• HABARI MPYA

    Tuesday, September 04, 2018

    SAMATTA NA ULIMWENGU WAINGIA KAMBINI TAIFA STARS…WA HISPANIA KUWASILI LEO, MSUVA NA HIMID MAO…

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    WASHAMBULIAJI Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wamewasili nchini Alfajiri ya leo kujiunga na timu ya taifa kwa ajili ya mchezo wa kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika dhidi ya Uganda mjini Kampala Jumamosi.
    Samatta ambaye pia ni Nahodha wa Taifa Stars, ametokea Ubelgiji anakochezea klabu ya KRC Genk, wakati Ulimwengu ametokea Sudan anakochezea klabu ya El HIlal Omduran.
    Wanafanya idadi ya wachezaji wanaocheza nje walioripoti Taifa Stars kufika wanne, baada ya juzi mshambuliaji wa BDF XI ya Botswana, Rashid Mandawa kuwa wa kwanza kuingia akifuatiwa na beki wa Nkana FC, Hassan Kessy jana.
    Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu baada ya kuwasili nchini Alfajiri ya leo

    Kiungo Farid Mussa na mshambuliaji Shaaban Iddi Chilunda wa CD Tenerife ya Hispania wanatarajiwa kuwasili Saa 5:00 asubuhi ya leo wakifuatiwa na beki Abdi Banda wa Baroka FC ya Afrika Kusini, viungo, Himid Mao wa Petrojet ya Misri na Simon Msuva wa Difaa Hassan El-Jadida ya Morocco.
    Matarajio ni hadi kufika kesho wachezaji wote wa Taifa Stars wawe wamekamilika tayari kwa safari ya Kampala kwa ajili ya maandalizi ya mchezo huo wa Kundi L kufuzu AFCON ya mwakani nchini Cameroon.
    Wachezaji wengine waliopo kambini Taifa Stars ni makipa Aishi Manula wa Simba SC, Benno Kakolanya wa Yanga SC na Mohammed Abdulrahman Wawesha wa JKU, mabeki David Mwantika wa Azam FC, Ally Sonso, Paul Ngalema wa Lipuli FC ya Iringa, Gardiel Michael, Kelvin Yondan na Andrew Vincent ‘Dante’ wa Yanga SC, Aggrey Morris, viungo ni Salum Kimenya wa Tanzania Prisons ya Mbeya, Frank Domayo wa Azam FC, Salum Kihimbwa wa Mtibwa Sugar, Mudathir Yahya na washambuliaji Yahya Zayed wa Azam FC na Kelvin Sabato wa Mtibwa Sugar. 
    Kocha Mnigeria, Emmanuel Amunike aliyesaini mkataba wa kufundisha Taifa Stars mapema Agosti, ambaye anasaidiwa na Mnigeria mwenzake, Emeka Amadi na Mzalendo, Hemed Suleiman ‘Morocco’, baada ya mechi na Uganda Septemba 8, mwaka huu mjini Kampala, atawafuata Cape Verde Oktoba 10 kukamilisha mechi zake za mzunguko wa kwanza kufuzu AFCON.
    Na hiyo ni baada ya Taifa Stars kulazimishwa sare ya 1-1 nyumbani na Lesotho Juni 10, mwaka jana Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam ikiwa chini ya kocha mzalendo, Salum Mayanga.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SAMATTA NA ULIMWENGU WAINGIA KAMBINI TAIFA STARS…WA HISPANIA KUWASILI LEO, MSUVA NA HIMID MAO… Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top