• HABARI MPYA

    Friday, January 11, 2013

    OKWI AMESHINDIKANA SIMBA SC

    Okwi

    Na Prince Akbar
    AMESHINDIKANA. Emmanuel Arnold Okwi, mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda anayechezea Simba SC ya Dar es Salaam ameondolewa kabisa katika programu ya kambi ya timu hiyo nchini Oman.
    Hiyo inafuatia mshambuliaji huyo wa Uganda kutowasili Dar es Salaam hadi sasa na mbaya zaidi hata anapopigiwa simu na viongozi wa klabu hiyo hapokei.
    “Okwi tumemuondoa kabisa katika programu ya Oman, hatuwezi kubembeleza mchezaji kiasi hiki,”alisema Makamu Mwenyekiti wa Simba SC, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ leo alipozungumza na BIN ZUBEIRY.
    Okwi anaifanyia Simba SC ‘nyodo’ hizo akitoka kusaini mkataba mpya wa miaka miwili, Desemba mwaka jana na kuongezewa mshahara kwa zaidi ya nusu, hadi kuwa Sh. Milioni 3. 
    Kaburu alisema kwamba baada ya kundi la kwanza kuondoka juzi, kundi lingine la wachezaji waliokuwa Zanzibar kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi litaondoka leo na kesho.
    Amesema wachezaji walio na timu ya taifa, Taifa Stars nchini Ethiopia wataondokea nchini humo kwenda Oman, baada ya mechi dhidi ya Wahabeshi kesho
    Simba SC itakuwa kambini Oman kwa wiki mbili tangu jana ikijifua kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara pamoja na Ligi ya Mabingwa Afrika.
    Ikiwa huko, Simba SC itapatiwa kambi ya mazoezi na mechi tatu za kujipima nguvu, kujiandaa na changamoto zinazowakabili mbele.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: OKWI AMESHINDIKANA SIMBA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top