• HABARI MPYA

    Monday, January 21, 2013

    RAIS ZFA ATAKA KUJIUZULU KUKWEPA WAPINGA MAENDELEO

    Aman Ibrahim Makungu, rais wa ZFA aliyebeba matumaini ya soka ya Zanzibar 

    Na Ally Mohammed, Zanzibar
    RAIS wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), Aman Ibrahim Makungu, ameandika barua ya kutaka kujiuzulu nafasi yake kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kuchoshwa na vitendo vya baadhi ya viongozi wa juu wa chama hicho cha kukataa mabadiliko chanya.
    Taarifa zilizopatikana kutoka katika chanzo cha kuaminika, ni kuwa barua ya Rais wa Zfa Taifa iliyoandikwa kwenda kwa Katibu Mkuu wa Zfa Taifa, Kassim Haji Salum, ambayo imesainiwa na yeye mwenyewe imesema kuwa amechoshwa na tabia ya baadhi ya viongozi wa juu wa Chama hicho cha kukataa kumpa ushirikiano, huku lawama nyingi akizielekeza kwa Katibu wake Mkuu na Makano wa Rais kisiwani Pemba akiwataja kuwa ndio chanzo cha kukosekana ushirikiano katika chama hicho.
    Hata hivyo barua hiyo inatarajiwa kukabidhiwa rasmi keshokutwa mara baada ya kumalizika kwa ziara rasmi ya Zfa katika wilaya nne za Pemba, ziara ambayo inamalizika kesho katika wilaya ya Chake Chake.
    Hatua hiyo imekuja kufuatia ziara rasmi ya Viongozi wa ngazi za juu wa Zfa Taifa wakiongozwa na Rais mwenyewe Aman Makungu, kwenda kisiwani Pemba kwa lengo la kuzungumza na viongozi wa soka katika wilaya zote za Pemba na ziara hiyo kudaiwa kususiwa na viongozi wa juu wa Zfa kisiwani Pemba akiwemo Makamo wa Rais kisiwani Pemba pamoja na Msaidizi katibu wa Zfa kisiwani Pemba.
    Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na hali ya kutokuelewana kwa viongozi wa juu wa Zfa kati ya Unguja na Pemba huku kila upande ukiwa na sababu zake, wakati uongozi wa Zfa kisiwani Unguja ukilezea tabia ya viongozi wa Kisiwani Pemba kufanya mambo kienyeji, Uongozi wa Zfa kisiwani Pemba umekuwa ukilalamika juu ya maamuzi makubwa yanayofanywa na chama hicho bila ya kuwashirikisha huku wakitolea mfano wa suala la kufungiwa kwa wachezaji wa Timu ya Taifa ya Zanzibar 'Zanzibar Heroes'.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: RAIS ZFA ATAKA KUJIUZULU KUKWEPA WAPINGA MAENDELEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top