• HABARI MPYA

  Jumapili, Januari 27, 2013

  KWELI WACHEZAJI WAZURI WALIKUWA ZAMANI, NA VIONGOZI NAO!

  Na Bin Zubeiry

  KUNA mijadala huibuka na kujirudia na kujirudia kuhusu wachezaji wa kizazi cha sasa na wale wa vizazi vilivyopita, wapi ni bora zaidi.
  Mara nyingi wachezaji wa zamani humwagiwa sifa na wa sasa hukandiwa si lolote, watu wanakumbuka zamani, wanasema wakati huo ndipo soka ilikuwa inapambwa na wachezaji wa ukweli.
  Sitaki kupingana na hili, lakini naweza tu kulijadili kwa kina suala hili, nini tatizo la wanasoka wa leo au soka yetu kwa ujumla?
  Bahati nzuri nimeanza kuwa karibu na viongozi wa soka na wachezaji tangu miaka ya 1990, wakati naanza kuandika habari za michezo, kuanzia gazeti la Mfanyakazi, baadaye Dimba ambako nilistaafu Mei mwaka jana na kuwa mwandishi wa kujitegemea.
  Nimejifunza mengi sana juu ya wachezaji na viongozi kwa ujumla wa wakati huo na wa sasa na kwa muhtasari naweza kusema kuna tofauti kubwa, ambayo inasababishwa na mambo mengi, kubwa ni aina ya viongozi wa sasa.
  Viongozi wa sasa ni tatizo kubwa, wengi wapo kwa maslahi yao binafsi, kuitumia soka kujinufaisha kwa kipato na kusaka umaarufu.
  Miaka ya nyuma, fedha haikuwa kigezo cha mtu kupewa uongozi haswa katika klabu za Simba na Yanga- kama mtu ana fedha na anapenda timu anaweza akawa mfadhili tu na kupewa heshima kubwa, lakini suala la uongozi lilikuwa lina watu wa aina yake.
  Hatukuwa na viongozi wasomi sana, na wengine hawakuwa na elimu ya darasani kabisa, lakini waliweza kuongoza soka, kuwaheshimu wachezaji na kuishi nao vizuri.
  Kuna wakati, Edibily Jonas Lunyamila akiwa juu sana soka, aliendelea kuichezea Yanga chini ya Mwenyekiti Rashid Ngozoma Matunda (sasa marehemu), na japo hakuwa na fedha wala shule.
  Mzee Matunda alikuwa ana hekima na busara na alijua namna ya kuishi na wachezaji na ndio maana Lunyamila alijisikia raha kuicheza Yanga japo haikuwa na fedha. Chini ya Matunda, Yanga iliweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza nchini kufika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
  Najaribu kukumbuka namna wachezaji wa wakati ule walivyokuwa wanathaminiwa na viongozi wao, wanaheshimiwa na hiyo ilikuwa moja ya sababu ya wao kucheza muda mrefu.
  Madaraka Suleiman aliyeanza kucheza soka miaka ya 1970 aliichezea Simba hadi mwaka 2003 akiwa mtu mzima sana- kwa nini? Viongozi wa wakati huo walimheshimu na wakajua namna ya kumtumia licha ya umri wake mkubwa sana wakati huo.
  Lakini Said Maulid ‘SMG’ aliyeanza kucheza Ligi Kuu mwaka 2000 katika klabu ya Simba, kabla ya 2001 kuhamia Yanga, alikocheza hadi 2007 alipohamia Angola, sasa Yanga hawataki hata kumsikia.
  Baada ya kumaliza mkataba wake Angola, mwishoni mwa mwaka jana, SMG aliomba amalizie soka yake Yanga, klabu aliyoichezea kwa mapenzi yake yote, lakini hakupewa nafasi hiyo. Na mbaya zaidi alifanyiwa dharau sana.
  Mussa Hassan Mgosi aliyeanza kucheza Ligi Kuu mwaka 2001 pia, alitamani sana  baada ya kumaliza mkataba wake DRC amalizie soka yake Simba SC, klabu aliyoitumikia kwa mapenzi yake yote, lakini hakuipata nafasi hiyo.
  Emmanuel Gabriel na Ulimboka Mwakingwe waliachwa Simba eti wamekuwa wazee, lakini klabu baadaye ikamsajili mchezaji ambaye labda ni rika la akina Jamhuri Kihwelo, Paschal Ochieng.
  Viongozi wengi wa kisasa wanawadharau sana wachezaji. Kuna kiongozi mmoja wa Simba, alimkandia Uhuru Suleiman, eti hawezi kupata namba hata TASWA, ile timu ya Waandishi wa Habari za michezo, lakini bahati yake kiungo yuyo sasa hivi yupo Azam.
  Kwenye Katiba zetu, katika kanuni za uchaguzi kuna kipengele cha uzoefu wa mgombea kabla ya kugombea uongozi katika ngazi za juu, lakini umekuwa ukitumika ujanja ujanja tu kupitisha watu ambao hawana uzoefu na madhara yake ndiyo haya, tunaingiza watu mafedhuli, wajivuni, washamba wanakuja kutuharibia soka yetu.
  Watu wanajifanya wajuaji, wakati hawajui lolote na wanazitia hasara za mamilioni hata kampuni zao kwa ujuaji wao. Watu wenye tamaa ya fedha, wanafikiria fedha tu. Wanataka kupata fedha nyingi na utajiri wa haraka haraka kupitia mpira. Tatizo sana.
  Inawezekana kabisa mchezaji wa Tanzania wa leo akacheza hata miaka 20, iwapo atakuwa chini ya viongozi wadilifu, wenye busara na kuijua soka. Siyo hawa watafuta maisha wa leo.
  Mchezaji amekwishatumika mathalani miaka nane, kuna namna yake ya kumtumia ili acheze muda mrefu. Huyo hata mazoezi yake ni tofauti na wachezaji chipukizi. Hassan Afif alikuwa mtu mzima na kibonge mwaka 1991 akiwa kocha mchezaji Simba na kuiwezesha timu kutwaa Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, tangu 1974.
  Alikuwa akiingia kutokea benchi, anakwenda kuiongoza timu vema na mara nyingi alikuwa chachu ya ushindi. Hata matokeo yakiwa 0-0, enzi zile akiinuka tu Afif, jukwaa linaripuka kwa shangwe, wanajua mabao yanakuja. Vipi leo?
  Ni kweli kuna wachezaji mafedhuli, hao walikuwepo tangu zamani, lakini bado tuna tatizo la viongozi ambao hawajui namna ya kuishi na wachezaji.
  Viongozi wanawakatisha tamaa wachezaji, tena sana. Hivi SMG kama angesajiliwa Yanga au Mgosi Simba, wangezipunguzia nini klabu kama si kuzinufaisha kwa uzoefu wao? Samahani wapendwa wasomaji wangu, pamoja na yote niliyoeleza lakini naongeza kuna watu waliopewa mamlaka kwenye klabu wana roho mbaya!
  Wakati mwingine wachezaji wanadai haki zao za msingi, tena zilizomo kwenye mikataba matokeo yake wanaitwa watovu wa nidhamu na wanafukuzwa kwenye timu.
  Anayefanya hivyo hajali uwezo wa mchezaji na mchango wake kwenye timu, je kwa mtaji huu tutafika kweli? Naungana na mawazo ya mengi, wachezaji wa ukweli walikuwa zamani, lakini hata wa sasa wanashindwa kufikia kiwango cha wachezaji wa zamani kwa sababu ya kukwazwa na viongozi wetu wa leo. Alamsiki. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: KWELI WACHEZAJI WAZURI WALIKUWA ZAMANI, NA VIONGOZI NAO! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top