MABINGWA watetezi, Yanga SC wamerejea kileleni mwa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara kufuatia ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Namungo FC usiku huu Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam.
Pongezi kwa kiungo wa Kimataifa wa Uganda, Allan Jolly Okello ‘Star Boy’ aliyefunga mabao mawili dakika ya 53 na 84 kufuatia kiungo wa Kimataifa wa Kenya, Duke Ooga Abuya kufunga la kwanza dakika ya 26 – huku bao la Namungo FC likifungwa winga mzawa, Hassan Salum Kabunda dakika ya 39.
Kwa ushindi huo, Yanga SC inafikisha pointi 60 na kurejea kileleni mwa Ligi Kuu ikiwazidi pointi mbili watani wao, Simbna SC baada ya timu zote kucheza mechi 25 sasa.
Kwa upande wao Namungo FC baada ya kupoteza mchezo wa leo wanabaki na pointi zao 25 baada ya kucheza mechi 25 kadhalika wakiwa katika nafasi ya 13 kwenye ligi ya timu 16.
Ikumbukwe mwisho wa msimu timu mbili zitashuka Daraja moja kwa moja, wakati nyingine mbili zitakazomaliza nafasi ya 14 na 13 zitamenyana baina yao kwa mechi mbili za nyumbani na ugenini na mshindi wa jumla atasalia Ligi Kuu.
Timu itakayofungwa itakwenda kumenyana na timu kutoka Ligi ya Championship katika mechi nyingine mbili za mchujo nyumbani na ugenini na mshindi wa jumla ndiye atacheza Ligi Kuu msimu ujao.



.png)
0 comments:
Post a Comment