• HABARI MPYA

    Saturday, May 05, 2018

    MSUVA AWAIBUKIA YANGA KAMBINI ALGIERS KUWAPA NGUVU WAWAPIGE WAALGERIA KESHO

    Na Mwandishi Wetu, ALGER
    WINGA wa kimataifa wa Tanzania, Simon Happygod Msuva leo ametembelea kambi ya klabu yake ya zamani, Yanga SC mjini Algiers, Algeria.
    Msuva yupo huko na klabu yake ya sasa, Difaa Hassan El-Jadida ya Morocco ambayo usiku wa jana ililazimisha sare ya kufungana bao 1-1 na wenyeji, Mouloudia Club D'Alger Uwanja wa Julai 5, 1962 mjini Algiers katika mchezo wa kwanza wa Kundi B Ligi ya Mabingwa Afrika.
    Yanga nao wapo huko tangu jana kwa ajili ya mchezo wa kwanza wa Kundi D Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya wenyeji U.S.M. Alger utakaofanyika kesho usiku.
    Simon Msuva akiwa na wachezaji wa timu yake ya zamani, Yanga SC leo mjini Algiers 

    Msuva ambaye yupo katika msimu wake wa kwanza tu Difaa Hassan El- Jadidi tangu ajiunge nayo Juni mwaka jana kutoka kwa mabingwa wa kihistoria wa Tanzania, Yanga SC jana alicheza kwa dakika 87 kabla ya kumpisha kiungo Mmorocco, Houssine Khoukhouche kumalizia dakika tatu za mwisho.  
    Na wakati anaondoka uwanjani Msuva ambaye timu yake imepangwa Kundi B pamoja na Mouloudia Club D'Alger, E. S. Setifienne ya Algeria na TP Mazembe ya DRC tayari ilikuwa imekwishafungana 1-1 na MC Alger.
    Na walikuwa ni wageni, Difaa Hassan El-Jadidi waliotangulia kwa bao la mshambuliaji Mmorocco mwenye umri wa miaka 23, Hamid Ahadad dakika ya 77, kabla ya Amir Karaoui kuwasawazishia wenyeji, MC Alger dakika ya 82.
    Mechi nyingine za ufunguzi hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika jana, Al Ahly ililazimishwa sare ya 0 – 0 na ES Tunis Uwanja wa Borg El Arab mjini Alexandria mna bao pekee la Lemponye Tshireletso dakika ya 36 limetosha kuipa ushindi wa 1-0 Township Rollers dhidi ya KCCA ya Uganda Uwanja wa Taifa wa Gaborone nchini Botswana.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MSUVA AWAIBUKIA YANGA KAMBINI ALGIERS KUWAPA NGUVU WAWAPIGE WAALGERIA KESHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top