• HABARI MPYA

    Wednesday, April 29, 2026

    NI SIMBA SC MABINGWA WA KOMBE LA MUUNGANO 2026


    TIMU ya Simba SC imefanikiwa kutwaa Kombe la Muungano 2026 baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya watani wao, Yanga SC usiku huu Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar katika mchezo wa Fainali uliodumu kwa zaidi ya dakika 120 kufuatia timu hizo kutofungana ndani ya dakika 90.
    Pongezi kwa mfungaji wa bao hilo pekee, mshambuliaji Suleiman Abdallah Mwalimu ‘Gomez’ anayecheza kwa mkopo kutoka Wydad Athletics ya Morocco, aliyemchambua kipa raia wa Mali, Djigui Diarra kwa mkwaju wa penalti dakika ya 120’+4 kufuatia Mzambia, Clatous Chota Chama kuangushwa kwenye boksi na Edmund Godfrey John, wote viungo washambuliaji.
    Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Hassan Mwinyi aliwakabidhi Kombe na mfano wa Hundi ya Sh. Milioni 150 mabingwa, Simba SC na mfano wa Hundi ya Sh. Milioni 120 kwa washindi wa pili, Yanga SC.
    Pamoja na ushindi huo, Simba SC imetoa Mchezaji Bora wa Mashindano, beki Rushine De Reuck, ambaye ni Mchezaji Bora wa Mechi, Kocha Bora Steven Robeet Barker wote raia wa Afrika Kusini, Mfungaji Bora, Suleiman Mwalimu Abdallah ‘Gomez’, Kipa Bora, Hussein Abel Thomas na Mchezaji Bora Chipukizi, beki Hussein Ally Mbegu, wote wazawa.
    Timu zote mbili zinarejea Dar es Salaam kwa ajili ya mchezo mwingine baina yao, wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara Jumapili kuanzia Saa 12:00 jioni Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni.   

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NI SIMBA SC MABINGWA WA KOMBE LA MUUNGANO 2026 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top