Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
BARAZA la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limesogeza mbele kwa siku mbili michuano yake mipya ijulikanayo kama Nile Basin na sasa itaanza kesho wakati wawakilishi wa Tanzania, Mbeya City wataondoka usiku wa leo kwenda Sudan.
Taarifa ya CECAFA iliyotumwa BIN ZUBEIRY leo imesema kwamba timu zote za Misri zilizotarajiwa kushirki michuano hiyo hazitakuja tena na baadhi ya timu zilizowekwa kwenye ratiba awali zimejitoa na nafasi yake kupewa timu nyingine.
Sasa michuano hiyo inayoshirikisha mabingwa wa Kombe la Fa na washindi wa pili wa Ligi Kuu za nchi wanachama wa CECAFA makundi yake matatu yamepangwa upya pamoja na ratiba nzima.
Kundi A sasa litakuwa na timu za El Merreikh ya Sudan, Victory University ya Uganda, Malakia ya Sudan Kusini na Polisi ya Zanzibar, Kundi B kuna Mbeya City ya Tanzania Bara, AFC Leopars ya Kenya, Academie Tchite ya Burundi na Entincelles ya Rwanda, wakati Kundi C kuna Al Shandy ya Sudan, Defence ya Ethiopia na Dkhil ya Djibouti.
Awali michuano hiyo ilitarajiwa kushirikisha timu za Misri pia, Al Masry, Hey Al Arab, Arab Contractors, zilizoalikwa kunogesha mashindano hayo, lakini zikajitoa dakika za mwishoni.
Kwa ujumla, awali timu zilizotarajiwa kushiriki mashindano hayo ni Al Ahly Shandy, Al Masry ya Misri, Defence na Dhikil zilizopangwa Kundi C, wakati Kundi D lilikuwa na Hey Al Arab, Arab Contractors, Flam beaude L'EsT ya Burundi na Etincelles ya jijini Kigali, Rwanda.
Mbeya City imeendelea kubaki Kundi B kama ilivyo AFC Leopard ya Kenya, lakini El Mereikh Al Fashery na Elman ya Somalia zimeondoka na nafasi yake imechukuliwa na Enticelles na Academie Tchite.
Mbeya City sasa itatupa karata yake ya kwanza Jumamosi mbele ya Academie Tchite ya Burundi Uwanja wa Merreikh kuanzia Saa 11:30 jioni na kufuatiwa na mchezo kati ya AFC Leopards ya Kenya na Enticelles ya Rwanda Saa 2:00 usiku, hizo zikiwa mechi za Kundi B.
Mechi tatu za Ufunguzi zinatarajiwa kuchezwa kesho, kati ya Victoria Univesrity ya Uganda na Malakia ya Sudan Kusini, wenyeji Al-Merreikh ya Polisi ya Zanzibar zote zikiwa za Kundi A na wenyeji wengine Al-Shandy dhidi ya Dkhill ya Djibouti, huo ukiwa mcheo wa Kundi C.
Katibu Mkuu wa Mbeya City, Emmanuel Kimbe, ameithibitishia BIN ZUBEIRY kupatiwa tiketi na leo usiku wanapanda ndege kwenda Sudan.
0 comments:
Post a Comment