• HABARI MPYA

    Sunday, May 06, 2018

    YANGA INAHITAJI VIONGOZI WAPYA KABISA ILI KUFUFUA MATUMAINI, VINGINEVYO…

    KWA mara nyingine tena wiki hii wachezaji wa Yanga SC waligoma kusafiri kwenda Algeria na kikosi cha timu hiyo kilichokwenda kumenyana na wenyeji, U.S.M. Alger katika mchezo wa ufunguzi wa Kundi D michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
    Yanga SC watakuwa wenyeji wa U.S.M. Alger leo mjini Algiers katika mchezo wa Kundi D Kombe la Shirikisho Afrika wakiianza hatua ya makundi ya ugenini. 
    Na wakati wa safari wa Algiers Alhamisi mjini Dar es Salaam wachezaji waligoma kwenda Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) hadi kwanza wapatiwe fedha zao za malimbikizo ya mishahara kwa miezi mitatu iliyopita.
    Uongozi uliwabembeleza na baadhi yao wakakubali kwenda JNIA na kupanda Ndege ya Emirates Air kupitia Dubai kwenda Algiers, lakini wengine wakiwemo beki Kelvin Yondan, kiungo Mkongo Papy Kabamba Tshishimbi na washambuliaji Mzambia Obrey Chirwa na Ibrahim hawajasafiri.
    Lakini uongozi umelipoza suala la wanne hao waandamizi kutosafiri kwa kusema kwamba wana udhuru wa sababu mbalimbali na si kweli wamegoma.
    Mgomo huu unakuja siku chache baada ya timu kufungwa 1-0 na mahasimu wa jadi, Simba katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika siku ambayo timu ilicheza kwa kiwango cha chini mno.
    Yanga iliingia uwanjani siku hiyo kujizuia kufungwa na Simba na si kutafuta kushinda mchezo na haikuwa ajabu wakashindwa kupata hata kona moja ndani ya dakika 90 wakichapwa bao moja na kukoswa mengine yasiyopungua matatu ya wazi.
    Haijawahi kutokea Yanga dhaifu mbele ya Yanga kwa miaka ya karibuni kuliko ile ya Jumapili iliyopita na kwa bahati waliyonayo wakafungwa 1-0 tu.
    Tayari Yanga wanajua wamekwishavuliwa ubingwa wa Ligi Kuu na kwa kuwa walitolewa mapema katika Robo Fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) mwakani hawatacheza michuano ya Afrika.
    Tutarajie Yanga kurudi kwenye michuano ya Afrika mwaka 2020 kama watafanya vizuri msimu ujao katika michuano ya nyumbani, kama si Ligi Kuu basi Kombe la TFF.
    Lakini kwa hali halisi ndani ya klabu huwezi kuona ni namna Yanga itaibuka hata mwaka 2010 ipate tena tiketi ya kucheza michuano ya Afrika.
    Azam FC baada ya msimu mbaya wanaanza kujiumba upya, Singida United wanazidi kujijenga kuwa timu ya ushindani, Mtibwa Sugar wamedhamiria kurejea kwenye enzi zao na Simba SC ndiyo hao sasa wamerejea katika ubora wao – Yanga itatokea wapi? 
    Hizo ni tafakuri tu. Tafakuri ambazo zinatokana na hali halisi ndani ya klabu ya Yanga. Baada ya miaka 11 ya ufahari chini chini ya ufadhili wa mfanyabiashara mwenye asili ya Kiasia, Yussfu Manji hatimaye Yanga iliingia kwenye wakati mgumu Mei mwaka jana baada ya bilionea huyo kijiuzulu.
    Manji aliingia Yanga mwaka 2006 kama mdhamini kupitia kampuni yake ya Lotto Kitita, lakini baadaye akawa mfadhili Mkuu wa klabu kabla ya kuwa Mwenyekiti.
    Katika kipindi chake cha kuwa mfadhili na Mwenyekiti wa Yanga, Manji aliifanyia mengi klabu– kubwa ni kuirejeshea hadhi na heshima klabu hiyo.
    Alipoingia mwaka 2006 aliikuta klabu ipo dhoofu kiuchumi na haiwezi kushindana na mahasimu wao, Simba katika kuwania wachezaji bora ambao ndiyo mtaji wa kushinda mataji.
    Wakati huo Yanga ilikuwa inasajili wachezaji ambao ama walikuwa wameachwa na timu zao, waliojipeleka wenyewe kwa mapenzi yao au waliopatikana kwa njia ya mchujo wa majaribio.
    Lakini mara baada ya Manji kuingia Yanga, klabu hiyo ikaanza kusifika kwa kusajili wachezaji wa kigeni na wale nyota wa hapa nyumbani, ikiwa ni pamoja na kubomoa ngome ya mahasimu, Simba SC.
    Mwaka 2009 fedha za Manji zilimtoa kipa kipenzi cha wana Simba Msimbazi, Juma Kaseja na desturi hiyo ikaendelea baadaye wakichukuliwa beki Kelvin Yondan na mshambuliaji Mganda Emmanuel Okwi.
    Yanga iliipiku Simba ‘kimafia’ katika kumsajili beki anayeweza kucheza kama kiungo pia, Mbuyu Twite kutoka APR ya Rwanda, tu kwa jeuri ya fedha.
    Aliyekuwa Mwenyekiti wa Simba, Alhaj Ismail Aden Rage alianza kuonekana akimsainisha Mbuyu mjini Kigali, lakini baadaye Mwenyekiti wa Usajili wa timu ya Jangwani, Abdallah Bin Kleb akaingia kwa ‘gia kubwa’ na kubadilisha mambo, Mbuyu akatua Jangwani.
    Na ni katika kipindi hicho imeshuhudiwa Manji amewazima kabisa Simba na Yanga ikitawala soka ya Tanzania na kuzidi kujiongezea mashabiki na wapenzi.
    Lakini migogoro haikukosekana pia wakati wa utawala wa Manji, ambayo wakati fulani iliiathiri timu mfano ule wa kutaka kumng’oa aliyekuwa Mwenyekiti, Wakili Lloyd Nchunga ulioiponza klabu ifungwe 5-0 na mahasimu, Simba Mei 6, mwaka 2012.
    Mapema mwaka jana, Manji alikuja na mpango wa kutaka kujikodisha klabu kupitia kampuni aliyoisajili kwa jina la Yanga Yetu, lakini ukapata upinzani mkali na kuamua kuachana nao.  
    Kabla ya kufikia maamuzi haya, Manji alipitia kwenye misukosuko na Serikali kuanzia Januari hadi Aprili, kwanza akikamatwa na kuwekwa ndani kwa tuhuma za kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya na baadaye akidaiwa kumiliki pasipoti mbili.
    Hali hiyo ilisababisha ashindwe kutekeleza majukumu yake ya kiufadhili Yanga na kufanya wachezaji wakose mishahara kwa kipindi chote hicho kabla ya viongozi wenzake kuanza kufanya jitihada za kulipa taratibu.
    Kwa kipindi kirefu chza ufadhili na utawala wa Manji, Yanga ilikuwa pia ikidhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia yake ya Kilimanjaro Premium Lager – lakini akapishana siku chache tu na kampuni hiyo kujitoa Jangwani.
    Bahati nzuri ikatokea kampuni ya SportPesa kuziba pengo la TBL Yanga ambyo pia inaidhamini na Simba kama ilivyokuwa Kilimanjaro Premium Lager na baadaye zikaja kampuni za Macron, Maji ya Afya na inafahamika pia klabu inapata fedha kutoka Azam TV, lakini bado kwa kipindi chote tangu Mei mwaka jana hali bado ngumu Yanga.
    Na ilipofikia hali hiyo haimuogopeshi yeyote kati ya viongozi waliopo madarakani Yanga, si wa kuchaguliwa, kuteuliwa wala kuajiriwa – wote wanaonekana kuizoea na kuikubali.
    Yanga sasa imekuwa ya ‘kuunga unga’, inavyokwenda wala huwezi kuamini, lakini inakwenda na hadi sasa inashika nafasi ya tatu kwenye Ligi Kuu nyuma ya Simba na Azam na ipo hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho.
    Pamoja na matatizo ya kiuchumi, lakini viongozi wa Yanga na Kamati zake wanaonekana kukosa hata ya maarifa ya kawaida ya kufanya baadhi ya mambo, kama usajili wa wachezaji wa kiwango cha kuisaidia timu na hata kuunda timu kwa bajeti inayoendana na uwezo wa klabu.
    Makosa yaliyofanyika mwazoni mwa msimu kuwapa mikataba mipya minono wachezaji majeruhi yakaongezewa na makosa ya kutosajili mshambuliaji mbadala wao dirisha dogo na pia wakasajili beki Mkongo, Fiston 'Festo' Kayembe Kanku ambaye hajaonekana tena.
    Matunzo na malezi ya wachezaji waliopo si mazuri kiasi kwamba wachezaji wanafikia kugoma mara kwa mara kwa sababu ya kucheleweshewa mishahara. Yanga imekuwa timu ya ovyo sana inayowachoma mioyo mashabiki wake kila siku na bahati mbaya viongozi waliopo wanajioa sawa tu.
    Wakati umefika Yanga inahitaji uongozi mpya kuanzia wa Kamati ya Utendaji, Sekretarieti na Kamati Teule pia zikiwemo za Usajili na Mashindano. Hawa waliopo uwezo wao umefikia hapa. Na wamejitahidi kwa sababu mtu ni uwezo na kwa uwezo wao walipoifikisha klabu wanastahili sifa.
    Lakini sasa Yanga inahitaji viongozi wapya watakaokerwa na hali iliyopo klabuni na watapambana kuleta mageuzi kwa hali yoyote. Hao watu wapo na njia rahisi ya kuwapata ni kuitisha uchaguzi wenye mapenzi na uchungu na klabu wachukue fomu kuja kuinusuru klabu yao.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA INAHITAJI VIONGOZI WAPYA KABISA ILI KUFUFUA MATUMAINI, VINGINEVYO… Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top