• HABARI MPYA

    Sunday, May 13, 2018

    TFF WATUAMBIE KILICHOKWAMISHA LIGI YA VIJANA YA U20 PAMOJA NA AZAM NA KCB KUTOA MAMILIONI YA KUTOSHA

    TIMU ya soka ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro Heroes leo inateremka dimbani Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam kumenyana na Mali katika mchezo wa kwanza wa Raundi ya Pili ya mchujo wa kuwania tiketi ya Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON U20) mwakani nchini Niger.
    Ngorongoro imefika Raundi ya Pili baada ya kuitupa nje Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kwa penalti 6-5 kufuatia sare za 0-0 Dar es Salaam na Kinshasa, wakati Mali imeanzia hatua hii sawa na Angola, Burkina Faso, Cameroon, Kongo, Misri, Gambia, Ghana, Guinea, Ivory Coast, Libya, Nigeria, Senegal, Sudan, Afrika Kusini na Zambia.

    Baada ya mchezo wa kwanza leo, timu hizo zitarudiana Mei 20 mjini Bamako na mshindi wa jumla atakutana na mshindi kati ya Cameroon na Uganda katika hatua ya mwisho ya mchujo wa kuwania tiketi ya Niger 2019. 
    Wakati Ngorongoro hawajawahi kucheza fainali za AFCON U20, Mali ‘The Eagles’, yaani Tai ni wazoefu na wamewahi hadi kushika nafasi ya tatu katika Kombe la Dunia la FIFA la U20 mwaka 1999, baada ya kuifunga Senegal katika mchezo wa kuwania Medali ya Shaba.
    Ngorongoro hii inaundwa na idadi kubwa ya wachezaji waliokuwa kwenye timu ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys ambayo Mei mwaka jana ilishiriki fainali za AFCON U17 nchini Gabon, wakati wachache wamechomoza kwenye timu mbalimbali za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara akiwemo Peter Paul wa Azam FC baada ya kupandishwa kutoka vikosi vya pili. 
    Serengeti Boys iliyofuzu AFCON U17 ya Gabon mwaka jana ilitokana na mpango mzuri wa kuandaliwa tangu vijana wakiwa chini ya umri wa miaka 13, mpango ambao uliendelezwa na ndiyo uliozaa kikosi kingine kizuri cha U17 ya sasa, ambacho mwezi huu kimechukua Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge.
    Haya ni mafanikio ambayo yanaonekana kuanza kuwalevya viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kiasi cha kuanza kupuuza programu za kuendeleza vijana ili kujenga mazingira ya kuwa na timu bora ya taifa ya wakubwa baadaye, itakayowafuta machozi Watanzania.
    Hiyo inatokana na kwamba TFF wameanza kupuuza mashindano ya vijana, kwa mfano msimu huu Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inakaribia kabisa kutia nanga ikiwa katika majuma yake mawili ya mwisho, lakini hayajafanyika mashindano ya vijana chini ya umri wa miaka 20.
    Baada ya misimu kadhaa ya kuwakutanisha vijana wanaounda vikosi vya pili vya timu za Ligi Kuu katika mechi za kirafiki pekee, msimu uliopita TFF chini ya Rais wa wakati huo, Jamal Malinzi ambaye kwa sasa yuko rumande gereza la Keko pamoja na aliyekuwa Katibu wake, Selestine Mwesigwa kwa tuhuma za ubadhirifu ilianzisha mashindano rasmi ya U20.    
    Mashindano yalianzia kwa hatua ya makundi kwenye vituo vya Dar es Salaam na Bukoba vilivyotoa timu nne nne zilizokutana katika hatua ya Nane Bora kwenye makundi mengine mawili Dar es Salaam, baadaye Nusu Fainali na Fainali, Simba B wakiibuka mabingwa kwa ushindi wa penalti 6-5 baada ya sare ya 1-1.
    Katika fainali nzuri iliyofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, mshambuliaji wa Simba, Moses KItandu aliibuka mfungaji bora na mshambuliaji wa Azam FC, Shaaban Iddi Chilunda akawa mchezaji bora.
    Hawa ni wachezaji ambao kwa sasa wanaweza kuunda timu ya vijana chini ya umri wa miaka 23 kwa ajili ya Michezo ya Afrika na Olimpiki.
    Ikumbukwe michuano hiyo, pamoja na Ligi ya Wanawake yote ina udhamini wa Azam TV wa Sh. Milioni 200 kila mwaka kwa miaka mitano, huu ukiwa mwaka wake wa pili. 
    TFF iliahidi msimu huu ingepanua Ligi ya vijana kutoka kuchezwa kwa makundi, hadi kuchezwa sawa na Ligi Kuu kwa mechi za nyumbani na ugenini kwa msimu hadi kupata bingwa.
    Katika mastaajabu ya hali ya juu, Ligi Kuu ipo kwenye wiki zake mbili za mwisho hata ratiba ya Ligi ya U20 haijatoka – maana yake hakuna hata dalili za kufanyika mashindano hayo.
    Hapo hapo, Benki ya KCB Tanzania ikajitokeza kuongeza udhamini wa Sh. Milioni 325 katika Ligi Kuu na TFF ikasema fedha hizo zitaongezwa kwenye Ligi ya vijana – ajabu michuano hiyo haijafanyika na msimu unamalizika. 
    Tunaamini kabisa kikwazo kikubwa cha mambo kufanyika ni fedha – lakini TFF wana fedha wameshindwa kuendesha Ligi ya Vijana. Hii tuiite nini kama si uongozi wa shirikisho chini ya Rais mpya, Wallace Karia kuanza kulewa mafanikio kidogo yaliyopatikana? 
    Ukirudi nyuma namna ya upatikanaji wa timu bora ya Serengeti Boys iliyozaa Ngorongoro Heroes hii nzuri ambayo leo inamenyana na Tai wa Mali ni mashindano ya U13, ambayo mwaka huu hayajafanyika.
    Kwa mtaji huu tusitarajie tena matokeo mazuri kwenye timu za vijana kuanzia mwakani ikiwa misingi ya uundwaji wa timu imezikwa na viongozi waliolewa sifa baada ya mafanikio kidogo. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TFF WATUAMBIE KILICHOKWAMISHA LIGI YA VIJANA YA U20 PAMOJA NA AZAM NA KCB KUTOA MAMILIONI YA KUTOSHA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top