• HABARI MPYA

    Monday, May 12, 2014

    MWAMBUSI AWACHIMBA MKWARA WANAOTAKA KUHAMIA SIMBA NA YANGA, AWAAMBIA; “HUKO MNAFUATA KIFO CHA SOKA YENU”

    Na Renatus Mahima, Dar es Salaam
    HUKU kukiwa kuna habari kwamba, Saad Kipanga wa Mbeya City yuko njiani kuhamia Simba SC, kocha wa timu hiyo ya mkoa huo wa Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania, Juma Mwambusi ametoa onyo kali kwa mchezaji huyo na wengine wa MCC FC.
    Mwambusi amewaambia wachezaji wake wanaotaka kukimbilia ofa nzuri za maslahi za klabu kongwe nchini za Simba na Yanga kwamba wakienda huko wataweka rehani vipaji vyao.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY mjini Dar es Salaam jana, Mwambusi alisema wachezaji wake wengi bado hawajakomaa kisoka hivyo hawapaswi kukimbilia Simba na Yanga ambako "viongozi na mashabiki wake hawana uvumilivu".
    Saad Kipanga kulia inadaiwa yuko njiani kuhamia Simba SC

    "Ninatambua baadhi ya wachezaji wangu wanawindwa kwa udi na uvumba na klabu za Dar es Salaam hasa Simba na Yanga lakini sidhani kama ni wakati mwafaka mchezaji wa Mbeya City kujiunga na Simba au Yanga kwa sasa."
    Mwambusi ambaye ana asilimia kubwa ya kutwaa tuzo ya kocha bora msimu huu, alisema si wakati mwafaka kwa wachezaji wa City kujiunga na Simba au Yanga kwa sasa kwa sababu:
    "Alisimia kubwa ya wachezaji wa Mbeya City bado ni wachanga na hawana uzoefu."
    "Sisi hatuwazuii kuondoka lakini hizo shilingi milioni 30 wanazoambiwa watapewa zitaua soka lao kwa sababu hizi klabu mbili hazina uvumilivu.
    "Ninafikiri wanapaswa kubaki Mbeya City ili tuwapike vizuri zaidi kabla ya kujiunga na timu hizo. Yawezekana Mbeya City isiwe na uwezo wa kuwapa hizo shilingi milioni 30 lakini kuna faida kubwa ya kuwa na subira Mbeya City kuliko kuharakia maisha ya soka upate pesa."
    Ikiwa na kikosi chenye wachezaji wawili tu wenye uzoefu wa ligi kuu -- kipa David Burhan aliyenyakua tuzo ya kipa bora msimu wa 2012/13 akiwa na kikosi cha Tanzania Prisons na straika Paul Nonga aliyekuwa na Oljoro JKT msimu wa 2012/13 -- Mbeya City imeshika nafasi ya tatu kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu huu.
    Wachezaji wengi wa timu hiyo inayomilikiwa na Halmashauri ya Jiji la Mbeya wameng'ara kiasi cha kuwashawishi vigogo wa soka Simba na Yanga pamoja na mabingwa wapya Azam FC kuwania saini zao.
    Simba inataka kuwachukua mshambuliaji Saad Kipanga aliyejiunga na Mbeya City mzunguko wa pili akitokea Rhino Rangers na kiungo fundi Deus Kaseke.
    Kocha wa Azam FC, Mcameroon Joseph Omog anataka kiungo na mshambuliaji kutoka timu hiyo ambao hata hivyo uongozi wa timu hiyo hauko tayari kuweka wazi majina yao.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MWAMBUSI AWACHIMBA MKWARA WANAOTAKA KUHAMIA SIMBA NA YANGA, AWAAMBIA; “HUKO MNAFUATA KIFO CHA SOKA YENU” Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top