TIMU ya Tanzania Prisons imeibuka na ushindi wa ugenini wa mabao 3-2 dhidi ya wenyeji, Pamba Jiji FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza.
Mabao ya Tanzania Prisons yamefungwa na winga Haroun Athumani Chanongo dakika ya 45’+1 na washambuliaji George Enock Mpole Mwaigomole dakika ya 78 kwa penalti na Oscar Paul Mwajanga dakika ya 90’+4.
Kwa upande wao wenyeji, Pamba Jiji FC mabao yote yamefungwa na mshambuliaji wa Kimataifa wa Kenya, Mathew Tegisi Momanyi dakika ya 68 na 72.
Kwa ushindi huo, Tanzania Prisons inafikisha pointi 20, ingawa inabaki nafasi ya 15 kwenye ligi ya timu 16 mbele ya KMC FC yenye pointi tisa baada ya timu zote hizo kucheza mechi 25.
Kwa upande wa Pamba Jiji FC baada ya kupoteza mchezo huo wa nyumbani wanabaki na pointi zao 33 nafasi ya saba sawa na Dodoma Jiji FC hata kwa wastani wa mabao.
Ikumbukwe mwisho wa msimu timu mbili zitashuka Daraja moja kwa moja, wakati nyingine mbili zitakazomaliza nafasi ya 14 na 13 zitamenyana baina yao kwa mechi mbili za nyumbani na ugenini na mshindi wa jumla atasalia Ligi Kuu.
Timu itakayofungwa itakwenda kumenyana na timu kutoka Ligi ya Championship katika mechi nyingine mbili za mchujo nyumbani na ugenini na mshindi wa jumla ndiye atacheza Ligi Kuu msimu ujao.



.png)
0 comments:
Post a Comment