• HABARI MPYA

    Saturday, January 19, 2013

    ABBEL DHAIRA: Ngongoti aliyetua Simba kumsaidia kazi Juma Kaseja

    Abbel Dhaira

    Na Doris Maliyaga, Muscat
    SIMBA imemnasa kipa imara tegemeo wa Taifa la Uganda, Abel Dhaira kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara na michuano mingine.
    Ujio wa kipa huyo katika kikosi cha Simba kutaleta uhai mpya kwenye eneo hilo kutokana na uwezo wake katika kulinda lango.
    Dhaira atakuwa kipa mrefu zaidi kwenye Ligi Kuu Bara kwani kwani ana urefu wa zaidi ya futi 6.5.
    Mbali na urefu alionao, amejengeka vizuri kimazoezi na ana umbo linalomfanya atishe awapo langoni.
    Kwa mdau wa soka wa Tanzania, utamkumbuka Dhaira katika mashindano ya Kombe la Chalenji 2011.
    Dhaira ndiye alikidakia kikosi cha timu ya taifa ya Uganda 'The Cranes' katika mashindano hayo na wao wakachukua ubingwa katika ardhi yao.
    Uhodari wake wa kupangua michomo ya penalti ndiyo iliwapa ubingwa huo katika mchezo wa fainali walipocheza na Rwanda jijini Dar es Salaam. Uganda ilishinda kwa mikwaju ya penalti 3-2 ambayo Dhaira aliiokoa baada ya matokeo ya awali kuwa sare ya mabao 2-2.
    Hakung'ara katika mashindano ya Chalenji mwaka 2012 kutokana na kuwa majeruhi. Dhaira alipata majeruhi katika mechi ya kwanza hatua ya makundi dhidi ya Ethiopia.
    Aliumia jicho la kushoto dakika ya 73 ya mchezo huo na kumfanya akose michuano hiyo ambayo Uganda ilitetea taji lake.
    Wakati wa michuano hiyo ya Chalenji, Simba ilipata mwanya na kuzungumza naye akatua klabuni kwao kwa ajili kuisaidia klabu hiyo katika Ligi Kuu na mashindano mengine kama Ligi ya Mabingwa Afrika.
    Akiwa kikosini hapo, Dhaira atasaidiana na makipa wengine, Juma Kaseja, Wilbert Mweta na Wazir Hamad.
    Kumbuka Kaseja ndio amekuwa nguzo ya Simba tangu mwaka 2003 ingawa alihama msimu wa 2008/09 na kujiunga na Yanga.
    Kaseja, hata hivyo, alirejea Simba msimu uliofuata na ndio kinara wa timu hiyo hadi sasa.
    Ujio wa Dhaira ni changamoto kubwa kwa Kaseja, ambaye hajapata ushindani mkubwa wa namba tangu ameanza kuchezea timu hiyo.
    Dhiara ambaye ana miaka 26 sasa, udogo wa umri alionao na kiwango chake wanaweza kunufaika kwa namna nyingi katika udakaji wake.
    Mara baada ya kufika Tanzania kujiunga na kikosi chake, Mwanaspoti ilifanya mahojiano naye kwa kina naye alieleza sababu ya kutua Tanzania.

    Sababu ya kutua Simba
    "Simba ni klabu kubwa lakini pia maslahi, tumekubaliana ndiyo maana nimekuja hapa na naahidi kuitumikia kwa moyo mmoja kuona inafanya vizuri katika michuano mbalimbali itakayoshiriki,"anasema Dhaira.

    Utendaji wake Simba
    "Mungu ni kila kitu. Nimekuja kucheza Simba nikiwa na matumaini ya kufanya vizuri na naamini kila kitu kitakwenda sawa.
    "Najiamini na nimejipanga vizuri kuona naifanyia Simba kazi nzuri kwa sababu kufanya kwangu vizuri ni kawaida.
    "Nimekuwa bora katika ligi ngumu ya Iceland nikiwa na IBV msimu uliopita kwa hiyo sioni kama kutakuwa na cha ajabu kitakachonifanya nishindwe kufanya kazi hapa,"anaeleza Dhaira huku akijiamini.
    Kuhusu ushindani wa namba: "Ushindani upo kila mahali na hakuna chenye kushindikana mbele ya Mungu, hayo ni mambo ya kawaida kabisa kwa mchezaji.
    "Sina wasiwasi na jambo lolote ninachofanya ni kutimiza majukumu ya kazi yangu iliyonileta,"anasisitiza Dhaira.
    Hata hivyo, Dhaira anasisitiza jambo moja juu ya mashabiki wa kikosi hicho kwa kusema: "Nitafanya vizuri lakini mashabiki wa soka wa Simba na wengine wote, wanipe muda katika kipindi hiki kama wiki mbili ili niwe vizuri.
    "Unajua nimekuwa mgonjwa kwa kipindi kirefu kutokana na tatizo la jicho (anaonyesha) nikawa nafanya mazoezi lakini si ya nguvu si unajua kuumwa tena.
    "Kwa sasa kwa sababu nimepona, nataka kufanya ya nguvu zaidi ili niwe vizuri na kufanya kazi yangu kwa malengo.
    "Mashabiki wasiwe na wasiwasi na mimi kikubwa nahitaji ushirikiano wao wa hali na mali ili mambo yaende vizuri."

    Historia
    Dhaira amecheza soka katika mataifa mbalimbali kama Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na Iceland kabla ya kujiunga na Simba msimu huu.
    Akiwa na Uganda ambako ndiko kwao, aliichezea Express 2006-2008 ambapo klabu hiyo ilichukua ubingwa wa Uganda maarufu kama Uganda Cup mara mbili mfululizo.
    Baada ya hapo alihamia URA ambako pia walichukua ubingwa wa Ligi Kuu Uganda maarufu kama Uganda Premier League msimu wa 2009 na msimu huo ndiyo akatimkia Congo kuichezea klabu ya AS Vita.
    Akiwa na AS Vita walishiriki Kombe la Shirikisho hata hivyo walitolewa hatua ya awali na 2011 aliachana na Ligi Kuu Congo na akajiunga na IBV ya Iceland ambako alikuwa akicheza na kiungo, Tonny Mawejje ambaye pia ni raia wa Uganda lakini mwenzake ametolewa kwa mkopo kwenda Golden Arrows ya Afrika Kusini.
    Mwaka 2013 amejiunga na Simba kwa mkataba wa miaka miwili kwa ajili ya Ligi kuu Bara na michuano mingine inayowakabili.

    WASIFU WAKE:
    JINA: Abbel Dhaira
    KUZALIWA: Septemba 9, 1987
    ALIPOZALIWA: Jinja, Uganda
    NAFASI: Kipa
    KLABU ALIZOCHEZEA:
    Mwaka                      Klabu
    2006-2008:              Express (Uganda)
    2008-2010:              URA (Uganda)
    2010-2011:              AS Vita (DRC)    
    2011-2012:              IBV      (Iceland)
    Kuanzia 2013:          Simba SC
    (Tangu mwaka 2009, ameidakia Uganda mechi 21)
    MAKALA HII IMETOKA GAZETI LA MWANASPOTI LEO
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: ABBEL DHAIRA: Ngongoti aliyetua Simba kumsaidia kazi Juma Kaseja Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top