• HABARI MPYA

    Saturday, January 12, 2013

    NI AZAM AU TUSKER BINGWA MAPINDUZI LEO?

    Kikosi cha Azam

    Na Mahmoud Zubeiry, Zanzibar
    BINGWA wa 11 wa Kombe la Mapinduzi, anatarajiwa kupatikana leo kwenye Uwanja wa Amaan, visiwani hapa wakati Tusker FC ya Kenya itakapomenyana na Azam FC ya Dar es Salaam.
    Azam FC ambao ndio mabingwa watetezi wa michuano hii, waliingia fainali baada ya kuwatoa Simba kwa penalti 5-4, kufuatia sare ya 2-2 ndani ya dakika 120, wakati Tusker dakika 90 ziliwatosha kuwang’oa Miembeni ya hapa kwa kuwachapa 2-0.
    Mchezo huo unatarajiwa kuwa mkali na wa kusisimua kutokana na ubora wa soka wa timu zote katika mashindano haya tangu yanaanza Januari 2, Tusker wakitokea A lililokuwa na timu kali kama Simba na Jamhuri, Azam kundi B lililokuwa na timu kali pia za Miembeni, Mtibwa Sugar na Coastal Union.
    Nahodha wa Tusker, Joseph Shikokoti amerudia kusema kwamba Azam hawatawazuia kutwaa Kombe leo.
    “Tutawafunga Azam, hawawezi kutuzuia kutwaa hili Kombe, tumewaona wanavyocheza na tunakiri ni timu nzuri, lakini tutawafunga tu,”alisema beki huyo wa zamani wa Yanga alipozungumza na BIN ZUBEIRY jana.   
    Kwa upande wake, Kocha Msaidizi wa Azam FC, Muingereza Kali Ongala amesema kwamba wana matumaini ya kubeba Kombe la Mapinduzi leo, ingawa anakiri utakuwa mtihani mzito kwa sababu wapinzani wao, Tusker FC ya Kenya ni timu nzuri.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana, Kali alisema kwamba Wakenya wanawazidi Watanzania mambo mengi sana kisoka, lakini kwa hali yoyote Azam itapambana kubakisha taji nyumbani.
    “Itakuwa mechi ngumu, kama ulivyoiona Tusker ni timu nzuri kwa kweli, imekamilika kila idara, lakini sisi pia tuna timu nzuri na tutapigana kufa na kupona,”alisema mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga SC.
    Pamoja na hayo, Kali ameomba wapenzi wa soka Zanzibar kujitokeza kwa wingi leo uwanjani kuishangilia Azam FC kwa sababu ni timu ya nyumbani, ili iweze kubakiza taji hilo.
    “Sisi ni timu ya Tanzania, na Zanzibar ni sehemu ya Tanzania, hivyo tunaomba mashabiki wajitokeze kwa wingi kutushangilia ili tuweze kubakiza taji hapa nyumbani,”alisema.
    Azam wanatumia mfumo wa kushambulia moja kwa moja mipira mirefu na viungo wake karibu wote wanakuwa na jukumu la kukaba zaidi ya viungo wa pembeni ambao hushambulia moja kwa moja.
    Tusker wao wanapiga mipira mirefu na ni hatari sana kwa mipira ya kutokea pembezoni mwa Uwanja.
    Timu zote zina safu imara za ulinzi na kiungo na mabeki wake wana desturi ya kupanda kusaidia mashambulizi wakati wa mipira ya kona kwenye lango la wapinzani.
    Safu ya ushambuliaji ya Azam leo itamtegemea Mganda Brian Umony kwani hakuna uhakika wa Gaudence Mwaikimba kuanzishwa kutokana na kuonekana kupoteza nafasi nyingi za kufunga katika mashindano haya, ambayo hadi sasa amefunga bao moja tu.
    Tusker watakuwa na kinara wa mabao wa mashindano haya, Jesse Were ambaye hadi sasa amefunga mara nne.
    Kwa ujumla, kikosi cha Azam leo kinatarajiwa kuwa; Mwadini Ally, Himid Mao, Samir Hajji Nuhu, David Mwantika, Joackins Atudo, Kipre Balou, Uhuru Suleiman, Abdulhalim Humud, Brian Umony, Humphrey Mieno na Uhuru Suleiman.
    Tusker FC; Samuel Odhiambo, Luke Ochieng, Bright Jeremiah, Mark Odhiambo, Joseph Shikokoti, Frederick Onyango, Justine Monga, Khalid Aucho, Jesse Were, Ismail Dunga na Robert Omonok.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: NI AZAM AU TUSKER BINGWA MAPINDUZI LEO? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top