hili ni la msingi sana ambalo mashabiki wa Simba kwanza wanatakiwa walipokee na kulikubali, ikiwa kweli wanataka mabadiliko ndani ya timu yao. Kwa sasa, naona dalili kama Liewig ataendelea na mfumo huo, timu itafanya vizuri zaidi kipindi cha kwanza, lakini baadaye wachezaji wakichoka hali itabadlika.
  Hata hivyo, baada ya muda, tena si mrefu iwapo Simba watavumilia na kocha atapewa sapoti ya kukamilisha mipango yake, timu itakaa sawa na itakuwa tishio mno kwa mfumo wake.
  Tunajua, wapo wachezaji magwiji wa mizengwe, ambao anapotokea kocha mwenye mazoezi magumu, humfanyia mizengwe ili aondolewe na hili tayari linamkabili Liewig pale Simba SC na wanaoweza kumuepusha nalo ni viongozi kwa kuhakikisha wanampa nguvu ya kutekeleza programu yake na kuhakikisha wachezaji wote wote wanatii.
  Kwa lugha nyepesi naweza kusema Simba hivi sasa wanatengeneza timu, wakiwa tayari wana wachezaji wazuri na hiki ni kipindi ambacho wapenzi wa timu hiyo wanapaswa kuwa wavumilivu na kuiunga mkono timu yao.
  Ingekuwa kazi rahisi kwa Liewig kuisuka upya Simba, kama angekuta timu ile ile ya msimu uliopita iliyozoeana baada ya kucheza pamoja kwa muda mrefu, lakini ukitazama kikosi cha kwanza cha Wekundu hao wa Msimbazi kwa sasa na ukirejea kile kilichotwaa ubingwa msimu uliopita.    
  Juma Kaseja, Nassor Masoud ‘Chollo’, Amir Maftah, Shomary Kapombe, Kelvin Yondan, Patrick Mafisango, Uhuru Suleiman, Mwinyi Kazimoto, Felix Sunzu, Haruna Moshi ‘Boban’ na Emmanuel Okwi- hiki ni kikosi kilichoichapa Yanga 5-0, leo wangapi wamebaki hapo? 
  Maftah ameasi kwa sababu anadai haki zake, Yondan amehamia Yanga, Mafisango amefariki dunia, Uhuru amehamia Azam na Okwi amehamia Etoile du Sahel ya Tunisia.
  Bado hata baadhi ya wachezaji ambao walikuwa wa akiba kama Ally Mustafa ‘Barthez’, Obadia Mungusa na Juma Nyosso hawapo kwa sasa. Kama kukosekana kwa mchezaji mmoja tu kwenye timu kunaweza kuiathiri timu kwa kiasi kikubwa, amini hata Simba kwa sasa wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kuunda timu mpya.
  Tazama kwenye beki pale, hadi sasa bado hawajampata mbadala wa Yondan, licha ya kujaribu kusajili wachezaji kadhaa, Lino Masombo na Paschal Ochieng lakini wote wameona hawatafaa.
  Wameamua kubaki na Komabil Keita, lakini naye hakubaliki ndiyo maana kiungo Mussa Mudde amerudishwa kwenye safu ya ulinzi anacheza na Shomary Kapombe. Hizi ni changamoto ambazo zinaikabili timu hiyo kwa sasa na mashabiki wanapaswa kuwa waelewa na kuunga mkono jitihada za ujenzi wa Simba mpya.
  Wakishapatikana 11 wa kwanza wa uhakika, watakaocheza kwa uelewano, mambo mengine yatakuwa madogo tu kama suala la mfumo na kadhalika kwa sababu timu haiwezi kucheza mfumo ule ule katika kila mechi.
  Simba ina wachezaji wazuri sana hadi wale vijana wadogo waliopandishwa kutoka timu B na wengine wapya ambao bado hawajazoea na ni wajibu wa mashabiki wa Simba kuwapa sapoti wachezaji wao na si kuanza kuwakatisha tamaa mapema.
  Umefika wakati, mashabiki wa soka nchini waanze kubadilika taratibu na kuwa waelewa. Kwa sasa jambo la msingi kwa Simba SC ni pointi tatu ili kujiweka sawa kwenye mbio za ubingwa na bila shaka hilo ndilo lengo la benchi la ufundi kwa sasa pamoja na changamoto zinazowakabili.  Ipo haja ya Simba kuwa wavumilifu kwa sasa, timu yao ikisukwa upya. Alamsiki.

  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: SIMBA WAWE NA SUBIRA, VINGINEVYO WATAHARIBU KABISAAAA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top