• HABARI MPYA

    Wednesday, September 12, 2018

    UADILIFU NI PAMOJA NA KUHAKIKISHA FEDHA ZA WADHAMINI WA MASHINDANO ZINAWAFIKIA WALENGWA KWA WAKATI

    Na Mahmud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    MACHI 15, mwaka huu, Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ilimfungia maisha Makamu wa Rais wa shirikisho hilo, Michael Wambura kutojihusisha na masuala ya soka kwa makosa matatu.
    Taarifa ya TFF siku hiyo ilisema kwamba hatua hiyo imechukuliwa kwa mujibu wa kifungu cha 73(1) (c) cha Kanuni za Maadili ya TFF Toleo la 2013. 
    Hiyo ni baada ya kikao chake cha Machi 14, mwaka huu ambacho pamoja na mambo mengine, kilimjadili Wambura aliyefikishwa kwenye kamati hiyo kwa makosa matatu ya kupokea fedha za TFF malipo yasiyo halali, kugushi barua na kushusha hadhi ya TFF.
    Wambura alifikishwa kwenye kamati ya Maadili na Sekretarieti ya TFF baada ya Kamati ya Ukaguzi kukutana na kupitia mambo mbalimbali ya ukaguzi na suala hilo la Wambura kuonekana linatakiwa kufika kwenye Kamati ya Maadili.

    Mtibwa Sugar wakisherehekea na taji lao la Azam Sports Federation Juni 2, mwaka huu mjini Arusha

    Na Agosti 27, mwaka huu, Kamati hiyo hiyo ya Maadili ikamfungia maisha kutojishughulisha na mchezo huo aliyekuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya shirikisho hilo na Msimamizi wa kituo cha Shinyanga, Mbasha Matutu kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake.
    Matutu alifungiwa baada ya kikao cha Kamati ya Maadili kilichofanyika Jumamosi ya Agosti 25, mwaka huu makao makuu ya shirikisho hilo, Uwanja wa Karume mjini Dar es Salaam kumtia hatiani kwa makosa matatu ambayo ni ubadhirifu, kughushi na kuiba mambo ambayo ni kinyume na Kanuni za Maadili za TFF na Ligi Kuu.
    Na jana, Kamati hiyo hiyo Maadili ya TFF imemfungia Meneja wa Simba SC, Richard Robert kujihusisha na soka kwa mwaka mmoja na faini ya Sh. Milioni 4.
    Hiyo ni baada ya Kamati hiyo chini ya Mwanyekiti wake, Hamidu Mbwezeleni kumkuta na makosa mawili ya kuihujumu timu ya taifa na kushindwa kutii agizo la TFF – lakini atatumikia kifungo cha miezi sita kutokana na adhabu zake kwenda sambamba. 
    Mbwezeleni alisema katika mkutano na Waandishi wa Habari jana kwamba adhabu ya kuhujumu ni kwa mujibu wa kifungu 5 (2), kifungu cha 6 (c) na (h) vya Kanuni za Maadili za TFF toleo la 2013 na adhabu ya kutotii maagizo ya TFF ni kwa mujibu wa kifungu cha 41 (8) cha kanuni za ligi kuu toleo la 2013.
    Robert anadaiwa kuwa sababu ya wachezaji wa Simba SC, mabeki Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, viungo Jonas Mkude, Hassan Dilunga, Shiza Kichuya na mshambuliaji John Bocco wa Simba kutojiunga na kambi ya timu ya taifa, Taifa Stars wiki iliyopita kwa ajili ya mchezo dhidi ya Uganda Jumamosi.
    Kocha mpya wa Tafa Stars, Mnigeria, Emmanuel Amunike aliwaondoa wachezaji hao sita wa klabu bingwa ya Tanzania pamoja na kiungo wa Yanga, Feisal Salum baada ya kukaidi kuripoti mwanzoni mwa wiki iliyopita.
    Lakini baada ya uchunguzi wake TFF juu ya sakata hilo, imemshushia rungu Meneja huyo wa Simba SC, siku mbili tu baada ya Taifa Stars kulazimisha sare ya 0-0 na Uganda mjini Kampala.
    Na mapema wiki hii, Mtibwa Sugar ya Morogoro walilalamika kutopatiwa fedha zao za ushindi wa Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) Sh. Milioni 50, ambazo hutolewa na wadhamini Azam TV.
    Taarifa zaidi zinasema kwamba hata wachezaji walioshinda tuzo binafasi, kama Mchezaji Bora, Hassan Dilunga, Mfungaji Bora Habib Kiyombo na wengine nao hawajapatiwa zawadi zao.
    Juni 2, mwaka huu Mtibwa Sugar ilitwaa Komba la TFF baada ya ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Singida United jioni ya leo Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha.
    Na habari zinasema wadhamini, Azam TV wamekwishatoa fungu lote la udhamini wa mashindano hayo kwa msimu uliopita, lakini bado wahusika hawajapatiwa stahiki zao.
    Uadilifu ni pamoja na kuhakikisha fedha zinazotolewa na wadhamini na wafadhili kwa ajili ya mashindano au chochote zinawafikia walengwa kwa wakati – kama hadi leo washindi wa ASFC hawajapatiwa zawadi zao hli ni doa kwa TFF.
    Na mbaya zaidi timu na wachezaji kuibuka wakati huu kudai fedha zao za zawadi kwa mashindano ambayo yalimalizika Juni inawachafua hadi wadhamini, Azam TV wanaonekana kama wao ndiyo hawajatimiza wajibu wao. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: UADILIFU NI PAMOJA NA KUHAKIKISHA FEDHA ZA WADHAMINI WA MASHINDANO ZINAWAFIKIA WALENGWA KWA WAKATI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top