• HABARI MPYA

    Thursday, May 22, 2014

    WAMBURA KIKAANGONI UCHAGUZI SIMBA SC, HUENDA AKAENGULIWA

    Na Renatus Mahima, Dar es Salaam
    HATMA ya wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi wa Simba wenye dosari akiwamo Michael Wambura anayeutaka Urais wa klabu hiyo itajulikana katika usaili wa wagombea jijini Dar es Salaam Mei 27, imefahamika.
    Jumatatu Kamati ya Uchaguzi ya Simba chini ya Mwenyekiti Damas Ndumbaro ilipitisha majina yote 41 ya wanachama wa Simba waliojitosa kuwania uongozi katika uchaguzi mkuu wa klabu hiyo uliopangwa kufanyika Juni 29 mwaka huu baada ya wanachama hao kuzijaza kikamilifu fomu za kuwania uongozi.
    Hatihati; Michael Wambura huenda akaenguliwa kugombea uongozi wa Simba SC kwa kukiuka Katiba

    Akizungumza na BIN ZUBEIRY akiwa Songea jana mchana, Ndumbaro amesema kamati yake haitakuwa na upendeleo na mgombea yeyote na itaanza kukunjua makucha yake Mei 27 wakati wa zoezi la usaili wa wagombea.
    Lakini, kwa mujibu wa ratiba ya mchakato wa uchaguzi huo, matokeo ya usaili wa wagombea watakaokuwa wamepita kwenye zoezi la pingamizi, yatatangazwa Mei 29.
    "Tumepitisha majina yote bila kuzingatia makosa ya nyuma ya wagombea kwa sababu tulichokizingatia ni ujazaji halali wa fomu za uchaguzi kwa kusaini, kuweka picha, kadi ya uachama wa Simba na vyeti vinavyotakiwa. Vyegti vyote vya elimu tumepeleka NECTA (Baraza la Mitahani la Taifa) ili vihakikiwe," amesema Ndumbaro.
    "Tutaanza kuwashughulikia wagombea wenye matatizo Mei 27 wakati wa usaili. Kwa kuwa usaili ni mtihani wa kamati kwa wagombea, vigezo vyote vinavyotumika siwezi kuvianika kwa chombo cha habari maana ni siri ya kamati.
    "Mei 22 (kesho saa 10:00 alasiri) ni siku ya mwisho ya kupokea pingamizi na Mei 25 (Jumapili) tutasikiliza pingamizi. Kamati haitamuonea wala kumpendelea mgombea. Uchaguzi wa Simba unaendeshwa kwa misingi ya Kanuni na Katiba ya klabu na TFF," amesema zaidi mwanasheria huyo.
    Wambura amekuwa akikumbana na vigingi katika chaguzi mbalimbali za soka anazojitosa kuwania uongozi baada ya kuupeleka mahakamani uongozi wa Klabu ya Simba uliokuwa madarakani mwaka 2010 akisimamisha uchaguzi na kupinga kuondolewa katika mchakato huo.
    Katibu mkuu huyo wa kilichokuwa Chama cha Soka Tanzania (FAT sasa TFF), alifungua kesi akiushitaki uongozi wa mwenyekiti, Hassan Dalali, kwenye Mahakama ya Ilala jijini Dar es Salaam na baadaye kesi hiyo ilitupiliwa mbali na Simba ikafanya uchaguzi wake.
    Ibara ya 11(2)(b) cha Katiba ya Simba kinakataza mwanachama kutopeleka masuala ya mpira wa miguu katika mahakama ya kawaida ya sheria.
    Ibara ya 12(3) cha Katiba ya klabu hiyo pia kinasema: “Mwanachama au mtu yoyote (mchezaji au kiongozi) atakayetafuta msaada katika mahakama ya kawaida ya kisheria kuhusu mgogoro unaohusiana na katiba, kanuni maagizo ya maamuzi ya Simba Sports Club atasimamishwa mara moja na Kamati ya Utendaji."
    Pamoja na msamaha uliotolewa jijini Dar es Salaam usiku wa kuamkia Oktoba 28 mwaka jana na Rais wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Jamal Malinzi kwa watu wote wa mpira nchini isipokuwa kwa wenye makosa ya klabu kama la Wambura, Katiba ya TFF pia inakataza wanachama TFF kupeleka masuala ya soka katika mahakama za kiraia.
    Kwa tafsiri isiyo rasmi, Ibara ya 12(e) cha Katiba ya shirikisho hilo lenye mamlaka ya juu kisoka nchini kinasema: "Kuhusisha mahakama za kiraia kwenye masuala ya soka hakuruhusiwi. Mwanachama yeyote anayekiuka utaratibu huu aidha kwa matakwa yake mwenyewe au kwa faida ya mtu mwingine, atafungiwa kujihusisha na shughuli za mpira wa miguu." 
    Mbali na Wambura, wagombea wengine walio katika hatari ya kuenguliwa ni wanaotoka kwenye Kamati ya Utendaji ya Simba inayomaliza muda wake baada ya kufanya mkutano na kumpindua Mwenyekiti (Rais) Ismail Aden Rage kinyume cha Katiba ya Simba na Shirikisho la Soka nchini (TFF).
    Baadhi ya wanachama hao wa Simba ni wagombea wa nafasi ya Makamu wa Rais Joseph Itang’are 'Kinesi' aliyekuwa mwenyekiti wa mkutano wa kusimamisha Rage na Swedi Nkwabi aliyepachikwa cheo cha Makamu Mwenyekiti baada ya mapinduzi na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Ibrahim Masoud 'Maestro' anayewania pia nafasi hiyo.
    Aidha, Kamati ya Utendaji ya Simba chini ya Rage imekiuka Katiba ya klabu hiyo kwa kutoitisha mkutano mkuu wa dharura wa uchaguzi wa Makamu Mwenyekiti siku 90 baada ya kujiuzulu kwa Kaburu.
    Ndumbaro amesema zoezi la kupitia pingamizi za wagombea litafanyika Mei 25 na 26, kwenye Ukumbi wa Gymkhana Club jijini na watakaoruhusiwa kuingia ni wale walioweka pingamizi na wagombea waliowekewa pingamizi na maamuzi ya pingamizi hizo yatatangazwa Mei 27, mwaka huu.
    Hadi jana mchana hakuna pingamizi yoyote iliyokuwa imefika mbele ya Kamati ya Uchaguzi ya Simba, kwa mujibu wa katibu msaidizi wa kamati hiyo Halid Kamguna.
    "Mpaka sasa (jana saa 7:53 mchana) hatujapokea pingamizi yoyote zaidi ya watu kuja na kutamka maneno tu kwamba wanaleta pingamizi. Pingamizi ni suala nyeti na linahitaji uwe na vithibitisho vya uhakika," amesema Kamguna huku akieleza kuwa hakuna ada kwa ajili ya pingamizi.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: WAMBURA KIKAANGONI UCHAGUZI SIMBA SC, HUENDA AKAENGULIWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top