• HABARI MPYA

    Thursday, January 17, 2013

    KIIZA HATARINI KUWAKOSA BLACK LEOPARD KESHOKUTWA

    Kiiza

    Na Mahmoud Zubeiry
    MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Uganda, Hamisi Kiiza na beki mzalendo, Juma Abdul wako hatarini kuukosa mchezo wa keshokutwa wa kirafiki wa timu yao, dhidi ya timu ‘tishio’ kutoka Afrika Kusini, Black Leopard kutokana na kuwa wagonjwa.
    Wawili hao wanasumbuliwa na Malaria na leo wameshindwa kufanya mazoezi na wenzao kujiandaa na mchezo huo unaotarajiwa kuwa ‘mkali na wa kusisimua’.
    Mabingwa hao wa soka Afrika Mashariki na Kati, Yanga SC ya Dar es Salaam Jumamosi hii watashuka kwenye Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam kumenyana na Black Leopard ya Polokwane, Limpopo nchini Afrika Kusini.
    Yanga ilikuwa Uturuki kwa wiki mbili kwa kambi ya mazoezi na ilirejea Jumapili Alfajiri nchini. Katika ziara yake hiyo, ilicheza mechi tatu za kujipima nguvu na kufungwa mbili na kutoka sare moja.
    Katika mchezo wake wa kwanza, ilitoka sare ya 1-1 Ariminia Bielefeld ya Daraja la Tatu (sawa na la nne) Ujerumani kabla ya kufungwa 2-1 na Denizlispor FC ya Daraja la Kwanza Uturuki na baadaye 2-0 na Emmen FC ya Ligi Daraja la Kwanza Uholanzi.
    Yanga iliweka kambi katika hoteli ya Fame Residence Lara & Spa kilomita chahce kutoka katika Uwanja wa Ndege wa Jiji la Antalya, iliyopo ufukweni mwa bahari ya Mediteranian.
    Kikosi cha wachezaji 27 kilikuwa kambini nchini Uturuki, ambacho ni makipa; Ally Mustafa 'Barthez', Said Mohamed na Yussuf Abdul, mabeki Juma Abdul, Shadrack Nsajigwa, Godfrey Taita, Stefano Mwasyika, Oscar Joshua, Mbuyu Twite, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Ladisalus Mbogo na Kelvin Yondani.
    Viungo ni Athumani Iddi ‘Chuji’, Frank Domayo, Haruna Niyonzima, Kabange Twite, Nurdin Bakari, Omega Seme, Simon Msuva, Rehani Kibingu, Nizar Khalfani na David Luhende wakati washambuliaji ni Didier Kavumbagu, Said Bahanunzi, Jerry Tegete, George Banda na Hamisi Kiiza na Kocha Mkuu Mholanzi, Ernie Brandts, Kocha Msaidizi, Freddy Felix Minziro na Kocha wa makipa na Razak Ssiwa.
    Hiyo inakuwa mara ya tatu kihistoria Yanga kufanya ziara nje ya Afrika baada ya Brazil mwaka 1975 na Romania mwaka 1978. Yanga pia imewahi kuweka kambi Afrika Kusini mwaka 2008.
    Leopards ilirejea Ligi Kuu ya Afrika Kusini mwaka juzi tangu ishuke 2008 na msimu uliopita iliponea chupuchupu kushuka tena, baada ya kushika nafasi ya 14 katika Ligi ya timu 16, na kwa msimu huu hadi sasa ipo nafasi ya 12.
    Katika mechi 15 zilizopita za klabu ya Black Leopard, imemudu kushinda mechi mbili tu, nyingine zote imefungwa na kutoka sare. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: KIIZA HATARINI KUWAKOSA BLACK LEOPARD KESHOKUTWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top