Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
BONDIA Francis Miyeyusho ameendeleza ubabe dhidi ya ukoo wa
Matumla, baada ya usiku huu kumshinda kwa pointi Mohamed Matumla katika pambano
lisilo la ubingwa uzito wa Bantam, ukumbi wa PTA, Temeke, Dar es Salaam.
Mtoto wa Rashid Matumla alimaliza raundi 10 za pambano na majaji
wote watatu wakampa ushindi wa pointi Chichi Mawe- ambao alistahili.
Pamoja na kushinda, Miyeyusho alikutana na mpinzani mkali ulingoni
ambaye alisimama naye wakijibizana makonde mwanzo hadi mwisho.
Chichi alianza vizuri pambano hilo akimkalisha chini mpinzani wake
raundi ya kwanza tu, baada ya kumpa ngumi ya kidevu ya kushitukiza.
![]() |
| Miyeyusho akibwa amebebwa na shabiki wake kushangilia ushindi baada ya pambano |
Hata hivyo, Matumla aliinuka na kumalizia vizuri raundi hiyo,
kisha kuibuka upya katika raundi ya pili na kuendelea vizuri hadi mwisho.
Miyeyusho alipiga ngumi nyingi zaidi ya mtoto wa Matumla,
aliyeongozwa na baba yake ulingoni lakini mabondia wote walichapana makonde ya
nguvu na kila mmoja kuna wakati alionekana kulewa.
Pambano hilo lilitawaliwa na vurugu za mashabiki wa mabondia hao
kutokana na upinzani wa asili- Matumla akikusanya watu wa Keko na Temeke kwa
ujumla na Miyeyusho akikusanya watu wa Kinondoni na Manzese.
Miyeyusho alipanda ulingoni leo kiasi cha wiki tatu tangu apigwe
vibaya na Sukkassem Kietyongyuth wa Thailand Aprili 19 kwenye ukumbi huo huo
kwa Technical Knockout (TKO) raundi ya
kwanza sekunde ya 55.
![]() |
| Miyeyusho akipigana na Matumla mdogo usiku huu PTA |
Awali, Miyeyusho alimpiga baba yake mdogo Matumla, Mbwana Matumla
Oktoba 30, mwaka 2011 na leo ameendeleza ubabe dhidi ya ukoo huo maarufu katika
mchezo wa ngumi.
Hilo lilikuwa pambano la 51 kwa Miyeyusho tangu aanze kupigana
kifua wazi Februari 1, mwaka 1998 akiwa ameshinda mapambano 38, kati ya hayo 23
kwa KO na kupigwa 11, kati ya hayo 10 kwa KO na sare mawili. Mtoto wa Rashid Matumla ambaye ngumi katika ukoo wao zinaanzia kwa
babu yake Mzee Ally Matumla, leo amepigwa kwa mara ya kwanza katika pambano la
15 tangu ajitose kwenye ngumi za kulipwa Novemba 17, mwaka 2010 akiwa ameshinda
mapambano 11, manne kwa KO na ametoka sare mara tatu.




.png)
0 comments:
Post a Comment