• HABARI MPYA

  Jumatatu, Januari 28, 2013

  HILI NDILO TATIZO LA KIAFYA LA DOMAYO LILILOMFANYA ASHINDWE GHAFLA KUCHEZA JANA

  Frank Domayo jana Uwanja wa Taifa

  Na Mahmoud Zubeiry
  KIUNGO tegemeo wa Yanga SC ya Dar es Salaam, Frank Domayo ana tatizo a kupatwa na kizunguungu ambalo humtokea mara kwa mara na sasa klabu yake hiyo imeamua kulifanyia uchunguzi wa kina ili kulipatia ufumbuzi, imeelezwa.
  Msemaji wa klabu hiyo bingwa Afrika Mashariki na Kati, Baraka Kizuguto ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba, Domayo aliyepatwa na hali hiyo ghafla jana muda mfupi kabla ya timu hiyo kuingia uwanjani kumenyana na Prisons katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kwa sasa yupo chini ya uangalizi wa Daktari wa timu, Nassor Matuzya.
  “Leo tulikuwa na mazoezi kidogo asubuhi, Domayo naye alifanya kidogo mazoezi, ila Daktari akamuambia apumzike, na baada ya mazoezi akaondoka naye kwenda kumfanyia uchunguzi zaidi, taarifa zaidi zitatolewa baadaye,”alisema Kizuguto.
  Domayo jana alizidiwa ghafla Uwanja wa Taifa, akiwa tayari amefika kwenye chumba cha kubadilishia nguo na amevaa jezi akiwa miongoni mwa wachezaji 11 waliopangwa na kocha Mholanzi, Ernie Brandts kuanza mechi hiyo.
  Kutokana na hali hiyo, benchi la ufundi la Yanga lilidhani ni Malaria na kumkimbiza katika Zahanati ya Uwanja wa Taifa, ambako alipatiwa huduma ya kwanza na kupata nafuu.
  Kwa sababu hiyo, ilibidi nafasi yake aanze kiungo mwingine, Nurdin Bakari na timu ikafainiwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-1, hivyo kuzidi kujiimarisha kileleni mwa Ligi Kuu, ikifikisha pointi 32, baada ya kucheza mechi 14, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 27 na Simba 26.
  Hadi mapumziko jana, timu hizo zilikuwa tayari zimefungana bao 1-1, Yanga wakitangulia kupata bao lao dakika ya 10 kabla ya Prisons kusawazisha dakika ya 17.
  Bao la Yanga lilifungwa na Jerry Tegete aliyeunganisha krosi nzuri ya Simon Msuva kutoka wingi ya kulia, wakati la Prisons lilifungwa na Elias Maguri, aliyeunganisha krosi nzuri ya Misango Magai kutoka wingi ya kushoto.
  Yanga walicheza vizuri dakika 15 za mwanzo na baada ya hapo, timu hizo zilianza kushambuliana kwa zamu, ingawa Watoto wa Jangwani ndio waliopoteza nafasi nzuri zaidi za kufunga.
  Kipindi cha pili, Yanga walirudi na kasi nzuri kusaka ushindi na iliwachukua dakika 11 tu kupata bao la pili, lililofungwa na Mbutu Twite baada ya kutokea piga nikupige langoni mwa Prisons.
  Wakati Prisons wakiwa kwenye jithada za kusaka bao la kusawazisha, walijikuta wakitandikwa bao la tatu, Tegete tena akiwainua vitini mashabiki wa Yanga, baada ya kupokea pasi nzuri ya Nurdin Bakari dakika ya 65.
  Baada ya bao hilo, Yanga walianza kuonyesha vitu vya Uturuki walipoweka kambi ya wiki mbili kabla ya kuanza kwa mzunguko huu wa pili wa Ligi Kuu, wakicheza soka ya madoido pasi nyingi, uzungu na kila aina ya mbwembwe, ili mradi tu kuwaburudisha mashabiki wake.
  Yanga itashuka tena dimbani, Februari 2, mwaka huu kumenyana na Mtibwa Sugar, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: HILI NDILO TATIZO LA KIAFYA LA DOMAYO LILILOMFANYA ASHINDWE GHAFLA KUCHEZA JANA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top