• HABARI MPYA

    Sunday, September 02, 2018

    KILA MTU AJIFUNZE KUTOKANA NA KOSA LAKE, KILA LA HERI TAIFA STARS!

    MEI mwaka 2016, aliyekuwa Nahodha wa klabu ya Yanga, Nadir Haroub Ally ‘Cannavaro’ alijiondoa kwenye kikosi cha timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kilichokuwa chini ya kocha Charles Boniface Mkwasa.
    Cannavaro alifanya hivyo baada ya kuvuliwa Unahodha wa Taifa Stars na Mkwasa aliyeamua kumpa mshambuliaji, Mbwana Ally Samatta anayecheza Ulaya.
    Mapema Januari mwaka 2016, kama miezi minne tangu apewe ukocha wa Taifa Stars baada ya kufukuzwa kwa Mholanzi, Mart Nooij, Mkwasa alitangaza mabadiliko ya Unahodha Taifa Stars akimteua Samatta badala ya Cannavaro.
    Na Mkwasa alifanya hivyo baada tu ya Samatta kununuliwa na klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji kutoka TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) akitoka kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Afrika, kuwa mfungaji bora wa michuano hiyo na kushinda tuzo ya Mwanasoka Bora Anayecheza Afrika.

    Mkwasa alisema kwamba ili kumpa heshima zaidi Samatta na kumfanya ajione mwenye majukumu ya kuibeba timu yake ya taifa, anamkabidhi beji ya Unahodha. Hakuna aliyepingana na Mkwasa wakati ule.  
    Na hata Cannavaro alipogoma kwa sababu zile zile, hakuna aliyepingana naye na hilo likaisha kimya kimya, tu huo ukawa mwisho wa maisha yake timu ya taifa yaliyoanza mwaka 2005, baada ya kuitwa kwa mara ya kwanza na Dk. Mshindo Msolla, aliyekuwa Kocha Taifa Stars wakati huo.   
    Ni Nooij aliyempa Unahodha Cannavaro Mei mwaka 2014 mara tu baada ya kupewa mikoba ya kufundisha Taifa Stars akichukua nafasi ya Mdenmark, Kim Poulsen. Kwa kipindi kirefu baada ya kustaafu kwa Nsajigwa Shadrack mwaka 2012, Nahodha wa Taifa Stars alikuwa Juma Kaseja.
    Ukiachana na sakata la Cannavaro na Mkwasa, wachezaji wengine waliokuwa wanasumbua wakiitwa Taifa Stars ni mabeki Aggrey Morris wa Azam FC na Kelvin Yondan wa Yanga SC, nao kwa sababu binafsi pia ambazo hazikuwahi kuwekwa wazi.
    Na kama itakumbukwa, Yondan ndiye angekuwa Nahodha wa Taifa Stars katika kikosi cha Nooij badala ya Cannavaro kama asingegoma kujiunga na timu Mei mwaka 2016, tabia ambayo ameendelea nayo hata kwa makocha waliofuatia. 
    Hakuna hatua walizowahi kuchukuliwa Yondan na Cannavaro au Aggrey kwa ukaidi wao wa kujiunga na timu na katika kipindi chote hiki imekuwa kawaida kusoma habari za wachezaji kuchelewa kujiunga na Taifa Stars kwa sababu mbalimbali.
    Wachezaji wa Tanzania, haswa wale wanaochezea timu kubwa, yaani hizi zenye mashabiki wengi, kwao kuchelewa kujiunga na timu ya taifa imekuwa si kesi – sana wamekuwa wakipigwa mikwara kupitia vyombo vya habari kwamba wasipofika hadi muda fulani watachukuliwa hatua ndipo nao hujitokeza.
    Kumekuwa kuna maisha fulani ya kubembelezwa kwa wachezaji wanaoitwa nyota wa Taifa Stars na hakukuwahi kutokea hatua zozote za kupambana na hali hiyo.
    Pamoja na hayo, kwa miaka ya karibuni kesi za matatizo ya nidhamu za wachezaji, kuchelewa kujiunga na Taifa Stars tumezisahau, lakini wiki hii zimeibuka tena.       
    Mjadala mkubwa wiki hii umekuwa ni kufukuzwa kwa wachezaji saba wa Taifa Stars katika kambi ya maandalizi ya mchezo dhidi ya Uganda Septemba 8 utakaofanyika mjini Kampala.
    Kocha mpya, Mnigeria, Emmanuel Amunike amewaondoa kikosini mabeki Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, viungo Jonas Mkude, Hassan Dilunga, Shiza Kichuya na mshambuliaji John Bocco wa Simba pamoja na kiungo wa Yanga, Feisal Salum baada ya kukaidi kuripoti mwanzoni mwa wiki.
    Hatua hiyo iliwashitua wengi na kuanzia Jumatano mjadala mkubwa nchini Tanzania ukawa juu ya uamuzi huo, wengine wakimuunga mkono mwalimu na wengine wakiona kama hatua zilizochukuliwa hazikuwa sahihi.
    Wanaomuunga mkono kocha ni wale wanaoamini moja kwa moja wachezaji hao walikaidi wito wa kujiunga na timu kwa wakati waliotakiwa wakiuchukulia huo ni utovu wa nidhamu.
    Na wanaopinga ni wale wanaoamini juu ya uwezo wa wachezaji walioondolewa ambao pamoja na kukiri nyota hao walikosea, lakini wanaona walistahili kuelimishwa kwanza na kaumbiwa kwamba sasa tupo katika zama mpya za kocha Amunike anayetaka nidhamu na utii. 
    Ni kweli tunahitaji nidhamu katika timu ya taifa kama tunahitaji mafanikio ya kweli – japo ya kiwango fulani tu, yasiwe ya juu.
    Na uzuri ni kwamba wachezaji wetu wamekuwa hawana desturi ya utovu wa nidhamu, ukaidi mbele ya makocha wa kigeni – labda kwa sababu muda mrefu tumekuwa tukitumia makocha wa kigeni Wazungu tu, ukiondoa Mkenya marehemu James Sianga mwanzoni mwa miaka ya 2000. 
    Alipokuwa nchini, kocha Mbrazil Marcio Maximo kati ya 2006 na 2010 kama kocha wa Taifa Stars alikuwa hataki watovu wa nidhamu kikosini mwake na ilishuhudiwa akiacha kuwaita wachezaji walioonekana wana uwezo mkubwa, tu kwa sababu za kinidhamu.
    Na aliwaondoa pia wachezaji waliokuwa tegemeo kikosini kwake kwa sababu za kinidhamu pia, jambo ambalo mwisho wa siku lilimletea shida na likachangia safari yake japo alifanikiwa kuipeleka timu CHAN mwaka 2009 na kuibua vipaji vipya.
    Wachezaji waliochelewa kuingia kambini Taifa Stars wiki hii walikosea – lakini suala hili lingekuwa dogo kama kocha Amunike angetulizwa na kuombwa avute subira akutane nao kwanza.
    Kwa sababu, wakati Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wilfred Kidau anazungumza na Waandishi wa Habari Uwanja wa Karume akitangaza kuwafukuza wachezaji hao, nao ndiyo walikuwa wanafika kambini na wakafanya kikao na Amunike.
    Mwisho wa siku Amunike akawasamehe wachezaji hao, lakini kwa sababu alikuwa amekwishaita wachezaji wengine kukawa hakuna nafasi ya wao kurejeshwa. Msamaha uliotolewa ndani ya saa mbili baada ya hatua kuchukuliwa, japo ilitangazwa saa 24 baadaye.
    Na ikumbukwe wachezaji hao walichelewa kwa saa mbili tu, kwani walitakiwa kufika saa 2:00 asubuhi, wao wakaripti baada ya saa 4:00 na kufanya kikao na kocha.  
    Tukiri wachezaji walikosea na hiyo ni kwa sababu ya mazoea na desturi, lakini kama tunaazimia kuingia kwenye zama mpya za kuzingatia nidhamu kwa kiasi hicho tulipaswa kuwa na mwanzo – kwani hatua nzito kama hizi mara nyingi huwa na gharama kubwa ambazo si vyema kujiruhusu kuzibeba kwa urahisi.
    Tumetumia muda mrefu na gharama kubwa kutengeneza timu hadi kupata muunganiko mzuri uliotupa ushindi wa 2-0 dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) katika mchezo wa mwisho Machi 27, mwaka huu Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam ambao ulikuwa wa maandalizi ya mchezo ujao na Uganda.
    Tuseme kama walivyosema mjadala umefungwa na tuitakie kila la heri Taifa Stars kuelekea mchezo na Uganda Septemba 8, lakini katika hili kila mtu ajifunze kutokana na kosa lake.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KILA MTU AJIFUNZE KUTOKANA NA KOSA LAKE, KILA LA HERI TAIFA STARS! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top