• HABARI MPYA

  Thursday, January 24, 2013

  VODACOM YAONYA UPANGWAJI MATOKEO LIGI KUU, YASEMA INATAKA USHINDANI NA MATOKEO YA UWANJANI

  Meneja Mahusiano ya Nje wa Kampuni ya Vodacom Tanzania, Salum Mwalim (katikati), akizungumza na Waandishi wa Habari katika ukumbi wa mikutano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), zilizopo ndani ya Uwanja wa Karume, Ilala, Dar es Salaam kuhusu Ligi Kuu ya Vodacom, ambayo mzunguko wake wa pili unaanza mwishoni mwa wiki. Wengine kulia ni Ofisa wa Idara ya Masoko, anayeshughulika na masuala ya Udhamini, Ibrahim Kaude na kushoto ni Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura. 

  Na Mahmoud Zubeiry
  WADHAMINI wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kampuni ya Vodacom Tanzania wametoa tahadhari kwa timu zinazoshiriki ligi hiyo, kuendeleza ushindani wa kweli unaozalisha matokeo halisi ya uwanjani, badala ya kupanga matokeo nje ya Uwanja.
  Akizungumza na Waandishi wa Habari, mchana huu katika ukumbi wa mikutano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), uliopo ndani ya Uwanja wa Karume, Ilala, Dar es Salaam kuhusu Ligi Kuu, Meneja Mahusiano ya Nje wa Kampuni ya Vodacom Tanzania, Salum Mwalim alisema kwamba kampuni yake inajisikia fahari kuona soka sasa inachezwa viwanjani zaidi na si nje.
  Akitoa tathmini yake juu ya mzunguko wake wa kwanza wa Ligi Kuu, Mwalim alisema kwamba ulikuwa na ushindani mkubwa na umeleta motisha kwa wachezaji mmoja mmoja na hata kwa mashabiki wa soka nchini.
  “Mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom, umeonyesha taswira ya wapi Ligi Kuu ya Tanzania inaelekea, tumeshuhudia timu kubwa zikienda mikoani zinakabiliana na hali ngumu ya kiushindani, hazijui zitatokaje. Hicho ni kielelzo cha ushindani,”alisema.
  Mwalimu alisema hata kupanda kwa kiwango cha timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars pia ni kielelezo kingine cha kukua kwa Ligi Kuu. “Timu ya taifa imekuwa imara na hata inapokwenda nje ya nchi, imekuwa inakwenda kushindana, sasa si wasindikizaji tena,”alisema Mwalim.
  Aidha, bosi huyo Vodacom na mtangazaji wa zamani wa Televisheni ya Channel Ten ya Dar es Salaam, alisema kwamba imeshuhudiwa pia katika dirisha dogo la usajili timu zinazoshiriki ligi hiyo zikienda mbio kusaka wachezaji wa kuimarisha vikosi vyao.
  “Hii maana yake ligi ni ngumu na ya ushindani, kama kungekuwa hakuna ushindani, timu zisingeenda mbio kuimarisha vikosi vyake,”alisema Mwalim na kuongeza; “Kama wadhamini, hili linatupa moyo sana, kile ambacho tunawekeza ndani yake tunapata matunda,”alisema.
  Mwalim alisema kwamba soka sasa ni uwekezaji mkubwa katika taifa na ni ajira, wachezaji wanalipwa vizuri na wengine wananunuliwa na klabu za nje na kupata mikataba minono.
  “Haya yote ni kielelezo cha ubora wa ligi yetu, kama mtu ananunuliwa nje, maana yake ligi yetu ni ubora na itazidi kumulikwa,”alisema.
  Kuelekea mzunguko wa pili, Mwalim alisema wanazitakia kila la heri timu zinazoshiriki ligi hiyo na wananatarajia kuona ushindani ule ule hasa kwa timu za mikoani.
  Alisema Vodacom walikaa pamoja na Kamati ya Ligi Kuu na TFF na kupitia changamoto mbalimbali ambazo zilijitokeza katika mzunguko wa kwanza na kwamba mambo mengi ambayo yanawahusu moja kwa moja, wameyafanyia kazi.
  “Kabla ya kuanza mzunguko wa pili, tutangaza mambo mengi mapya kuhusu udhamini wetu, kuna mambo yanafanyiwa kazi na yanakwenda vizuri, Menejimenti ilikuwa likizo, sasa wamerudi, wakikamilisha yatatangazwa”alisema.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: VODACOM YAONYA UPANGWAJI MATOKEO LIGI KUU, YASEMA INATAKA USHINDANI NA MATOKEO YA UWANJANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top