![]() |
| Na Bin Zubeiry |
ALIPOKUJA Mwanasoka Bora wa zamani Afrika, Abedi Ayew ‘Pele’
nchini Novemba mwaka jana, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilimtembeza
katika maskani ya klabu moja tu, Azam FC huko Mbade, eneo la Chamazi, nje
kidogo ya Dar es Salaam.
Hii ni klabu ambayo ilianzishwa tu mwaka 2004 na kucheza Ligi
Kuu ya nchi kwa mara ya kwanza mwaka 2008.
Ni klabu ambayo haina historia yoyote katika soka ya
Tanzania, haijawahi hata kuchukua taji moja la ubingwa wa Ligi Kuu na haina
mashabiki, zaidi ya kukwepa kusema inamilikiwa na familia ya kitajiri ya Said
Salim Awadh Bakhresa, mfanyabiashara mwenye historia ya kipekee.
Lakini kwa nini TFF ilimpeleka Pele Chamazi na si kwenye
maskani za klabu kongwe nchini na za kihistoria, Simba na Yanga za katikati ya
Jiji la Dar es Salaam? Hilo ndilo swali ambalo bila shaka wengi walijiuliza.
TFF iliipendelea Azam? Hapana. Narudia kusema hapana.
Haikutaka fedheha na kumpotezea muda Balozi huyo wa Shirikisho la Soka la
Kimataifa (FIFA).
Kwa sababu TFF inajua hakuna cha maana ambacho Pele angekwenda
kukiona Msimbazi yalipo maskani ya Simba au Jangwani kwa Yanga.
Simba na Yanga kwa sasa hazina mvuto na zaidi zinajivunia tu
huo udhamini wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), uliowawezesha kupata mabasi
matatu kila timu, yakiwemo makubwa kabisa ya kisasa.
Lakini ajabu, hadi kufika mwaka 1975, klabu za Simba na Yanga
zilikuwa tayari zina majengo mazuri, magari na hadhi kubwa- na wakati huo
waliokuwapo walitabiri miaka 20 baadaye klabu hizo zitakuwa mbali zaidi
kimafanikio.
Hayakuwa mafanikio ya kiuchumi tu, bali hata soka- hicho ndio
kipindi ambacho Simba na Yanga zilikuwa moto wa kuotea mbali katika michuano ya
Afrika.
Yanga ilicheza Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika mara mbili
mfululizo mwaka 1969 na 1970, mara zote ikitolewa kwa mbinde na Asante Kotoko
ya Ghana, wakati Simba ilifika Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika na kutolewa
na Mehallal El Kubra ya Misri mwaka 1974.
Simba na Yanga ziliendelea kuwa tishio kisoka na kipindi
hicho ilishuhudiwa zikifanya ziara za mafunzo Ulaya na Amerika.
Ilitabiriwa miaka 20 baadaye, mambo yatakuwa mazuri zaidi
kwenye klabu hizo, lakini kutoka mwaka 1975 hadi leo sasa ni miaka 38 imepita,
hali ikoje Simba na Yanga?
Ni mbaya, mbaya kabisa, majengo yamechakaa, magari hakuna
tena zaidi ya yale ya msaada kutoka TBL, yanayotokana na mkataba wao wa
udhamini. Yanga ambayo ilikuwa juu zaidi kwa kuwa na mabasi, majengo zaidi ya
matatu, Uwanja wa Kaunda, sasa imebaki na jengo moja ambalo lilifanyiwa
ukarabati hivi karibuni na Yussuf Manji, pale Jangwani, japokuwa tayari limeanza
kuharibika.
Uwanja wa Kaunda umechoka, umechakaa kwa sababu hauna matunzo
na haufai kwa matumizi, hali inayosababisha klabu iingie gharama kukodi viwanja
kwa mfano kwa sasa katika sekondari ya Loyola, Mabibo, Dar es Salaam.
Hakuna taarifa za uhakika kuhusu majengo mengine ya klabu
kama lile la Mtaa wa Mafia, lile la Tandale na ile nyumba ya NHC ambayo awali
aliishi Profesa Victor Stanslescu, baadaye Tambwe Leya, kabla ya Charles
Boniface Mkwasa. Leo Yanga inaingia gharama kuwapangia nyumba makocha wake,
wakati wana nyumba yao waliyopangishiwa na NHC pale Fire, wamepokonywa?
Najaribu kutafakari hali ndani ya Yanga ingekuwaje kama
asingejitokeza Manji mwaka 2006 na kujitolea kwa hali na mali kuisaidia klabu
hiyo, kwa kweli sipati jibu mambo yangekuwaje.
Aliingia baada ya jitihada zilizofanywa na wanachama wa klabu
hiyo akina Theonist Rutashoborwa (sasa marehemu), Mzee wa Mpunga, Mawakili
Lugaziya na Matunda na baadhi ya waandishi wa habari za michezo wenye mapenzi
na klabu hiyo, kuanzisha harambee ya Saidia Yanga, kufuatia hali mbaya ya
kiuchumi kukithiri ndani ya klabu hiyo, chini ya uongozi wa Francis Kifukwe.
Katika kutafuta misaada ya kuibeba timu wakati huo ipo kwenye
michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame
ndipo wakampata Manji naye kwa mapenzi yake, akasema; “Nitaubeba mzigo wote”,
na kweli hadi leo, amekuwa akiilea Yanga na sasa ameamua kabisa kuwa Mwenyekiti.
Wafadhili wamekuwa wakiingia na kutoka kwenye klabu hizi
tangu miaka ya 1990 na wamekuwa wakisaidia mno, angalau Simba wamekuwa
wakitumia vizuri fursa ya ufadhili, lakini kwa Yanga zaidi wamekuwa wakiwageuza
‘mabuzi’ tu wafadhili wao.
Zama za ufadhili wa Azim Dewji, Simba ilifika fainali ya
Kombe la CAF mwaka 1993, zama za ufadhili wa Mohamed Dewji, Simba ilicheza
hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2003, ikiitoa Zamalek
iliyokuwa inashikilia taji. Haya sasa, Yanga watuambie walifanya nini wakati
wanafadhiliwa na Abbas Gulamali kwa pamoja na Murtaza Dewji au wakati huu
wanaogelea kwenye bwawa la fedha za Manji, kiasi cha kufanhya ziara ya Uturuki,
wanafanya nini?
Narejea nyuma miaka ile Yanga iko chini ya Mwenyekiti Mangara
Tarbu namna ilivyopata mafanikio ya haraka ya uwanjani na kiuchumi kama Simba
ilipokuwa chini ya akina Mwenyekiti Dumelezi na Katibu Mkuu Said Mpolaki, naona
kabisa kizazi kipya kimeshindwa kuzivusha katika hatua nyingine klabu hizi.
Binafsi sijali kujiongezea watu wa kunichukia kwa kuandika
ukweli juu ya soka ya nchi hii na sitarudi nyuma; wamepita watu wengi ndani ya
miongo hii miwili, lakini hakuna chochote kilichofanyika na kila siku
kinachojitokeza ni afadhali ya waliokuwapo.
Umefika wakati serikali iingilie kati kuziokoa hizi klabu,
kwani ni rasilimali za taifa hizi iwapo zitatumika vizuri. Zitatoa ajira kwa
vijana, zitachangia pato la taifa kwa kodi, ikiwa tu zitakuwa chini ya
usimamizi imara wenye tija.
Leo Waingereza wamekubali timu zao zimilikiwe na wageni na
sasa timu zote kubwa zinamilikiwa na wageni, lakini kwa sababu wenyewe haswa
wenye timu wanachotaka ni furaha, wanaangalia mambo ya msingi mawili; klabu
inanufaika kiuchumi, inapata mafanikio uwanjani? Inatosha.
Manchester United, ama Chelsea FC, au Arsenal hata Liverpool,
hazina makomandoo. Hazina ombaomba wa kuomba fedha viongozi. Hazina watu
wanaolilia wapewe nafasi ya kuuza tiketi wala kusimama milangoni. Zina watu
ambao wanataka ushindi na kusikia klabu inaigiza fedha.
Hata kwetu Tanzania, mashabiki wa kweli wa timu hizi ni wale
wanaonunua tiketi kwenda uwanjani kushangilia timu zao. Wanachotaka ni ushindi
na kusikia klabu zao zinapata mafanikio na kuwa sawa na klabu nyingine
zilizopiga hatua kubwa kiuchumi na kisoka Afrika.
Lakini inasikitisha kuona miongo miwili imekatika Simba na
Yanga zinazidi kutumbukia kwenye dimbwi la umasikini wa soka na uchumi, kwa
sababu gani tusiwakumbuke akina Mangara na Dumelezi, waliozijengea klabu hizi
misingi imara ya kisoka na uchumi? Wakubwa wa leo wanabadilisha suti na magari
ya Kijapani, lakini klabu zinanuka uvundo, zinatia kichefuchefu. Wapo kwa ajili
ya kusaka umaarufu tu, hawana cha maana wanachofanya.
Angalau sasa Manji ameingia pale Yanga, naamini atasababisha
mabadiliko makubwa na nitafurahi Mohamed Dewji naye akigombea Uenyekiti Simba
katika uchaguzi ujao, kwa sababu atasaidia mno kuimarisha klabu hiyo na
upinzani wa jadi wa klabu hizo, ambao ni chachu ya msisimko wa soka yetu. Wasalam!!



.png)