• HABARI MPYA

  Jumamosi, Januari 26, 2013

  MORO MARATHON KUFANYIKA FEBRUARI 23


  Na Daudi Julian, Morogoro
  MASHINDANO ya Riadha ya Nusu Marathon (Morogoro Half Marathon) yanatarajia kufanyika Februari 23, mwaka huu, mjini hapa.
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY, Msemaji wa mashindano hayo, Christopher Ngao alisema lengo la mashindano hayo ni kutangaza utalii wa ndani ikiwemo vivutio vya utalii vilivyopo mkoani Morogoro.
  Ngao alisema maandalizi kwa ajili ya mashindano hayo yanakwenda vizuri na kwamba wanariadha kutoka mkoani hapa na nje ya mkoa huu watashiriki.
  Msemaji huyo alisema katika mashindano hayo kutakuwa na zawadi mbalimbali kwa washindi, wanaume na wanawake, ikiwemo fedha taslimu pamoja na kutolewa vyeti vya ushiriki kwa washiriki wa mashindano.
  Alisema mshindi wa kwanza atazawadiwa Sh.50,000, wa pili atapata Sh.30,000 na wa tatu atapata Sh.20,000.
  Hata hivyo, Ngao alisema zawadi hizo huenda zikaongezeka iwapo wafadhili zaidi watajitokeza na kudhamini mashindano hayo.
  “Kimsingi, maandalizi yanakwenda vizuri na Jumatatu tunatarajia kuanza kutoa fomu kwa washiriki”, alisema.
  Msemaji huyo amewataka wanariadha wanaotarajia kushiriki mashindano hayo kuanza mazoezi ili kuhakikisha wanafanya  vizuri katika mashindano hayo.
  Aidha, ametoa wito kwa wadau wa michezo mkoani Morogoro na nje ya mkoa kujitokeza kwa wingi na kudhamini mashindano hayo ya aina yake kufanyika mkoani hapa.

  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: MORO MARATHON KUFANYIKA FEBRUARI 23 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top