Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Deo Lyatto na Makamu wake, Hamidu Mbwezeleni kulia. Kushoto ni Katibu wa TFF, Angetile Osiah |
Na Boniface Wambura
KAMATI ya
Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imeahirisha uchaguzi wa Chama cha
Makocha wa Mpira wa Miguu Tanzania (TAFCA) uliokuwa ufanyike leo (Januari 19
mwaka huu) jijini Dar es Salaam.
Uchaguzi
umeahirishwa kwa vile ulitaka kufanyika bila kuzingatia Katiba ya TAFCA Ibara
ya 32(1) na Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF Ibara ya 10(6) na 26(2),
hivyo Kamati ya Uchaguzi ya TFF imeahirisha uchaguzi huo kwa vile nafasi
zilizoombwa kugombewa na idadi ya waombaji uongozi haikidhi matakwa ya Katiba
ya TAFCA.
Pia taratibu
za kikanuni ikiwa ni pamoja na kuwaarifu waombaji uongozi ambao hawakukidhi
matakwa ya Katiba ya TAFCA hazikukamilika kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za
Wanachama wa TFF.
Licha ya
upungufu huo, TAFCA haikuwasilisha taarifa za mchakato mzima kama ilivyoombwa
na TFF. Kamati ya Uchaguzi ya TFF imeiagiza Kamati ya Uchaguzi ya TAFCA kuandaa
uchaguzi mpya utakaokidhi matakwa ya Kamati ya TAFCA baada ya Uchaguzi Mkuu wa
TFF.
TFF
inaishauri TAFCA kutumia fursa ya Mkutano Mkuu wa leo (Januari 19 mwaka huu)
kujadili mustakabali wa TAFCA kwa kuwa chama hicho kimeshindwa mara mbili
kupata idadi ya wagombea wanaokidhi akidi ya Kamati ya Utendaji.
Pia TAFCA
haijawahi kufanya mikutano ya Kamati ya Utendaji na Mkutano Mkuu kwa karibu
miaka minne.