• HABARI MPYA

  Saturday, January 26, 2013

  KIPYENGA CHALIA LEO LALA SALAMA LIGI KUU BARA, NANI ANA NINI?

  Simba na Yanga katika mechi ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu iliyoisha kwa sare ya 1-1

  Na Mahmoud Zubeiry
  MZUNGUKO wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, unatarajiwa kuanza leo, nyasi za viwanja sita tofauti nchini zikiwaka moto katika mechi za ufunguzi za mzunguko huo wa lala salama.
  Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam,Watoto wa Zamunda, African Lyon watamenyana na mabingwa watetezi, Simba SC wakati Manungu, Turiani mkoani Morogoro, Mtibwa Sugar watakuwa wenyeji wa Polisi ya Morogoro mjini.
  Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, Coastal Union watakuwa wenyeji wa Mgambo JKT wakati Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani, Ruvu Shooting watawakaribisha ndugu zao, JKT Ruvu, huku Azam FC wakiwa wenyeji wa Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam na Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha, JKT Oljoro wataikaribisha Toto Africans ya Mwanza.
  Vinara wa Ligi hiyo, Yanga SC wao wataanza mbio za kurejesha taji Jangwani keshokutwa, watakapomenyana na Maafande wa jeshi la Magereza, Prisons kutoka Mbeya.
  Je, timu zinaingia kwenye mzunguko wa pili zikiwa katika nafasi gani na zimejiandaaje kuelekea hatua hiyo ya lala salama? Endelea.
  Yanga SC

  YANGA SC:
  Walimaliza mzunguko wa kwanza wakiwa kileleni mwa Ligi Kuu, wakiwa na pionti zao 26, baada ya kucheza mechi 13, kufungwa mbili dhidi ya Mtibwa Sugar 3-0 na Kagera Sugar 1-0, zote ugenini, kutoa sare mbili 1-1 dhidi ya Simba SC na 0-0 dhidi ya Prisons.
  Yanga ambayo msimu uliopita ilishika nafasi ya tatu Ligi Kuu, ilipanda kileleni Novemba 4, baada ya kuifunga Azam FC mabao 2-0 na kuwashusha mabingwa watetezi, walioongoza ligi hiyo tangu mwanzoni.
  Katika ya mzunguko wa kwanza, Yanga ilifikia kuzidiwa pointi saba na Simba lakini Oktoba 31, ikafanikiwa kuwafikia Wekundu hao wa Msimbazi, siku hiyo wao wakiifunga Mgambo JKT 3-0 Dar es Salaam na wapinzani wao0 wakilazimishwa sare ya bila kufungana na Polisi Morogoro.
  Baada ya mapumziko mafupi, Yanga walianza kujifua Dar es Salaam, kabla ya kwenda kwenye ziara ya mafunzi Uturuki kwa wiki mbili ambako pamoja na mazoezi walipata mechi tatu za kujipima nguvu na waliporudi, pia wamecheza mechi mbili za kujipima nguvu dhidi ya Black Leopard ya Afrika Kusini, ambazo wameshinda zote. Katika dirisha dogo, Yanga imeongeza mchezaji mmoja tu, Kabange Twite kutoka APR ya Rwanda. 
                                     P    W  D   L    GF GA GD Pts
  1    Yanga                   13 9    2    2    25 10 15 29
  KOCHA; Ernie Brandts (Uholanzi)

  Azam FC
  AZAM FC:
  Ilimaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ikiwa katika nafasi ya pili, kwa pointi zake 24, ikiwazidi pointi moja tu mabingwa watetezi, Simba SC. Azam walikuwa na mwelekeo wa kumaliza katika nafasi nzuri zaidi kama si kufungwa mechi mbili mfululizo za mzunguko wa kwanza, dhidi ya Yanga 2-0 na Mgambo JKT 2-1.
  Azam ilianza vema tu ligi hiyo, ikiwa nyuma ya Simba tangu mwanzo hadi Oktoba 31, ilipoenguliwa na Yanga katika nafasi ya pili. Ikielekea kwenye mechi yake ya mwisho dhidi ya Mgambo, Azam ilifukuza wachezaji wake wanne, Deo Munishi ‘Dida’, Erasto Nyoni, Said Mourad na Aggrey Morris kwa madai walipokea hongo waifungishe timu hiyo dhidi ya Simba na wanadai wana ushahidi hadi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU). Dhahiri kuondolewa kwa wachezaji hao tegemeo kikosini kulichangia matokeo ya kufungwa na Mgambo katika mechi ya mwisho.
  Baada ya mapumziko mafupi, Azam ilianza kujifua tena na ikaenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kucheza Kombe la Hisani, walilofanikiwa kutwaa. Waliporudi wakaenda kwenye Kombe la Mapinduzi, ambako pia walitwaa taji hilo. Baada ya hapo, wakafanya ziara ya wiki moja Kenya, ambako walicheza mechi tatu za kujipima nguvu, wakishinda mbili na kufungwa moja.
  Katika dirisha dogo, Azam imesajili wachezaji saba, ambao ni Humphrey Mieno kutoka Kenya, Brian Umony (Uganda), Jockins Atudo (Kenya), David Mwantika (Prisons), Abdallah Seif (Ruvu Shooting), Malika Ndeule (Mtibwa Sugar) na Uhuru Selemani kwa mkopo kutoka Simba SC.
                                    P    W  D   L    GF GA GD Pts
  2    Azam                    13 7    3    3    17 11 6    24
  KOCHA: Stewart Hall (Uingereza)
  Simba SC

  SIMBA SC:
  Mabingwa hao watetezi, waliianza Ligi Kuu vema wakionyesha dalili zote za kutetea ubingwa wao kwa kufanikiwa kuwa kileleni hadi mwishoni mwa mzunguko huo, kabla ya mambo kugeuka ghafla.
  Zilianza sare kwanza, 1-1 na Yanga, 0-0 na Coastal Union, 2-2 na Kagera Sugar na baadaye 0-0 na Mgambo, 0-0 na Polisi Morogoro kabla ya kufungwa mechi ya kwanza msimu huu, mbele ya Mtibwa Sugar na kumaliza mzunguko wa kwanza kwa kipigo cha 1-0 kutoka kwa Toto Africans.
  Matokeo haya kwa kiasi kikubwa yameivuruga Simba SC na inasemekana Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ anafikiria kujiuzulu na baada ya kufungwa na Mtibwa Sugar, hakujihusisha na chochote juu ya maandalizi ya mchezo dhidi ya Toto, wakati huo Mwenyekiti wake, Alhaj Ismail Aden Rage yuko bize na shughuli za kisiasa Dodoma.
  Baada ya mapumziko mafupi, Simba walirudi mazoezini na Desemba wakaenda Zanzibar kushiriki Kombe la Mapinduzi, ambako walitolewa Nusu Fainali na baada ya hapo, wakaenda Oman, kwenye kambi ya wiki mbili ya mafunzo. Waliporejea, juzi walicheza mchezo wa kujipima nguvu na Black Leopard ya Afrika Kusini.
  Habari mbaya, au njema kwa wapenzi wa Simba ni kumpoteza mshambuliaji wake hatari, Emmanuel Okwi aliyeuzwa dola za Kimarekani 300,000 katika klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia. Simba imeingiza fedha nyingi, ambazo ni rekodi katika historia yao ya kuuza wachezaji, ila wamepoteza kifaa cha maana sana.
  Katika dirisha dogo, Simba imesajili wachezaji wawili tu kutoka Uganda, kipa Abbel Dhaira na kiungo anayeweza kucheza kama beki pia, Mussa Mudde. Aidha, Simba SC imebadilisha benchi lake Ufundi, imemuondoa Mserbia, Milovan Cirkovick na kuleta Mfaransa, Patrick Liewig ambaye atakuwa anasaidiwa na Mganda, Moses Basena na Mzalendo Jamhiri Kihwelo ‘Julio’.
                                     P    W  D   L    GF GA GD Pts
  3    Simba SC             13 6    5    2    20 11 9    23
  KOCHA: Patrick Liewig (Ufaransa)
  Mtibwa Sugar

  MTIBWA SUGAR:
  Ilianza vizuri, katikati ikavurunda na mwishoni mwa mzunguko wa kwanza ikazinduka tena hatimaye imemaliza katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu.
  Inaonekana Mtibwa Sugar inaanza kurejesha makali yake iliyoingia nayo katika soka ya Tanzania miaka ya 1990 hadi wakafanikiwa kutwaa ubingwa wa ligi hiyo mara mbili mfululizo 1999 na 2000, wakiweka rekodi ya kuwa timu pekee nje ya Simba na Yanga kutetea taji hilo.
  Hiyo si kwa sababu tu ipo nyuma ya Yanga, Azam na Simba, bali katika mzunguko wa kwanza msimu huu imefanikiwa kuvifunga vigogo vyote vya soka nchini, Simba na Yanga.  Baada ya mapumziko mafupi, Mtibwa walianza mazoezi Desemba na mapema mwezi huu walikwenda kucheza Kombe la Mapinduzi, ambako hata hivyo hawakufanya vizuri. Waliporejea Morogoro, waliendelea na mazoezi na kupata mechi kadhaa za kujipima nguvu. Katika dirisha dogo, Mtibwa Sugar imesajili wachezaji wane tu, wote huru Rajab Mohamed, Zakayo Joseph, Baraka Anthony na Mussa Chambo.
                                 P    W  D   L    GF GA GD Pts
  4    Mtibwa Sugar    13 6    4    3    18 12 6    22
  KOCHA: Mecky Mexime (Mzalendo)
  Coastal Union

  COASTAL UNION:
  Wana Mangushi wamerudi tena kwenye makali yao yaliyowafanya wakawa mabingwa wa ligi hiyo mwaka 1988, kwani hadi sasa wameonyesha upinzani wa kutosha kwenye Ligi Kuu. Wagosi hao wa Kaya wamemaliza katika nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu kwa pointi zao 22 sawa na Mtibwa walio nafasi ya nne, lakini wanazidiwa wastani tu wa mabao ya kufunga na kufungwa.
  Hata hivyo, Coastal walianza Ligi Kuu kwa kusuasua kiasi cha kufikia kuwafukuza makocha wake wa awali waliosajili na kuandaa timu kwa ajili ya ligi hiyo, Juma Mgunda na Habib Kondo ambao nafasi zao zilichukuliwa na Hemed Morcco na Alloy Kiddy.
  Baada ya mapumziko mafupi, Coastal walianza kujifua Desemba na mapema mwezi huu walikwenda Zanzibar kucheza Kombe la Mapinduzi, ambako hata hivyo hawakufanhya vizuri. Waliporejea waliweka kambi Tanga wakiendelea kujifua na kucheza mechi kadhaa za majaribio.
  Katika dirisha dogo, Coastal wamewasajili Shabani Kado kutoka Yanga, aliyekuwa anacheza kwa mkopo Mtibwa Sugar, Rashid Simba, Zuberi Hamisi, Shaongwe Ramadhan, Castory Mumbara na Tinashe Machemedze, wote huru.
                                  P    W  D   L    GF GA GD Pts
  5    Coastal Union    13 6    4    3    16 14 2    22
  KOCHA: Hemed Morocco (Zanzibar)
  Kagera Sugar

  KAGERA SUGAR:
  Kagera Sugar wamemaliza katika nafasi ya sita wakiwa na pointi 21 na wangeweza kumaliza juu ya hapo, kama wangeutumia vizuri mchezo wao wa mwisho kwenye Uwanja wa nyumbani dhidi ya vibonde Polisi Morogoro.
  Wakipewa nafasi kubwa ya kushinda, katika mastaajabu ya wengi, Kagera wakalazimishwa sare ya bila kufungana na Maafande hao wa Morogoro kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, hivyo kuwapa nafasi Coastal na Mtibwa kuendelea kuwa juu yao.
  Kagera inajivunia kutofungwa na vigogo wa soka nchini, kwani waliifunga Yanga 1-0 na wakatoa sare ya 2-2 na Simba na Dar es Salaam.   Baada ya mapumziko mafupi, Kagera walianza kujifua Desemba na kupata mechi kadhaa za kujipima nguvu.
  Katika dirisha dogo, Kagera Sugar wamesajili wachezaji wawili tu na wote huru; Edmund Kashamila na Julius Mrope.
                                    P    W  D   L    GF GA GD Pts
  6    Kagera Sugar      13 5    6    2    15 10 5    21
  KOCHA: Abdallah Athumani Seif ‘Kibadeni’ (Mzalendo)
  Ruvu Shooting

  RUVU SHOOTING:
  Katika timu zote za majeshi kwenye ligi hiyo, Ruvu Shooting ndio inaonekana kuwa imara zaidi na ndiyo maana ilimaliza katika nafasi nzuri zaidi, ya saba. Ruvu ipo katikati ya msimamo wa ligi, nafasi ya saba kwa pointi zake 20.
  Timu hii inayotumia Uwanja wa Mabatini, Mlandizi, Pwani ni moja kati ya timu zilizoonyesha kandanda safi ya kuvutia, tena ikiundwa na wachezaji wengi chipukizi, kama Seif Abdallah anayegombea kiatu cha dhahabu.  
  Baada ya mapumziko mafupi, Ruvu Shooting walianza kujifua na kupata mechi kadhaa za kujipima nguvu na katika dirisha dogo, Ruvu Shooting wamesajili wachezaji watatu tu na wote huru; Juma Mdindi, Njaidi Mohamed na Mahmoud Mbulu. Habari mbaya kwa wapenzi wa timu hiyo, ni kumpoteza kinara wake wa mabao katika mzunguko wa kwanza, Seif Abdallah aliyesajiliwa Azam FC.
                                  P    W  D   L    GF GA GD Pts
  7    Ruvu Shooting   13 6    2    5    19 17 2    20
  KOCHA: Charles Boniface Mkwasa (Mzalendo)
  Mgambo JKT

  MGAMBO JKT:
  Ligi Kuu ya Bara imepokea timu mpya tushio ambayo imeongeza ladha katika ligi hiyo. Hiyo si nyingine zaidi ya JKT Mgambo ua Handeni, Tanga inayotumia Uwanja wa Mkwakwani, Tanga pamoja na Coastal Union. Mgambo ilimaliza katika nafasi ya nane, kwa pointi zake 17. Mgambo walianza kwa kusuasua na watu wakaitabiria itashuka daraja, ila ilipokuja kuzinduka mwishoni mwa msimu, watu wamebadilisha kauli zao. 
  Baada ya mapumziko mafupi, Mgambo JKT walianza kujifua na kupata mechi kadhaa za kujipima nguvu, wakati katika dirisha dogo Mgambo JKT wamesajili wachezaji watatu, ambao ni Moaka Shabani, Ismail Mkaima na Damas Milanzi.
                                  P    W  D   L    GF GA GD Pts
  8    Mgambo JKT      13 5    2    6    10 13 -3  17
  KOCHA: Mohamed Kampira (Mzalendo)
  JKT Ruvu

  JKT RUVU:
  Imeshuhudiwa katika msimu mwingine, timu hii inazidi kupoteza makali yake, baada ya kumaliza katika nafasi ya tisa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu.
  Siyo JKT ile ambayo ilikuwa tishio kwa vigogo, Simba na Yanga bali hii ya sasa ni ‘urojo’ na hali hii inatokea huku ikiwa inaundwa karibu na asilimia kubwa ya wachezaji wake wale wale, walioifanya iwe tishio misimu michache iliyopita, tena wakiwa chini ya kocha yule yule, kiungo wa zamani wa Yanga, Charles Killinda.
  Baada ya mapumziko mafupi, Ruvu JKT walirudi mazoezini na kupata mechi kadhaa za kujipima nguvu na katika dirisha dogo, JKT Ruvu imesajili wachezaji wanne, Zahoro Pazi kwa mkopo kutoka Azam, ambaye hata hivyo amekwenda kufanya majaribio ya kucheza soka ya kulipwa Afrika Kusini, Emmanuel Linjechele, Kisimba Luambano na Nashon Naftali.
                                     P    W  D   L    GF GA GD Pts
  9    JKT Ruvu              13 4    3    6    13 20 -7  15
  KOCHA: Charles Kilinda (Mzalendo)
  JKT Oljoro

  JKT OLJORO:
  Haina makali yake iliyoingia nayo kwenye Ligi Kuu msimu uliopita yaliyowafanya wamalize mzunguko wa kwanza wakiwa kileleni. Msimu huu JKT Oljoro imemaliza katika nafasi ya 10 kwa pointi zake 14 na huwezi kusita kusema ipo kwenye hatari ya kushuka daraja hadi sasa.
  Ina pointi 14, sawa na Toto Africans iliyo nafasi ya 11 na inabebwa juu kwa wastani wa bao moja tu katika mabao ya kufunga na kufungwa, huku ikiwa inaizidi kwa pointi mbili tu Africans Lyon iliyo nafasi ya 12- JKT Oljoro hakika imemaliza mzunguko wa kwanza katika eneo baya.  Baada ya mapumziko mafupi, Oljoro ilianza kujifua Desemba mwaka jana na katika kujisuka upya, ilimfukuza kocha wake Mbwana Makatta, na hadi sasa haijamtaja kocha wake mpya.
  Katika dirisha dogo, Oljoro imesajili wachezaji wapya wanane, ambao ni Nurdin Selemani, Shaibu Nayopa, Hamidu Hassan, Paul Malipesa, Josephat Moses, Muharami Mnyangamala, Majaliwa Mbaga na Alphonce Peter.
                                   P    W  D   L    GF GA GD Pts
  10 JKT Oljoro           13 3    5    5    13 16 -3  14
  KOCHA: Hajatajwa baada ya Makatta kufukuzwa
  TZ Prisons

  TZ PRISONS:
  Imerejea Ligi Kuu msimu huu na hadi sasa unaweza kusema inapambana kuhakikisha inabaki kwenye ligi hiyo msimu ujao. Prisons ilimaliza katika nafasi ya 11 ikiwa na pointi 14.
  Ipo katika hali mbaya na inakabiliwa na vita ngumu ya kupigana kuhakikisha inabaki Ligi Kuu. Mbaya zaidi katika dirisha dogo, limpoteza beki wake kisiki, David Mwantika aliyesajiliwa Azam FC.
  Hata hivyo, nayo imejiimarisha katika usajili wa dirisha dogo, baada ya kusajili wapya wawili, akiwemo mshambuliaji wa zamani wa Simba SC, Emmanuel Gabriel na Mohamed Kayi, ambao wote ni huru.
  Prisons ilianza kujifua kwa ajili ya mzunguko wa pili tangu Desemba mwaka jana na imepata mechi kadhaa za kujipima nguvu, hadi za ugenini ikiwemo ya wiki hii dhidi ya Mtibwa Sugar huko Morogoro, ambako walifungwa 1-0 Manungu.
                                   P    W  D   L    GF GA GD Pts
  11 TZ Prisons           13 3    5    5    8    12 -4  14
  KOCHA: Jumanne Charles (Mzalendo)
  Toto Africans

  TOTO AFRICANS:
  Wana Kishamapanda bado wapo katika wakati mgumu, kwani walimaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu wakiwa katika nafasi ya 12, ambayo ni ndani ya nafasi tatu za kushuka Daraja.
  Washukuru sana ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Simba SC kwenye mchezo wao wa mwisho wa mzunguko wa kwanza, kwani umewainua kidogo, vinginevyo wangemaliza ligi hiyo vibaya zaidi.
  Lakini hii ni timu ambayo inacheza kwa ushindani zaidi inapokutana na timu tishio, ila kwa timu ambao zinaonekana si tishio, Toto hufanya vibaya. Bila shaka kuna kudharau mechi, ambako ndiko kunawaponza na kama watabadilika mzunguko wa pili, wanaweza kufanya vizuri na kubaki Ligi Kuu.  Baada ya mapumziko mafupi, Toto walianza kujifua na kupata mechi kadhaa za kujipima nguvu na katika dirisha dogo, waliimarisha kikosi chao kwa kusajili wachezaji wapya wanne, ambao ni Donald Obimma, Exavery Muhollery, Mohamed Hussein na Ulugbe Odia.
                                 P    W  D   L    GF GA GD Pts
  12 Toto African       13 2    6    5    10 15 -5  12
  KOCHA: John Tegete (Mzalendo)
  African Lyon

  AFRICAN LYON:
  African Lyon, ilimaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ikiwa katika nafasi ya 13 kwa pointi zalke tisa. Licha ya kunolewa na kocha Muargentina, Pablo Ignacio Velez, lakini Lyon walikuwa vibonde tu mzunguko wa kwanza.
  Mmiliki wa timu hiyo, Rahim Kangezi ‘Zamunda’ amejitahidi kuboresha kikosi kwa kusajili wachezaji wapya wa kuongeza nguvu, ingawa si wale alioahidi Emmanuel Okwi na Mrisho Ngassa wa Simba na Mbuyu Twite wa Yanga.
  Katika dirisha dogo, Zamunda amemudu kuwasajili Obadi Mungusa, Juma Seif, Yusuf Mgwao wote huru, Ibrahim Job na Shamte Ally wote kwa mkopo kutoka Yanga SC, Buya Jamwaka, Takang Valentine, Nurdin Mussa, Salvatory Jackson, Mohamed Athuman, Athuman Kajembe na Jarufu Kizombi huru pia.
  Aidha, Mmarekani huyo mwenye asili ya Tanzania, pia amemtupia virago kocha kocha Pablo Ignacio Velez na kwa sasa timu itakuwa chini ya Mkurugenzi wa Ufundi, Mkenya Charles Otieno. Lyon imekuwa ikijifua kwenye Uwanja wa TCC, Chang’ombe tangu Desemba mwaka jana, baada ya mapumziko mafupi.
                                 P    W  D   L    GF GA GD Pts
  13 African Lyon       13 2    3    8    9    20 -11 9
  KOCHA: Pablo Ignacio Velez (Argentina)
  Polisi Morogoro

  POLISI MOROGORO:
  Imerejea Ligi Kuu msimu huu, lakini haitakuwa ajabu mwishoni mwa msimu ikarudi tena kucheza Ligi Daraja la kwanza. Timu ya Morogoro, ilimaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, ikiwa inashika mkia. Polisi haijashinda mechi hata moja zaidi ya kutoa sare nne na kufungwa mechi nyingine tisa.
  Sijui maajabu gani yatokee, msimu ujao tuendelee kuwa na timu ya Morogoro, kwani kulingana na ushindani wa Ligi Kuu msimu huu, hakuna dalili za Polisi kupona. Lakini hakuna linaloshindikana, timu hiyo inaonekana kufanyia kazi suala hilo na imeboresha kikosi kwa kusajili wachezaji kadhaa wenye uzoefu wa Ligi Kuu wainusuru timu, ingawa bahati mbaya kwao, wamepoteza kocha wao John Simkoko.
  Katika dirisha dogo, Polisi Moro imewasajili Shukuru Kassim, Chacha Marwa, Salum Machaku, Mzamiru Said, Victor Bundala, Delta Thomas, Edward Mzeru na Tizzo Chomba.
                                 P    W  D   L    GF GA GD Pts
  14 Polisi Moro         13 0    4    9    4    16 -12 4
  KOCHA: adolph rishard  (Mzalendo)
  Brian Omony aliyetua Azam kutoka Uganda 

  WALIOINGIA DIRISHA DOGO LIGI KUU BARA:
  Yanga SC; Kabange Twite (APR, Rwanda/FC Lupopo DRC)
  Coastal FC; Shabani Kado (Kutoka Mtibwa Sugar/Yanga SC) Rashid Simba, Zuberi Hamisi, Shaongwe Ramadhan, Castory Mumbara, Tinashe Machemedze (Huru).
  Azam FC; Humphrey Mieno (Kenya), Brian Umony (Uganda), Jockins Atudo(Kenya), David Mwantika(Prisons), Abdallah Seif (Ruvu Shooting), Malika Ndeule (Mtibwa Sugar) na Uhuru Selemani (mkopo, Simba SC).
  Ruvu Shooting; Juma Mdindi, Njaidi Mohamed na Mahmoud Mbulu (Huru),
  Prisons; Mohamed Kayi na Emmanuel Gabriel (Huru).
  JKT Oljoro; Nurdin Selemani, Shaibu Nayopa, Hamidu Hassan, Paul Malipesa, Josephat Moses, Muharami Mnyangamala, Majaliwa Mbaga na Alphonce Peter (Huru)
  Polisi Moro; Shukuru Kassim, Chacha Marwa, Salum Machaku, Mzamiru Said, Victor Bundala, Delta Thomas, Edward Mzeru na Tizzo Chomba (Huru)
  Kagera Sugar; Edmund Kashamila na Julius Mrope (Huru).
  Mtibwa Sugar; Rajab Mohamed, Zakayo Joseph, Baraka Anthony na Mussa Chambo (Huru)
  JKT Ruvu; Zahoro Pazi (mkopo, Azam), Emmanuel Linjechele, Kisimba Luambano na Nashon Naftali (Huru)
  Mgambo JKT; Moaka Shabani, Ismail Mkaima na Damas Milanzi (Huru)
  Toto Africans; Donald Obimma, Exavery Muhollery, Mohamed Hussein na Ulugbe Odia (Huru).
  African Lyon; Obadi Mungusa, Juma Seif, Yusuf Mgwao (Huru), Ibrahim Job (mkopo, Yanga SC) Shamte Ally(mkopo, Yanga SC), Buya Jamwaka, Takang Valentine, Nurdin Mussa, Salvatory Jackson, Mohamed Athuman, Athuman Kajembe na Jarufu Kizombi (Huru)
  Simba SC; Mussa Mudde (Uganda) na Abel Dhaila (Uganda).
  Kipa Abbel Dhaira kulia akibadilishana mikataba na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe kushoto

  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: KIPYENGA CHALIA LEO LALA SALAMA LIGI KUU BARA, NANI ANA NINI? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top