• HABARI MPYA

    Sunday, September 16, 2018

    YANGA SC YASHINDA MECHI YA PILI MFULULIZO LIGI KUU KWA TOFAUTI YA BAO MOJA TU

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    VIGOGO, Yanga SC wamepata ushindi wa mbinde wa mabao 4-3 kutoka kwa Stand United ya Shinyanga katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara uliofanyika Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
    Yanga SC inafikisha pointi sita katika mechi mbili za mwanzo za Ligi Kuu, zote ikishinda kwa tofauti ya bao moja, baada ya kuichapa Mtibwa Sugar 2-1 katika mchezo wake wa kwanza, wakati Stand United inabaki na pointi zake sita baada ya mechi nne. 
    Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Benedict Magai aliyesaidiwa na Michael Mkongwa na Mashaka Mwandembwa, hadi mapumziko Yanga walikuwa mbele kwa mabao 3-1.
    Wachezaji wa Yanga SC kutoka kulia Mrisho Ngassa, Papy Tshishimbi na Deus Kaseke baada ya bao la kwanza  
    Mrisho Ngassa akimtoka beki wa Stand United leo Uwanja wa Taifa 

    Kiungo Papy Kabamba Tshishimbi akitoka mchezaji wa Stand United leo

    Mkongwe, Mrisho Khalfan Ngassa alianza kufunga kwa ustadi mkubwa bao la kwanza dakika ya pili tu akimalizia pasi ndefu ya Ibrahim Ajib, kabla ya Alex Kitenge kuisawazishia Stand United dakika ya 15 kwa shuti kali akiwa katikati ya mabeki kufuatia pasi ya Sixtus Sabilo.
    Ajib akaifungia Yanga bao la pili dakika ya 32 kwa shuti kali baada ya pasi ya Papy Kabamba Tshishimbi kabla ya kumsetia beki Andrew Vincent ‘Dante’ kufunga la tatu dakika ya 35.
    Kiungo mshambuliaji aliyerejea Yanga SC baada ya msimu mmoja wa kuwa na Singida United akaifungia timu hiyo bao la nne dakika ya 57 kwa shuti zuri kabla ya Kitenge kuifungia tena Stand United dakika ya 59.
    Mshambuliaji mjanja, Alex Kitenge kwa mara nyingine akatumia makosa ya kipa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Klaus Kindoki kufunga hat trick ya kwanza ya msimu huu wa Ligi Kuu akiifungia Stand United bao la tatu dakika ya 90 na ushei.  
    Kikosi cha Yanga kilikuwa; Klaus Kindoki, Paulo Godfrey, Gardiel Michael, Andrew Vincent, Kevin Yondan/Abdallah Shaibu ‘Ninja’ dk80, Feisal Salum, Mrisho Ngassa/Yussuf Mhilu dk62, Papy Kabamba Tshishimbi, Heritier Makambo, Ibrahim Ajib/Raphael Daudi dk62 na Deus Kaseke.
    Stand United; Mohammed Makaka, Bigirimana Ramadhani, Ndoriyabija Eric, Erick Mulilo, Niyonkuru Nassor, Erick Mbirizi, Datius Peter/Charles Chinongo dk55, Jackob Massawe, Alex Kitenge, Hafidh Mussa na Sixtus Sabilo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA SC YASHINDA MECHI YA PILI MFULULIZO LIGI KUU KWA TOFAUTI YA BAO MOJA TU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top