• HABARI MPYA

  Jumanne, Januari 29, 2013

  UCHUNGUZI WA DAKTARI WATOA MAJIBU KUHUSU DOMAYO, HANA TATIZO LOLOTE LA KIAFYA ILIKUWA MSHITUKO WA MECHI TU

  Frank Domayo juzi

  Na Mahmoud Zubeiry
  KIUNGO tegemeo wa Yanga SC ya Dar es Salaam, Frank Domayo hana tatizo zaidi la kiafya, uchunguzi wa Daktari wa klabu, Nassor Matuzya umetoa majibu hayo.
  Yanga iliamua kumfanyia uchunguzi wa afya yake Domayo kutokana na kusema hupatwa na kizunguzungu mara kwa mara.
  Msemaji wa klabu hiyo bingwa Afrika Mashariki na Kati, Baraka Kizuguto ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba, uchunguzi wa Daktari umeonyesha kiungo hana tatizo na labda alitokewa na mshituko wa kawaida wa mechi Jumapili, kiasi cha kushindwa kucheza.
  Domayo aliyepatwa na hali hiyo ghafla juzi muda mfupi kabla ya timu hiyo kuingia uwanjani kumenyana na Prisons katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kwa sasa ameruhusiwa kuendelea na mazoezi.
  “Kesho ataungana tena na wenzake mazoezini, baada ya Daktari kuthibitisha huyu mtu hana tatizo lolote,”alisema Kizuguto.
  Domayo juzi alizidiwa ghafla Uwanja wa Taifa, akiwa tayari amefika kwenye chumba cha kubadilishia nguo na amevaa jezi akiwa miongoni mwa wachezaji 11 waliopangwa na kocha Mholanzi, Ernie Brandts kuanza mechi hiyo.
  Kutokana na hali hiyo, benchi la ufundi la Yanga lilidhani ni Malaria na kumkimbiza katika Zahanati ya Uwanja wa Taifa, ambako alipatiwa huduma ya kwanza na kupata nafuu.
  Kwa sababu hiyo, ilibidi nafasi yake aanze kiungo mwingine, Nurdin Bakari na timu ikafainiwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-1, hivyo kuzidi kujiimarisha kileleni mwa Ligi Kuu, ikifikisha pointi 32, baada ya kucheza mechi 14, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 27 na Simba 26. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: UCHUNGUZI WA DAKTARI WATOA MAJIBU KUHUSU DOMAYO, HANA TATIZO LOLOTE LA KIAFYA ILIKUWA MSHITUKO WA MECHI TU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top