• HABARI MPYA

  Jumatatu, Januari 28, 2013

  DHAIRA HUENDA AKAANZA LEO MAZOEZI SIMBA SC

  Dhaira

  Na Mahmoud Zubeiry
  HALI ya kipa wa Simba SC, Abbel Dhaira inaendelea vizuri na leo jioni anaweza kuanza mazoezi kwenye Uwanja wa Sigara, Chang’ombe, Dar es Salaam.
  Msemaji wa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Ezekiel Kamwaga ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba, wataangalia leo jioni kama Dhaira ataweza kufanya mazoezi baada ya kupewa mapumziko ya siku tatu.
  “Baada ya mapumziko ya jana, timu leo inaanza mazoezi, kwa hivyo tutaangalia Dhaira kama atakuwa katika nafasi ya kufanya mazoezi, baada ya kupumzika kwa siku tatu,”alisema Kamwaga.
  Kipa huyo namba moja wa Uganda, hakuingizwa kwenye programu ya mechi ya kwanza ya timu yake ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara juzi dhidi ya African Lyon kutokana na maumivu ya nyonga.
  Katika mchezo huo, ambao Simba iliibuka na ushindi wa mabao 3-1, ‘Tanzania One’ Juma Kaseja alianza langoni na kufanya kazi nzuri, ikiwemo kuokoa mkwaju wa penalti ya Shamte Ally.
  Hata hivyo, refa Israel Mujuni aliyetoa penalti hiyo baada ya beki Paul Ngalema kumkwatua Fred Lewis, aliamuru irudiwe kwa madai Kaseja alitokea kabla ya mpira kupigwa na safari hiyo mpigaji akapiga nje kabisa.
  Kamwaga alisema hata kiungo Mganda ambaye sasa anarudishwa kucheza nafasi ya ulinzi, Mussa Mudde alitolewa kipindi cha pili kwenye mechi dhidi ya Lyon, kutokana na kuumia misuli, hivyo naye ataangaliwa pia jioni ya leo kama atakuwa kwenye nafasi ya kufanya mazoezi.
  Aidha, Kamgwa alisema kikosi cha Simba SC kinarudi kambini leo, katika hoteli maridadi na adilifu ya Sapphire, iliyopo Kariakoo, Dar es Salaam, kujiandaa na mchezo ujao wa Ligi Kuu, dhidi ya JKT Ruvu, Februari 3, mwaka huu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: DHAIRA HUENDA AKAANZA LEO MAZOEZI SIMBA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top