TIMU ya Azam FC imeibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya KMC katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara usiku huu Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Ilikuwa siku nyingine nzuri kwa nyota wa timu hiyo, kiungo mshambuliaji wa Kimataifa wa Tanzania, Feisal Salum Abdallah aliyefunga mabao mawili dakika ya tatu na 16, huku bao lingine likifungwa na beki wa kati wa Kimataifa wa Mali, Yoro Mamadou Diaby dakika ya 34.
Kwa ushindi huo, Azam FC inafikisha pointi 52, ingawa inabaki nafasi ya tatu nyuma ya mabingwa watetezi, Yanga SC wanaoongoza kwa pointi zao 60 wakifuatiwa na vigogo wenzao, Simba SC wenye pointi 58 baada ya timu hizo zote tatu kucheza mechi 25.
Hali inazidi kuwa mbaya kabisa kwa KMC kufuatia kupoteza mchezo huo, wakibaki na pointi zao tisa baada ya kucheza mechi 25 pia hivyo kuendelea kushika mkia kwenye Ligi Kuu inayoshirikisha timu 16.
Ikumbukwe mwisho wa msimu timu mbili zitashuka Daraja moja kwa moja, wakati nyingine mbili zitakazomaliza nafasi ya 14 na 13 zitamenyana baina yao kwa mechi mbili za nyumbani na ugenini na mshindi wa jumla atasalia Ligi Kuu.
Timu itakayofungwa itakwenda kumenyana na timu kutoka Ligi ya Championship katika mechi nyingine mbili za mchujo nyumbani na ugenini na mshindi wa jumla ndiye atacheza Ligi Kuu msimu ujao.



.png)
0 comments:
Post a Comment