• HABARI MPYA

    Sunday, May 13, 2018

    KILA LA HERI NGORONGORO HEROES, WAPIGENI MALI MABAO YA KUTOSHA MRAHISISHE SHUGHULI MECHI YA MARUDIANO KWAO

    Na Rehema Lucas, DAR ES SALAAM
    TIMU ya soka ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro Heroes leo inateremka dimbani Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam kumenyana na Mali katika mchezo wa kwanza wa Raundi ya Pili ya mchujo wa kuwania tiketi ya Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON U20) mwakani nchini Niger.
    Ngorongoro imefika Raundi ya Pili baada ya kuitupa nje Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kwa penalti 6-5 kufuatia sare za 0-0 Dar es Salaam na Kinshasa, wakati Mali imeanzia hatua hii sawa na Angola, Burkina Faso, Cameroon, Kongo, Misri, Gambia, Ghana, Guinea, Ivory Coast, Libya, Nigeria, Senegal, Sudan, Afrika Kusini na Zambia.

    Mechi hiyo itachezeshwa na marefa kutoka Comoro, Soulaimane Ansudane atakayepuliza kipyenga akisaidiwa na washika vibendera Mmadi Faissoil na Abdoulmadjid Azilani na viingilio katika mchezo huo vitakuwa Sh. 3,000 kwa VIP zote na Sh. 1, 000 kwa mzunguko wote.
    Wakati Ngorongoro hawajawahi kucheza fainali za AFCON U20, mafanikio makubwa ya Mali ni kushika nafasi  ya tatu katika Kombe la Dunia la FIFA la U20 mwaka 1999, baada ya kuifunga Senegal katika mchezo wa kuwania Medali ya Shaba.
    Baada ya mchezo wa kwanza leo, timu hizo zitarudiana Mei 20 mjini Bamako na mshindi wa jumla atakutana na mshindi kati ya Cameroon na Uganda katika hatua ya mwisho ya mchujo wa kuwania tiketi ya Niger 2019. 
    Kila la heri Ngorongoro Heroes. Mungu ibariki Tanzania. Ibariki Ngorongoro Heroes. Amin.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KILA LA HERI NGORONGORO HEROES, WAPIGENI MALI MABAO YA KUTOSHA MRAHISISHE SHUGHULI MECHI YA MARUDIANO KWAO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top