• HABARI MPYA

  Sunday, May 20, 2018

  KILA LA HERI NGORONGORO HEROES MJINI BAMAKO LEO MECHI NA MALI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  TIMU ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro Heroes leo inateremka Uwanja wa Omnisports Modibo Keita mjini Bamako, kumenyana na wenyeji, Mali katika mchezo wa marudiano Raundi ya pili ya mchujo wa kuwania tiketi ya Fainali za Vijana chini ya umri wa miaka 20 Afrika mwakani nchini Niger.
  Katika mchezo wa leo, Tanzania inahitaji ushindi wa kuanzia mabao 2-0 ugenini ili kusonga mbele, kufuatia kukubali kipigo cha mabao 2-1 kwenye mchezo wa kwanza Mei 13 Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Kipigo hicho kilitokana na Kocha Mkuu, Ammy Ninje kutompanga kipa namba moja, Ramadhani Kabwili ambaye alitofautiana naye kabla ya mchezo wa huo kutokana na kipa huyo kwenda klabu yake, Yanga nchini Algeria kwenye mechi ya ufunguzi ya Kombe la Shirikisho bila kuaga na akamfukuza kwenye timu. 

  Lakini Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia alimrejesha kipa huyo kikosini, akisema kilichotokea ni kukosekana kwa mawasiliano mazuri baina ya klabu ya Kabwili na uongozi wa timu na shirikisho.
  Kabwili alikuwa namba moja wa timu ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys iliyoshiriki fainali za U17 za Afrika nchini Gabon Mei mwaka jana, ambayo wachezaji wake wengi ndiyo wanaunda Ngorongoro.
  Na ndiye aliyedaka mechi zote mbili Ngorongoro ikiitoa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) katika Raundi ya Kwanza kwa penalti 6-5 mjini Kinshasa baada ya sare mbili za 0-0 nyumbani na ugenini, kabla ya kwenda kuokoa penalti kwenye mechi ya marudiano na kuivusha Ngorongoro hadi hatua hii.  
  Na Kabwili aliondoka peke yake kwenda Mali, siku moja baada ya wenzake kutangulia, kwa sababu aliruhusiwa kwenda kuichezea timu yake, Yanga kwenye mchezo mwingine wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Rayon mjini Dar es Salaam katikati ya wiki hii.    
  Mshindi wa jumla atakutana na mshindi kati ya Cameroon na Uganda katika hatua ya mwisho ya mchujo kuelekea Niger 2019. Kila la heri Ngorongoro Heroes. Mungu ibariki Tanzania. Amin.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KILA LA HERI NGORONGORO HEROES MJINI BAMAKO LEO MECHI NA MALI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top