• HABARI MPYA

    Monday, January 28, 2013

    YANGA MTAMBO WA KUTENGENEZA FEDHA

    Mfungaji wa mabao mawili ya Yanga jana, Jerry Tegete kushoto akiwatoka wachezaji wa Prisons

    Na Prince Akbar
    KWELI Yanga ni mtambo wa kutengeneza fedha, acha wajanja waitumie kujinufaisha. Wakati mechi ya ufunguzi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kati ya Simba SC na African Lyon juzi iliingiza kiasi cha Milioni 53 tu, mchezo wa jana wa ligi hiyo kati ya Yanga na Tanzania Prisons umeingiza Sh. Milioni 101.
    Jumla ya kiasi kilichopatikana katika mchezo huo ambao ni Sh. 101,016,000 ikiwa ni karibu zaidi ya nusu ya pato la mchezo wa juzi.
    Taarifa ya Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura imesema mechi hiyo namba 94 iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 3-1, watazamaji 17,946 walikata tiketi kushuhudia pambano hilo kwa viingilio vya sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000.
    Wambura amesema watazamaji 16,158 kati ya hao walikata tiketi za sh. 5,000 wakati idadi ndogo ya washabiki ilikuwa ni 98 waliokata tiketi za sh. 20,000 na kila klabu imepata mgawo wa sh. 24,314,752.45 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 15,409,220.34. Asilimia 15 iliyokwenda kwenye uwanja baada ya kuondoa VAT na gharama za tiketi ni sh. 12,363,433.45.
    Amesema mgawo mwingine wa mapato hayo ni tiketi sh. 3,183,890, gharama za mechi sh. 7,413,060.07, Kamati ya Ligi sh. 7,418,060.07, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 3,709,030.03 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 2,884,801.14.
    Ikumbukwe mechi namba 92 juzi Uwanja wa Taifa pia iliyomalizika kwa Simba kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya African Lyon, iliingiza Sh. 53,756,000.
    Watazamaji 9,408 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo iliyochezwa kwa viingilio vya sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 12,499,752.45 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 8,200,067.80.
    Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya Uwanja sh. 6,355,806.33, tiketi sh. 3,183,890, gharama za mechi sh. 3,813,483.80, Kamati ya Ligi Sh. 3,813,483.80, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) Sh. 1,906,741.90 na Chama cha Soka Dar es Salaam (DRFA) Sh. 1,483,021.48.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: YANGA MTAMBO WA KUTENGENEZA FEDHA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top