• HABARI MPYA

    Saturday, May 12, 2018

    SIMBA SC YAENDELEZA SHANGWE ZA UBINGWA, YAIBAMIZA SINGIDA UNITED 1-0

    Na Mwandishi Wetu, SINGIDA
    SIMBA SC wameendeleza wimbi la ushindi katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya kuwachapa wenyeji, Singida United 1-0 katika mchezo wa ligi hiyo uliofanyika Uwanja wa Namfua jioni ya leo. 
    Pongezi kwake mfungaji wa bao hilo la leo, beki anayeweza kucheza kama kiungo pia, Shomari Salum Kapombe dakika ya 23 aliyefumua shuti baada ya kukutana na mpira uliookolewa na kipa wa Singida, Ally Mustafa ‘Barthez’ kufuatia shuti la Nahodha, mshambuliaji John Bocco. Ushindi huo unaifanya Simba SC ifikishe pointi 68 baada ya kucheza mechi 28 na kuzidi kuunenepesha ubingwa wake, iliyoutwaa rasmi Alhamisi baada ya mahasimu wao, Yanga kufungwa 2-0 na Tanzania Prisons mjini Mbeya. 
    Simba SC itateremka tena dimbani Mei 20 Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam kumenyana na Kagera Sugar katika mchezo ambao ndiyo watakabidhiwa taji lao la ubingwa wa Ligi Kuu kabla ya kwenda kuhitimisha msimu wa 2017-2018 kwa kumenyana na Maji Maji mjini Songea Mei 28.
    Mechi nyingine ya Ligi Kuu leo, Kagera Sugar wameichapa Njombe Mji FC mabao 3-1 Uwanja wa Kaitaba Bukoba. Mabao ya Kagera yamefungwa na Jaffar Kibaya, Edward Christopher na Japhet Makalai, wakati la Njombe limefungwa na Notikel Masasi. 
    Ushindi huo unaifanya Kagera Sugar ifikishe pointi 31 katika mechi ya 28 na kupanda kwa nafasi tatu hadi ya 10 wakati Njombe Mji FC inaendelea kuzibeba timu nyingine 15 zilizopo kwenye Ligi Kuu kwa pointi zake 22 za mechi 28 pia. Ligi Kuu itaendelea kesho kwa mechi mbili, Mtibwa Sugar wakiwakaribisha Yanga SC Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro na Mbeya City wakimenyana na Tanzania Prisons katika mechi ya mahasimu wa Jiji la Mbeya. 
    Kikosi cha Singida United kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Miraji Adam, Shafiq Batambuze, Malik Antiri, Juma Kennedy, Mudathir Yahya, Deus Kaseke/Kiggi Makasi dk88, Kenny Ally, Kambale Salita/Danny Usengimana dk56, Lubinda Mundia na Salum Chukwu. 
    Simba SC; Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein, Paul Bukaba, Yusuph Mlipili, Erasto Nyoni, James Kotei/Said Ndemla dk76, Jonas Mkude, John Bocco, Laudit Mavugo/Haruna Niyonzima dk51 na Emmanuel Okwi/Shiza Kichuya dk84.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC YAENDELEZA SHANGWE ZA UBINGWA, YAIBAMIZA SINGIDA UNITED 1-0 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top